Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mfahamu Alain-Guillaume Bunyoni, Waziri Mkuu mpya wa Burundi
Siku moja baada ya bunge la Burundi kumuidhinisha Alain Guillaume Bunyoni kuwa Waziri Mkuu wa Burundi katika utawala wa rais Evariste Ndayinsimiye gumzo limeibuka kuhusu hatua hiyo.
Ofisi ya Waziri Mkuu ilifutwa nchini Burundi mwaka 1998.
Alain-Guillaume Bunyoni mtu anayefahamika sana nchini Burundi kutokaa na mamlaka aliyonayo ndani ya utawala wa chama tawala cha CNDD-FDD tangu mwaka 2005, na sasa amechaguliwa kuchukua cheo cha Waziri Mkuu ambacho mara ya mwisho kilikuwepo miaka 22 iliyopita.
Mara ya mwisho kiti hicho kiliachwa na Pascal Ndimira Firmin aliyehudumu chini ya ya utawala wa rais wa pili Pierre Buyoya.
Alain-Guillaume Bunyoni nani hasa?
Alain-Guillaume Bunyoni amwenye umri wa miaka 48, si mgeni katika ulingo wa siasa na usalama nchini Burundi, kwani alikua Waziri wa usalama kuanzia mwaka 2015.
Alizaliwa katika Wilaya ya Kanyosha iliyopo katika mji mkuu Bujumbura.
Alisomea katika Chuo Kikuu cha Burundi mwaka 1994, lakini hakuweza kuendelea na masomo kwani alijiunga na wapiganaji wa FDD mwaka 1994 katika vita vilivyoibuka nchini Burundi, baada ya kuuawa kikatili kwa aliyekua rais wa nchi Melchior Ndadaye hadi pale chama cha CNDD-FDD kilipofikia makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka 2003.
Bwana Bunyoni ni mtu aliyeshikilia nyadhfa tofauti wakati chama cha CNDD-FDD kilipoingia madarakani, na baadae kupata ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2005.
Kati ya 2004 na 2005, yalipewa mamlaka ya kuongoza idara mpya ya polisi ambapo alipewa jukumu la kufanya mabadiliko mapya ndani jeshi la polisi.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2007 aliteuliwa kuwa mkuu wa polisi nchini Burundi.
Kuanzia mwaka 2011 hadi 2014, Alain-Guillaume Bunyoni aliteuliwa kuwa, mkuu wa kitengo kinachoshughulikia matatizo ya raia katika ofisi ya rais.
Brigadia Jenerali Alain Guillaume Bunyoni aliapishwa kama waziri wa Burundi wa usalama wa umma na udhibiti wa maafa tarehe 24 Aprili.
Aliangaliwa kama mtu wa pili mwenye mamlaka zaidi baada Pierre Nkurunziza.
Baada ya kuhudumu kama kiongozi wa wanamgambo katika kikundi cha waasi wa CNDD-FDD pamoja na President Pierre Nkurunziza kati ya mwaka 1993 na 2003, aliteuliwa kuwa mkuu wa polisi wa Burundi mwishoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005.
Alihudumu kama waziri wa usalam wa umma kati ya mwaka 2007 na 2011.
Bunyoni anafahamika kuwa na mchango mkubwa katika kuzima mwamko wa mwaka 2015 wa kupinga azma ya Pierre Nkurunziza ya kuwania muhula wa tatu.
Brigadia Jenerali Bunyoni, ni mmoja wa viongozi wenye mamlaka zaidi CNDD-FDD, anayetuhumiwa kwa kufanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika ghasia za kisiasa zilizoibuka mwaka 2015.
Mbali na siasa pamoja na jeshi, Brigadia Bunyonyi anayetambuliwa na wengi kama anayependa maisha ya raha na ya hali ya juu kwa kumiliki mali za thamani kubwa, kama vile nyumba kubwa, magari makubwa:
Ni mmoja wa watu waliowekewa vikwazo na Marekani vilivyowekwa chijdi ya utawala wa Pierre Nkurunziza kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi.
Mwaka 2017 serikali ya Burundi ilijiondoa katika uanachama wa Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai baada ya mahakama hiyo kutangaza kufanya uchunguzi wa makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu yaliyofanyika nchini Burundi kuanzia mwaka 2015.
Wachambuzi wa siasa za Burundi wanasema kurejeshwa kwa kiti cha Waziri Mkuu nchini Burundi baada ya miaka 22 kuondolewa ni hatua ya kugawanya madaraka miongoni mwa wakuu wa zamani wa waasi wa CNDD-FDD waliochukua mamlaka mwaka 2005, kwani rais mpya Bwana Evariste Ndayishimiye na Bwana Bunyoni wanaangaliwa kama watu waliokua wafuasi wa rais Nkurunziza.