Uchaguzi Marekani 2020: Trump adaiwa kuomba usaidizi wa rais Xi Jinping kushinda uchaguzi ujao

John Bolton - 15 June

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Bwana Bolton amekanusha kwamba kitabu hicho kina taarifa nyeti

Rais wa Marekani Donald Trump alijaribu kuomba msaada wa rais wa China Xi Jinping ili kushinda awamu ya pili ya urais, mshauri wa zamani wa Trump wa Usalama wa Taifa John Bolton ameeleza katika kitabu chake kipya.

Bolton amesema Trump aliitaka China kununua bidhaa za chakula kutoka kwa wakulima wa Marekani, kwa mujibu wa maelezo ya awali ya kitabu ambacho kimeanza kuchambuliwa na vyombo vya habari nchini Marekani.

Mwandishi wa kitabu pia anasema Trump "alisalia kuwa mbumbumbu wa namna ya kuendesha ikulu ya White House".

Serikali ya Trump inajaribu kuzuia kitabu hicho kuingia sokoni.

Tahadhari: Taarifa hii huenda ikawa yenye maneno makali kwako

Je kitabu hicho kinaweza kuzuiliwa?

Kitabu cha bwana Bolton chenye kurasa 577 kiitwacho The Room Where It Happened (Chumba ambacho yalitokea) kinatarajiwa kuanza kuuzwa Juni 23.

Hata hivyo, Jumatano usiku, Wizara ya Sheria ya Marekani ilipeleka maombi ya dharura kwa jaji wa mahakama kuzuia uzinduzi wa kitabu hicho.

Mchapishaji wa kitabu hicho kampuni ya Simon & Schuster, imeeleza: "Maombi ya leo ya serikali hayana uzito na yamechochewa kisiasa."

Imesema maelfu ya nakala za kitabu hicho tayari zimeshasambazwa sehemu mbalimbali ulimwenguni na pingamizi la serikali halitafua dafu.

Kwa upande mwengine, Trump alipiga simu katika runinga ya Fox News na kueleza kuwa: "Bolton amevunja sheria. Hizi ni taarifa za siri na hakupata kibali cha kuzitoa."

"Alikuwa ni mtu ambaye amekwisha kabisa," aliongeza rais Trump. "Nilimpatia nafasi ."

Bolton ambaye anatajwa kuwa mfuasi wa sera za kimataifa za mabavu Ali kiungo na Ikulu ya White House Aprili 2018 na kuondoka Septemba 2019.

Awali Bolton alitangaza kuwa aliamua kujiuzulu nafasi yake, lakini Trump alisema kuwa alimfukuza kwa kuwa alikuwa anapingana naye vikali.

Bolton anadai nini kilitokea katika mkutano na Xi?

Madai ya Bolton ni kuwa mazungumzo hayo yalifanyika baina ya rais Trump na rais Xi katika mkutano wa G20 jijini Osaka, Japani Juni 2019.

Rais wa China alilalamika kuwa wakosoaji nchini Marekani walikuwa wanachochea vita baridi baina ya mataifa hayo mawili, bw Bolton anaeleza kwenye kitabu kama ilivyochapishwa kwenye gazeti la New York Times.

Close aides of the president considered resigning in disgust or frustration, Mr Bolton alleges

Chanzo cha picha, Getty Images

Bolton anaeleza kuwa Trump aliamini Xi alikuwa akiwazungumzia wanasiasa wa chama hasimu cha Trump cha Democrats.

"Trump, kwa shauku, akageuza mazungumzo hayo na kuwa juu ya uchaguzi ujao wa urai Marekani [ Novemba 2020], na kugusia kuhusu uwezo wa kiuchumi wa China na kumuomba Xi amsaidie kushinda," Bw Bolton ameeleza.

"Alisisitiza umuhimu wa wakulima na kuongezeka kwa manunuzi ya China ya magaharage ya soya na ngano kutakuwa na mchango wa matokeo ya uchaguzi."

Baada ya rais Xi kukubali kufanya majadiliano ya manunuzi ya bidhaa za wakulima kuwa kipaumbele katika majadiliano ya kibiashara ya nchi hizo mbili, Trump akamsifu kuwa "kiongozi bora zaidi katika historia ya China."

Mwakilishi wa kibiashara wa Marekani Robert Lighthizer amekanusha maelezo ya Bolton na kudai kuwa hakukutolewa ombi lolote la msaada wa uchaguzi.

Bw Bolton pia ameeleza kuhusu mazungumzo ya chakula cha jioni wakati wa ufunguzi wa mkutano wa G20 kuhusu ujenzi wa kambi katika jimbo la magharibi la Xinjiang.

Trump alisema ujenzi huo uendelee kwa kuwa "lilikuwa jambo sahihi kufanyika".

China imewazuia takribani watu milioni moja kutoka jamii ya waislamu ya Waiuighur kama adhabu ama kuwafundisha itikadi za serikali katika kambi hizo.

Utawala wa Trump umeikosoa China hadharani juu namna jamii ya Uighur inavyotaabishwa, na Jumatano wiki hii rais Trump amesaini sheria ya kuwawekea vikwazo maafisa wanaowakandamiza raia waislamu katika jimbo la Xinjiang.

Mpinzani wa Trump kutoka chama cha Democrats katika uchaguzi wa Novemba, bwana Joe Biden, ameeleza kuhusu kitabu hicho kuwa: "Kama maelezo haya ni ya kweli, si tu kwamba ni jambo ambalo halikubaliki kimaadili bali pia ni ukiukaji wa wa Donald Trump wa majukumu yake kwa Wamarekani."