Virusi vya Corona: Mabenki Tanzania yaelekezwa kutoa ahueni kwa wakopaji wao

Benki Kuu ya Tanzania imetoa maelekezo kwa mabenki na makampuni ya simu juu ya namna ya kutoa unafuu wa masuala ya kifedha kwa wateja wao

Kwa upande wa mabenki, Benki Kuu imeyaagiza kufanya mjadala na wateja wao juu ya urejeshwaji wa mikopo na kutafuta namna nafuu ya urejeshaji wa mikopo hiyo

"Benki Kuu itatoa unafuu kwa mabenki na taasisi za fedha zitakazotoa unafuu katika urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa kuzingatia uwazi na bila upendeleo," imeongeza taarifa kutoka Benki ya Dunia

Kwa upande wa makampuni yanayotoa huduma za kifedha kwa njia ya mitandao, Benki Kuu imeagiza kuongezwa kwa kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka TSh 3,000,000 (Milioni 3, sawa na takribani $1300) hadi Tsh 5,000,000 (Milioni 5, sawa na takribani $2,160)

Maelekezo yametolewa pia juu ya kuongezwa kwa kiwango cha akiba kwa siku kwa mteja kutoka Tsh 5,000,000 (Milioni 5, sawa na takribani $2,160)

Hadi Tsh. 10,000,000 (takribani $10,000,000)

Benki Kuu imesema sababu ya kuchukuliwa kwa hatua hii ni kumsaidia mteja na mwananchi kwa ujumla kupunguza ulazima wa kwenda katika mabenki kupata huduma za kifedha

Sera hii ya kifedha inakuja takribani miezi miwili tangu mgonjwa wa kwanza wa homa kali ya mapafu (COVID-19) kugundulika nchini.

Ikilinganishwa na nchi zingine kama vile Kenya, Benki Kuu nchini humo ilitangaza hatua kama hizi katikati ya mwezi Machi, siku chache tu baada ya maambukizi kugundulika nchini humo.

Taarifa hiyo kutoka Benki Kuu imesisitiza pia kwamba Tanzania bado ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kuwezesha uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.

Jinsi mataifa mengine yalivyochukua hatua za kuwapatia ahueni raia wake

Ghana

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo alitangaza kuwa serikali yake italipia gharama ya maji kwa kipindi cha miezi mitatu ikiwa ni jitihada za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Wafanyakazi wote wa afya hawata katwa kodi katika kipindi cha miezi hiyo mitatu.

Kuosha mikono kwa sabuni na maji, Maji yanatajwa kuwa namna nzuri ya kukabiliana na maambukizi.

Matenki ya maji pia yatakuepo kutoa huduma ya maji kwa wananchi wasio na uwezo.

Kwa sasa wafanyakazi wa afya wanao wahudumidia wagonjwa wa Covid-19 wataongezewa mshahara kwa asilimia hamsini.

DR Congo

Shirika la maji na shirika la umeme nchini DR Congo yamethibitisha kufuata agizo la serikali kwa kutoa huduma ya maji ya bila malipo pamoja na umeme kwa kipindi cha miezi miwili.

Mkurugenzi wa shirika la umeme bwana Jean-Bosco Kayombo, alisema kuwa watakaofaidika na huduma hiyo ya umeme na maji ya bila malipo, ni nyumba za watu na wafanyabiashara wadogo na wenye viwanda vya wastani ili kupunguza uwezekano wa maambukizi kuenea zaidi.

Serikali ya Kongo imesema kuwa imeamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu watu hawaendi kazini kwa sasa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.

Kenya

Gavana wa benki kuu Kenya, bwana Patrick Njoroge anasema kuwa wataweka mikakati ya kuimarisha uchumi katika kipindi hiki cha athari za kiuchumi ambazo zinawakumba wateja wao kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Katika harakati za kuokoa uchumi binafsi, bwana Njoroge ametaka mikopo ya ujenzi kutolewa kwa wastani.

Vilevile rais pamoja na makamu wake, wametaka mishahara yao ikatwe kwa asilimia ishirini.

Uganda na Rwanda wanatoa huduma ya chakula kwa raia wenye uwezo wa chini.