Virusi vya Corona: Fahamu taarifa ghushi ambazo zimesambaa Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchi za Afrika zimeonesha kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona na serikali nyingi kwasasa zinachukua hatua kali kuhakikisha watu hawakaribiani.
Wakati ambapo nchi hizo zinaendelea kujiweka tayari katika kukabiliana na ongezeko la visa vya virusi vya corona, taarifa za kupotosha zimeendelea kusambaa kote barani humo.
1. Video hii haioneshi kwamba Waafrika wanashambuliwa nchini China
Kuna video iliysambaa kwenye mitandao ya kijamii inayoonesha raia wa Afrika wakivamiwa katika mitaa ya China. Hili linawadia wakati ambapo jamii za Afrika zinashtumiwa kwa kusambaza virusi hivyo.
Mwanablogu wa Kenya kwenye mtandao wa Twitter na mingine kama YouTube na Facebook, alisambaza taarifa moja iliyokuwa na kichwa:" Wanandoa wa Kenya wapigana na wanandoa wa China katika mji wa Wuhan.... ni kuendelea kuishi kwa walio na nguvu."
Taarifa za video hiyo pia zilitumika katika kituo kimoja cha runinga nchini Kenya.

Tatizo ni kwamba video hiyo ilichukuliwa mji wa New York wala sio China.
Kwenye mtandao wa Twitter, video hiyo inaambatanisha taarifa za maeneo mengine yaliyokaribu na mji wa New York katika maelezo mafupi yanayopita chini ya video ikiwemo hospitali ya St Barnabas na barabara ya Fordham.
Kwa kutumia programu ya mtandao wa google ya Google Street View, unaweza kuona kituo kimoja chenye mashine ya kutolea pesa na hospitali vyote vikiwa vinajitokeza kwenye video hiyo.
2. Kunywa pombe hakukulindi dhidi ya ugonjwa wa Covid-19
Gavana wa mji wa Nairobi nchini Kenya, amekesolewa kwa matamshi yake ya kupotosha kuhusu pombe na virusi vya corona.
Gavana Mike Sonko alikuwa anaelezea kwanini anajumuisha pombe aina ya Hennessy cognac kwenye chakula anachosambaza kwa watu wasiojiweza mjini humo, akisema kwamba itasaidia kama "kitakasa cha koo" yaani "throat sanitiser".
"Kuanzia kwenye utafiti ambao umefanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi mashirika mengine ya afya imebainika kwamba pombe inajukumu muhimu katika kuua virusi vya corona, au virusi vingine vyovyote vile," gavana huyo alisema.

Inaonekana kwamba alielewa vibaya ushauri wa afya wa Shirika la Afya Duniani ambao unasema, kunywa pombe hakukulindi dhidi ya virusi vya corona lakini inaangazia vitakasa mkono vyenye pombe katika unawaji wa mkono ili kuondoa viini.
Ushauri wa WHO unaongeza kwamba unywaji wa pombe, "kuna uwezekano mkubwa ukaongeza hatari za kiafya ikiwa mtu ataambukizwa virusi vya corona".
Kampuni ya utengenezaji pombe ya Hennessy, inayotengeneza pombe aina ya Hennessy cognac, pia imetahadharisha Wakenya dhidi ya unywaji wa pombe kwa kuamini kwamba itakulinda.
3. Barakoa ''Maski'' za Buluu hazina maambukizi
Ujumbe mara mbili katika mtandao wa Facebook, ambao umekuwa ukisihi Waafika kutovaa barakoa za buluu kwa mdai kwamba zimepata virusi umesambaa pakubwa.

Ujumbe wa kwanza unadai kwamba umemnukuu mwasisi wa kampuni ya Amazon, Jeff Bezos na kuwa huo ni mpango wa kusambaza barakoa zenye viini.
"Waafrika, muepuke kuvaa barakoa za rangi ya buluu ambazo zinatengenezwa Marekani na Ulaya kwasababu barakoa hizo zina sumu mbaya yenye kuua" ujumbe huo unasema. lakini hauelezei ni sumu hiyo ni ya aina gani?
Kwa upande wake, Amazon imesema kwamba nukuu hizo watu wamejitungia hivyobasi ni ghushi.
Ujumbe mwengine - ambao sasa unamnukuu mkuu wa Shirika la Afya Duniani kwa madai ya uwongo, pia nao unasihi watu wasivae barakoa za rangi ya buluu.
Mary Stephen, kutoka Ofisi ya WHO, eneo la Afrika, imeiambia BBC kwamba shirika hilo halijapokea ripoti zozote kuwa barakoa hizo zina viini.
"Nchi zinaagiza barakoa zao kutoka kwa vyanzo tofauti tofauti, na hatufahamu kama kuna yoyote ambayo ina viini hivyo," anasema.
4. Barakoa sio hakikisha la kutoambukiza virusi
Gavana wa eneo nchini Nigeria amekosolewa baada ya kudai kwamba kuvaa barakoa ni hakikisho la kujilinda dhidi ya virusi vya corona na kwamba ukishaivaa, huna haja ya kufuatilia hatua ya kutokaribiana.

Ben Ayade, gavana wa jimbo la Cross River, alikuwa anazindua kampeni ya "Hujavaa Barakoa, Hutoweza kutembea" katika mji wa Calabar ili kufahamisha raia kuhusu umuhimu wa kuvaa barakoa.
Madai hayo kuhusu uvaaji wa barakoa ni ya uwongo.
Video inayosambaa kwenye mtandaoni inanamuonesha akisema: "Kwasababu mimi ni Profesa wa Sayansi na ninajua vile virusi hivi vilivyosambaa, najua kwamba ukishavaa barakoa, tayari umejilinda."
Pia anaendelea kusema kwamba huna haja ya kufuata hatua ya kutokaribiana ukishavaa barakoa yenyewe.
Kamishina wa afya wa jimbo, Dr Betta Edu, ameiambia BBC kwamba gavana alikuwa anajaribu kusisitizia umuhimu wa kuvaa barakoa lakini akaweka wazi kwamba unahitaji kuzingatia hatua zingine vilevile.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Kituo cha kudhibiti Magonjwa Nigeria (NCDC) kinasema: "Kuvaa barakoa pekee hakuwezi kukulinda dhidi ya #COVID19."
















