Virusi vya corona: Wanaofadhili WHO , na athari za Trump kulinyima ufadhili shirika hilo

Chanzo cha picha, Getty Images
Wingu la hofu limetanda kuhusu hatma ya shirika la afya duniani WHO kufuatia uamuzi uliochukuliwa na rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump Jumanne aliagiza kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani katika Shirika la Afya Duniani wakati linakabiliana na janga la virusi vya corona lililokumba ulimwengu.
Rais wa Marekani amesema kwamba hatua hiyo itatekelezwa huku ikipitia tena jukumu la Shirika hilo wakati ambapo limeshindwa kusimamia uendeshaji wa shughuli za kukabliana na ugonjwa wa covid-19, pamoja na madai ya kutosema ukweli kuhusu maambukizi hayo.


Chanzo cha picha, Getty Images
"Ikiwa WHO ingekuwa imefanya kazi yake ya kutuma wataalamu wa kitabibu nchini China ili kutathmini hali ilivyo, na kuikosoa China kwa kutokuwa wazi, ugonjwa huo ungeweza kudhibitiwa na kutokea kwa idadi ndogo ya vifo," Trump alisema, ambaye anashutumu shirika hilo kwa kuipendelea China chimbuko la janga la corona.
Lakini Je WHO imekuwa ikifadhiliwa vipi?
Ufadhili wa lazima na wakujitolea
Shirika hilo liliundwa 1948 kama sehemu ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, likilenga kuendeleza afya bora, kuhakikisha dunia inakuwa salama na kuhudumia wale walio katika hatari zaidi."
Taasisi hiyo, ambayo makao yake makuu ni Geneva (Uswizi), ilikuwa na bajeti ya karibia dola bilioni 5.6 kwa kipindi cha miaka miwili 2018-2019, na vyanzo vyake ni viwili tofauti.
Kwanza, kuna pesa ambazo ni lazima zitolewe na nchi washirika 194.
Kila nchi inatakiwa kulipa kiwango fulani kulingana na Umoja wa Mataifa kupitia mfumo ambao ni vigumu kuelezeka kwasababu unazingatia utajiri wa nchi na idadi ya watu.
Ni pesa ambayo kwa msingi huwa inasimamia mishahara na utawala wa shirika hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2018-2019, ufadhili huo ulijumuisha karibia dola milioni 950 za Marekani.
Pili ni ufadhili wa kujitolea unaowezesha nchi na maeneo kuahidi pesa watakazochangia kwa maswala maalum, kama vile chanjo ya ugonjwa wa polio, afya ya wanawake au ukabilianaji na matumizi ya tumbaku.
Mwaka 2018-2019, fedha hizo zilikuwa karibia dola bilioni 4.3.
Tatizo"
Jack Chow, aliyekuwa balozi wa Marekani katika kukabiliana na ukimwi na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa WHO, anasema katika miaka ya hivi ya karibu shirika hilo limekuwa likijitegemea kusaidiwa katika kupata raslimali zake ambazo tayari ni sehemu ya bajeti yake.
"Hili linasababisha matatizo kwasababu ni wafadhili ndio wanaoandaa ajenda zitakazofuatwa na shirika hilo badala ya kufanya maamuzi yao kwa kuzingatia taaluma," Chow amesema katika mahojiano na BBC Mundo.
Kulingana na taarifa za matumaizi ya fedha za hivi karibuni zilizotolewa na WHO, Marekani ndio mchangiaji mkubwa wa shirika hilo baada ya kujitolea kufadhili dola milioni 893 za Marekani 2018-2019 kwa miaka miwili, ambapo hadi dola milioni 553 za Marekani zimeshatolewa kufikia robo ya nne ya 2019.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 14.67 ya raslimali zote zilizopokelewa na shirika hilo.
Tofauti na China ambayo ilikuwa imejitolea kutoa dola milioni 86 za Marekani, ambayo tayari imetoa dola milioni 7.9. Ikiwa ni sawa na asilimia 0.21 ya fedha hizo.
Trump anashutumu WHO kwa kushindwa kuzungumza na serikali ya China kuhusu uchangiaji wao, chimbuko la mlipuko wa sasa wa virusi vya corona.
Baada ya Marekani, ni shirika la kibinafsi la Bill and Melinda Gates Foundation, ambalo liliahidi kutoa karibia dola milioni 530 ambazo tayari imetoa dola milioni 367 million, sawa na asilimia 9.76.
Shirika la Gates lilikosoa amri ya Trump ya kusitisha uchangia wake kwa WHO.
Mchangiaji mkubwa wa tatu ni GAVI, shirika ambalo linajumuisha mashirika ya umma na serikali ambayo yanapigia upato kuongeza upatikanaji wa chanjo kwa nchi 73 katika maeneo ya kaskazini kote duniani.
Ufadhili wao ni hadi dola milioni 316 million, asilimia 8.9 ya fedha hizo zilishapokelewa na WHO.
Uingereza ambayo ni mchangiaji mkubwa wa nne, na nchi ya pili ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa huku ikiwa hadi robo ya nne ya 2019 ilikuwa imeshawasilisha dola milioni 294 million, sawa na asilimia 7.79 ya bajeti hiyo.
Amerika ya Kusini, nchi zenye kuchangia kwa kiasi kikubwa ni Brazil (dola milioni 35.5 za Marekani), Mexico (dola milioni 13.7 za Marekani) na Argentina (dola milioni 8.5 za Marekani).
Athari yake bila ufadhili wa Marekani
Ikiwa Marekani itafanikiwa kutoanza kuchangia, Who itakuwa na changamoto.
"Uamuzi wa Trump kusitisha ufadhili kwa WHO utakuwa na athari kubwa," amesema Dr. Jack Chow katika mahojiano na BBC Mundo.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Lengo kuu la WHO ni kuzuia kusambaratika kwa mifumo ya afya ambayo ni hafifu kote duniani. Washauri wa WHO wanashirikiana na idara za afya, madaktari wa kijamii na wafanyakazi wa afya kuwasaidia kutoa huduma bora kwa wagonjwa," amiongeza.
"Hatua ya Trump huenda ikamaanisha kutamatisha miradi mingi ya msingi, kufutwa kazi kwa washauri wengi wa WHO kutoka nchi mbalimbali duniani, pamoja na kwamba watu wengi wa maeneo kama vile Amerika ya Kusini huenda wakawa hatarini sio tu kwasababu ya covid- 19 lakini hata kwa magonjwa mengine mengi kama kifua kikuu na malaria, " Chow ameonya.
Maneo yanayopata ufadhili mkubwa wa WHO
Kulingana na takwimu za hivi karibuni zilizochapishwa na WHO, raslimali iliyotolewa na Marekani kwa miaka miwili 2018-2019 kiwango kikubwa cha ufadhili wake umeelekezwa mashariki ya eneo la Mediterranean, kwa nchi 22 kutoka Morocco hadi Pakistan.
Eneo hilo limepokea karibia dola milioni 201 za Marekani, sawa na asilimia 36 ya pesa zilizotolewa na Washington.
Eneo la pili lenye kupokea kiwango cha juu cha pesa hizo ni Afrika, ambayo inajumuisha nchi 47 kwa bara hilo huku ufadhili kutoka Marekani ukiwa ni jumla ya dola milioni 151 za Marekani.
Eneo la tatu linalopokea ufadhili wa Marekani ni makao makuu ya WHO, ambayo yanapokea karibia dola milioni 101 za Marekani, kiasi hicho kikitumiwa kwa uendeshaji wa shughuli zake na kampeni kadhaa za masuala ya afya.
Ni asilimia kidogo tu ya ufadhili wa Marekani karibia dola 280,000 sawa na takriban asilimia 0.5, ambazo zimetumika kufadhili shughuli za WHO kwa nchi za Amerika ya Kusini na zile za Caribbean.
Upande wa kampeni za afya, zaidi ya robo ya ufadhili wa Marekani zimetegwa kukabiliana na polio duniani (dola milioni 158 sawa na asilimia 27 ya pesa ilizotoa kwa ujumla).
Pesa nyingine dola milioni 100 zimetumika katika miradi ya kuwezesha watu kupata afya bora na ulaji sahihi, huku dola milioni 44 za Marekani zikitumika katika miradi ya utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Na dola milioni 33 zinazohitajika kukabiliana na kifua kikuu zikiwa zimeanza kupokelewa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini hiyo ni baadhi tu ya miradi kwasababu pia kuna fedha zilizotengwa kukabiliana na Ukimwi na hepatitis hadi uzuiaji na udhibiti wa kutokea kwa majanga pamoja na pesa za kukabiliana na magonjwa ya kitropiki hadi afya ya uzazi, upatikanaji wa dawa na miradi mingine mingi.
Kwa covid-19, mwezi Machi, WHO iliomba pesa za ziada dola milioni
675 kukabiliana na janga hili na kwasasa hivi shirika hilo linatarajiwa kuomba ufadhili wa ziada wa angalau dola bilioni 1 na zaidi.
"Hatua hiyo inafanya mambo kuwa mabaya zaidi"
Chow anakubaliana na maono kwamba shirika hilo linahitaji kufanyiwa mabadiliko na kuimarishwa.
Alisema kwamba WHO na China zimekosolewa kwa kushindwa kusema ukweli kuhusu taarifa na ukubwa wa janga la covid-19 lakini akaonya kwamba huu sio muda mwafaka kuchukua uamuzi kama uliochukuliwa na Trump.
"Wakati mzuri wa kutathmini michango ya nchi katika janga hili na ukosoaji ikiwemo WHO itakuwa ni pale ambapo janga hilo limedhibitiwa na kutokomezwa. Kushambulia na kutikisha shirika la WHO katikati ya janga ni kufanya mambo kuwa mabaya zaidi," Chow amesema.
"Hili ni sawa na kuondoa ufadhili uliokuwa umetengewa idara ya moto wakati ambapo unaungua. "














