Coronavirus: Ugonjwa wa corona unavyoathiri mazishi na maombolezo

Wanasema kwamba kuzaliwa ni bahati ila kifo ni lazima. Ni usemi ambao unapaswa kutufanya kama binadamu kukubali kifo.

Lakini tangu miaka ya awali kila wakati kinapobisha hodi, huwa kinatuacha na dhiki, majonzi, uchungu na maswali mengi mbona marehemu akatuacha… alikuwa bado mdogo… alikuwa bado hajamaliza kujenga nyumba… nani atalinda watoto au famiia yake? Ama kweli pangookapo jino, pengo hubakia.

Pengine ni kutokana na pengo hili ndiyo sababu makabila mengi Afrika mashariki huamua kuandaa karamu wakati mtu anapofariki.

Jamii nyingi hasa za asili ya kibantu na nilotes huandaa sherehe ya kuomboleza inayochukua takribani juma moja. Sherehe hizi huandaliwa kulingana na hadhi ya mtu huyo katika jamii, umri, dini na hata fedha.

Lakini kutokana na janga la corona kumekuwa na mabadiliko.

Siku kadhaa zilizopita, baadhi ya marais kutoka Afrika Mashariki walitangaza kusitishwa kwa mikutano ya hadhara kama njia moja ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Hii ilimaanisha kwamba sherehe kama mazishi, harusi, sherehe za kuzaliwa, mikutano ya kisiasa na nyinginezo zilipaswa kuchukua mkondo tofauti.

Nchini Kenya, kumekuwa na sheria ya muda ya jinsi ambavyo watu watajumuika na kufanya mazishi. Idadi ya watu wanaohudhuria mazishi imepunguzwa hadi 10- 15 pekee.

Sheria hii hata hivyo imekuwa na athari si haba kwa jamii ambazo zina mitindo wa kufanyia wafu sherehe.

Jamii ya waluhya kutoka magharibi mwa Kenya ni miongoni mwa jamii ambazo zimeathirika na sheria hii. Maombolezo katika jamii hii huambatanishwa na mila na matambiko kadhaa ambayo huwa lazima yafanywe kulingana na umri au nafasi aliyokuwa nayo marehemu.

Julius Oronje ni mzee wa miaka 60 kutoka kaunti ya Kakamega nchini Kenya. Anasema kwamba mila na desturi zilizokuwa zikiandamana na sherehe za mazishi hazifanyiki tena.

" Kulingana na mila yetu, mtu akifa anapaswa kumaliza siku tatu. Ambapo jamaa hujumuika na kufanya sherehe za kumkumbuka marehemu... Ng'ombe jike au dume huchinjwa kulingana na jinsia ya marehemu. Ng'ombe huchinjwa na nyama hiyo kuliwa na watu wanaohudhuria. Iwapo nyama haitatosha, ng'ombe za watoto wao pia hutolewa na kuchinjwa."

Katika jamii hii, sherehe za mazishi ni njia ya kumwonesha heshima aliyeaga dunia. Na huhusisha kukesha na ngoma kuchezwa kwa siku tatu. Iwapo jamaa za marehemu wako mbali, basi sherehe hizi huchukua hata zaidi ya juma moja ili kuwapa nafasi ya wao kusafiri.

"Ngoma huchezwa, na watu hucheza densi. Ikiwa mtu huyo ni wa hadhi ya juu, basi fahari wawili huletwa na kupigana ndondi. Yote hii inafanywa kwa heshima ya marehemu. Lakini kutokana na janga hili la corona, tunalazimika kuacha mila zetu"

Wanaokodishwa kwa ajili ya kuomboleza wamepoteza ajira kipindi hiki

Jamii ya Waluo kutoka magharibi mwa Kenya, inatambulika kwa mtindo huu wa kutumia waombolezaji wa kulipwa. Hata hivyo wengi ambao hutegemea sanaa hii kujipatia kipato kwa sasa wamelazimika kutafuta njia nyingine ya kujipatia kipato.

Barrack Okello ni muombolezaji wa kulipwa kutoka kaunti ya Siaya magharibi mwa Kenya. Anaweza kwamba amelazimika kufanya kazi ya bodaboda baada ya kazi yake kuathirika.

"Ninahangaika. Kwa sasa hakuna matanga ambayo yanafanyika. Imebidi nitafute biashara ndogo ndogo ili niweze kulisha familia yangu."

Ni biashara ambayo anasema humpatia kati ya shilingi 5000 na zaidi Kwa siku kulingana na hadhi ya marehemu.

Barrack mwenye umri wa miaka 33 anasema kwamba ni muhimu kuiombea serikali ipate suluhisho ya janga hili.

"Kazi hii nimeifanya Kwa muda wa miaka 5. Imenisaidia kupata karo ya shule ya watoto na pia kuisaidia familia yangu. Kwa sasa ni muhimu kama wananchi kufuata maagizo tuliyopewa na serikali, ili tukabiliane na corona na maisha yarudi kama yalivyokuwa."

Mkuu wa wilaya wa Navakholo iliyoko Magharibi mwa Kenya Geoffrey Tanui anasema kuwa serikali imechukua jukumu la kuwahamasisha watu kuhusu umuhimu wa kufuata maagizo yaliyotolewa na serikali.

" Kufuatia kusitishwa Kwa mikutano, tumebuni njia ya kuwafikia watu na ujumbe kuhusu jinsi ya kujikinga na ugonjwa huu hasa kutojumuika katika matanga. Tunaweka vipaza sauti kwenye gari zetu na kuzunguka tukiwapasha raia. Ilikuwa ni vigumu amri hii kuzingatiwa awali ilivyotolewa lakini sasa wanafuata maagizo na yote ni kwa ajili ya usalama wao."

Vyumba vya kuhifadhi maiti vinavyomilikiwa na serikali pia vimefungwa.

"Tunawashauri watu kuwazika wapendwa wao haraka iwezekanavyo. Mtu akifa asubuhi anazikwa kabla ya jua kutua. Na ni jamaa 10-15 wa karibu wanaoruhusiwa kuhudhuria"

Pamoja na maagizo yaliyotolewa na serikali ya Kenya ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa corona ni amri ya kutotoka nje, ambayo bado inakumbwa na pingamizi huku raia wengi hasa wachuuzi wakilalamika kwamba wanafinyika kimapato.