Zaidi ya klabu 100 ambazo hazipo kwenye ligi zaiandikia FA juu ya kuahirishwa kwa msimu

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya klabu 100 ambazo hazishiriki kwenye ngazi za juu za ligi nchini England zimetuma barua ya wazi kwa Shirikisho la Mprira (la nchi hiyo) FA na kulitaka kufikiria tena uamuzi wake wa kufuta misimu yao.
Baadhi ya wabunge pia wameziambia klabu hizo kuwa wataiandikia Idara ya Digitali, Utamaduni, Mawasiliano na Michezo wakitaka iingilie kati katika kile ambacho wamekieleza kama moja ya uamuzi wenye kukatisha tamaa.
Wiki iliyopita ilitangazwa kwamba mashindano yote chini ya madaraja matatu ya juu ya England yanasitishwa mara moja huku matokeo ya mechi zilizochezwa tayari yakiufutwa.
Hii inamaanisha kwamba hakuna timu itakayopanda wala kushuka daraja katika ligi 91.
Hatua sawia na hiyo itatekelezwa katika ligi ya wanawake.
Hata hivyo umauzi huo bado haujaidhinishwa na Baraza la FA.
Michezo imeathirika vibaya na janga la virusi vya corona huku mechi ambazo zilikuwa zimepangwa zikiahirishwa mapema mwezi huu.


Ijumaa ya wiki hii klabu zinazoshiriki Ligi ya Primia zinatarajiwa kukutana na kujadili mustakabali wa ligi hiyo iliyosimamishwa mpaka Aprili 30.
Barua hiyo inasema: "Wasiwasi wetu ni kuhusu uamuzi uliochukuliwa kwa haraka bila ya majadiliano ya kina ama kushauriana na klabu zilizoathirika.
"Uamauzi huo pia hauzingatii mamilioni ya pauni ya wawekezaji na muda uliotumika ambavyo vyote vimekuwa na athari mbaya ya kifedha.
"Kuandika barua hii ya pamoja, tunatambua kwamba uamuzi wa kufuta matokeo ya msimu wa 2019-20 bado kunategemea kuidhinishwa na Baraza la FA.
"Hatahivyo, tunaamini kwamba kupitishwa kwa uamuzi kama huu ni jambo lisilokubalika. Tunaomba kufanya mazungumzo haraka iwezekanavyo na FA lengo likiwa ni kutaka uamuzi huo upitiwe tena."
BBC imekuwa ikifuatilia mawasiliano kati ya vilabu na wabunge wao wa eneo wameashiria kwamba wameandika au wataiandikia Idara ya Digitali, Utamaduni, Mawasiliano na Michezo kuhusu suala hili.
Barua hiyo inasema kwamba ikiwa hakuna makubaliano yatakayofikiwa na vilabu hivyo, watachukua mkondo wa kisheria".
Katika taarifa, Shirika la FA limesema: Uamuzi uliochukuliwa kutamatisha msimu wa mwaka 2019- 20, Ligi ya taifa, ligi ya wanawake na mashindano mengine ya eneo ulifanyika kupitia wawakilishi wa kamati za ligi husika na kuungwa mkono na bodi ya FA na bodi ya Wanawake ya FA.
"Kwa sasa barua hiyo itaenda katika Baraza la FA ili kuidhinishwa. Tunaunga mkono uamuzi unaotolewa wakati wa changamoto hizi na hatua ambazo hazijawahi kuchukuliwa kabla katika soka ya Uingereza."












