India: Baba azika ua kuchoma maelfu ya miili ya watu kujifariji kwa kifo cha mtoto wake

"Siku moja niliona maafisa wa polisi wakitupa mwili wa mtu kwenye mto. Niliogopa" anasema Mohammad Shareef.

"Kuanzia siku hiyo nilijiambia kwamba mimi nitakuwa mzazi wa miili ya watu wasiojulikana inayotupwa na serikali na kuwaandalia mazishi ya stahiki."

Kwa kipindi cha miaka 28 iliyopita, Shareef amekuwa akitimiza ahadi hiyo kama kumbukumbu ya kijana wake, ambaye aliuawa katika vita vya Wahindi za Waislamu na ambaye mwili wake haujawahi kuonekana.

Ikolojia ambaye anajulikana kama Chacha (Mjomba) Shareef, kaskazini mwa India mji wa Ayodhya, amezungumza na BBC kuhusu anachofanya. .

Kuzika na kuchoma miili

Hawezi kuhesabu idadi ya mazishi ambayo ameandaa mpaka hii leo. Mkuu wa eneo la Ayodhya, Anuj Kumar Jha, ameiambia BBC kwamba hawana rekodi kamili ya miili ambayo imekabidhiwa Shareef.

"Kwa kukadiria huenda tumempa miili karibia 2,5000," amesema. Hata hivyo, familia ya Shareef imesema kwamba amekuwa akiandaa mazishi stahiki kwa watu asiowajua zaidi ya 5,500 lakini vyombo vya habari vya India vinasema kwamba idadi hiyo ni zaidi ya 25,000.

Miili ya watu waliokufa ambao hawajatambuliwa na jamaa zao huwa ni mingi sana pengine hilo huchangiwa na ajali za barabaarani na za kwenye reli au watu wanaokufa wakiwa mbali na nyumbani kwao - pengine wameenda kuhiji, wahamiaji ama watu wazee waliotelekezwa na watoto wao.

Baadhi ya wagonjwa pia hufa hospitalini na kutokea kwamba hawana mtu au jamaa ya kuwaandalia mazishi kwa njia stahiki.

Maafisa huandaa mazishi kwa miili ambayo haijatambuliwa na jamaa zao kupitia shirika lisilo la kiserikali na watu wanaojitolea kama Shareef lakini kawaida huwa ni huduma isiyokuwa na malipo yoyote.

Kazi yake ya kupigiwa mfano inaanza kutambulika baada ya jina lake kuwa miongoni mwa wale waliotambuliwa na serikali - na atapokea tuzo maarufu ya taifa.

Kwa mjomba Shareef, tuzo hiyo ni kilele cha safari ambayo haijakuwa rahisi.

Namkumbuka mtoto wangu

Mama yake aliga dunia punde tu baada ya kuzaliwa na hivyo basi akalelewa na bibi na babu yake ambao hawakuwa na uwezo wa kumpeleka shuleni.

Alianza kufanyakazi akiwa na umri mdogo na kujifunza kutengeneza baiskeli lakini akawa mfanyakazi wa huduma za jamii akiingia miaka ya 50 baada ya kupata msiba.

"Baada ya kijana wagu kufa nilimtafuta kila mahali kiasi cha kama mwezi hivi, kama mwendawazimu."

Vita vya Wahindi na Waislamu

Kijana wa Shareef, Mohammad Rais, 25, aliuawa katika vita vya Wahindi na Waislamu 1992, ambavyo vilitikisa mji wa Ayodhya na nchi nzima kwa ujumla.

"Polisi waliniambia kwamba ameoza. Na hatukuona mwili wake bali nguo zake tu."

Wahindi wenye msimamo mkali wakiongozwa na waanzilishi wa chama tawala cha Bharatiya Janata walivamia msikiti uliokuwa umedumu kwa karne 16 katika mji wa Ayodhya Desemba 1992.

Hilo lilisababisha vita kati ya Wahindi na Waislamu kaskazini mwa India na kusababisha vifo vya mamia ya watu wasiokuwa na hatia.

Ni nani aliyemuua kijana wangu?

Hata hii leo, Shareef hana uhakika wa wapi au pale mtoto wake wa kiume alipouawa au nani aliyemuua.

"Nafikiri mwili wa mtoto wangu ulitupwa kwenye mto kama miili mengine inayotafutwa," amesema Shareef mwenye umri wa maika 80.

Wakati huo, maeneo mengi ya India hayakuwa na vyumba vya kuhifadhia maiti. Ilikuwa ni jambo la kawaida kutupa miili ya watu ambayo haijatambuliwa haraka iwezekanavyo.

Kuzika ndio njia iliyokuwa inatumiwa na wengi lakini katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa India walitupa miili ya watu ambayo haijatambuliwa kwenye mito ili kupunguza gharama, wakati na nguvu kazi pia.

"Niliendelea kumtafuta kijana wangu kwa mwezi mzima na sikuwahi kumuona popote. Kuna wakati niliamua kwenda katika mji jirani kumtafuta.

Familia ya Shareef ilishuku kwamba mwili wa Rais umetupwa katika mto Gomti umbali wa takriban kilomita 50.

Kifo cha Rais kilifadhaisha wazazi wake, na kusababisha mama yake kupata msongo wa mawazo tatizo ambalo bado analo hadi hii leo.

Uchungu wa kumpoteza mtoto unaongezeka kwasababu hawakuweza kumpa kijana wao mazishi stahiki.

Nilichotaka kufikia

Wakati wa mabadiliko makubwa ya kihisia ulipowadia, ulijidhihirisha kuwa mwanzo mpya. Shareef alitoka katika kuomboleza na kuanza kuandaa mazishi ya heshima kama inavyotakikana kwa miili ambayo haijulikani wenyewe.

"Niliamua kwamba katika eneo ninalokaa, hakuna mwili wa mtu asiyejulikana utatupwa tena kwenye mto," anasema.

Aliwaarifu polisi mpango wake wa kutaka kuchukua jukumu ambalo kila mmoja analiepuka.

"Nilipopata simu ya kwanza, moyo wangu ulikuwa unadunda. Baada ya kufanywa kwa uchunguzi, polisi wakaniambia nichukue mwili huo. Nakumbuka vizuri kabisa shingo ilikuwa imekatwa"

Muda mfupi tu baada ya hapo, kazi yake ikaanza kuongezeka kiasi kwamba alinunua mkokoteni wenye magurudumu manne kama usafiri wa kubeba miili hiyo.

'Nilionekana kama Mwendawazimu'

Familia yake, marafiki hata majirani walishangazwa na majukumu yake mapya.

"Hakuna yeyote katika familia yangu ambaye alikuwa anafurahishwa na kile ninachofanya. Walisema kwamba nimekuwa kichaa."

Katika dini ya Kihindi, watu wa tabaka la chini kulingana na historia ndio wanaolazimika kufanya kazi ya kuzika na kuchoma wale waliokufa.

Kwasababu ya kazi yake, Shareef ingawa ni Muislamu, alitengwa na jamii.

"Watu wengine walikuwa wananiogopa. Walikuwa wanaona kwamba watapata bakteria iwapo watagusana na mimi."

Lakini Shareef alikuwa ameamua kutimiza ndoto yake. Alikuwa ahudhurii harusi za familia, matamasha na hata ibada kunusuru wale wasiomjua. Hilo lilimpa amani na kumfariji.

"Ilinisaidia kukabiliana na uchungu wa kifo cha kijana wangu."

Wakati anafanya sala za mwisho mara nyingi huwa anamkumbuka kijana wake.

"Huwa namkumbuka kila wakati. Namtamani."

Mimi huosha maiti na kuwafanyia sala ya mwisho

Kawaida huwa anaosha miili ya waliokufa ama kabla ya kuuzika au kuuchoma. Iwapo atajua kuwa ni Muislamu, anaufunika mwili vizuri kwa kuuzungushia kipande cha nguo na kumuombea sala ya mwisho kama inavyotatikana kulingana na dini hiyo.

Iwapo mwili ni wa muumini wa Kihindi, anaupeleka kwenda kuchomwa umbali wa kilomita nne kutoka ilipo nyumba yake.

"Kila ninapopigiwa simu na polisi kuchukua mwili, naacha kila kitu na kukimbilia huko."

Mwili hutelekezwa baada ya kifo

Kawaida huwa anapata mwili siku au hata wiki kadhaa baada ya kifo kutokea.

Maafisa wa polisi wanajitahidi kadiri ya uwezo wao kutambua mwili lakini iwapo hakuna atakayejitokeza kama jamaa ya aliyekufa, mwili huo unatupwa.

"Wakati mwingine maafisa wa polisi huandamana na mimi hadi makaburini lakini pia nao tunapofiika eneo la tukio, husimama mbali kdogo."

Shareef anasema hajawahi kuchukizwa na maiti, lakini kama mwanadamu mwengine yeyote, huwa anapata mfadhaiko baada ya kuona mabaki ya mwanadamau aliyeoza na pia kuvuta ile harufu mbaya inayotoka kwasababu mwili umeoza.

"Ninapoona miili ambayo imechinjwa ama imeoza nahangaika kupata usingizi. Naota ndoto mbaya na hata kuamua kunywa dawa za kupata usingizi."

"Watu wananisifu kwa kile ninachofanya - wansema kwamba ninawapa mazishi ya heshima kama watu wa familia yangu."

Lakini maneno hayo haimaanishi kwamba wananipa pesa.

Nimekuwa mpambanaji kwa muda mrefu

Shareef alikuwa anahangaika peke yake kwa karibia miaka kumi. Si serikali wala mashirika yasiyo ya kifaida, hakuna anayempa usaidizi wa kifedha.

Maduka ya mtaani humpa pesa kuanzia $150 hadi $170 ili kukidhi gharama za mazishi.

Kwa sasa ana wasimamizi wawili ambao wanashirikishana gharama hizo.

"Wahindi na Waislamu wote wananisaidia. Watu wananipa chakula na mablanketi. Hivi karibu nilifanyiwa upasuaji wa jicho - mti nisiye mjua alinipigia simu na kunipa rupee 20,000 ($290)."

Sina Mrithi

Anaendelea kuzeeka lakini hana mtu ambaye anaweza kumrithisha kijiti hicho. Si vijana wake wawili wala wajukuu zake hakuna ambaye yuko tayari kumrithi kwa kazi hiyo.

"Wanasema, kama babu anafanya kazi hiyo, acha yeye afanye. Hakuna anaetaka kujihusisha na kazi ninayofanya."

Bado anaendelea kusimamia duka lake la kukarabati baiskeli ambalo linampa karibia $3 kwa siku.

Tuzo ya serikali haitamsaidia kifedha, lakini anafuraha kwamba hatimaye juhudi zake zimetambulika.

Siwezi kuacha kazi yangu

Pia, hawezi kuacha kufanya kazi hiyo kwasababu anafahamu fika kile kitakachotokea iwapo atadhubutu kuacha kufanya kazi yake.

"Iwapo nitakosekana, polisi watatupa miili ya watu kwenye mito kama walivyokuwa wanafanya awali."

Mimi ndo mkombozi wa waliokufa.

"Nitaendelea kufanya kazi hii hadi siku yangu ya mwisho duniani," anasema.