Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Coronavirus: Mahakama kuu ya Kenya imeaamrisha kusitishwa kwa ndege zote kutoka China
Mahakama kuu ya Kenya imesitisha kwa muda ndege zote kutoka China kuingia nchini humo kufuatia kesi kuhusu coronavirus iliyowasilishwa na chama cha mawakili wa Kenya.
Akitoa hukumu yake Ijumaa jaji James Makau amemuamrisha waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i na waziri wa zamani wa afya Sicily Kariuki kuwatafuta abiria wote 239 waliowasili nchini kutoka China kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata mnamo Februari 26, na kuwatenga katika hospitali ya kijeshi.
Huku hayo yakijiri Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa agizo la rais kuhusu coronavirus kufuatia malalamiko ya umma kutoka kwa Wakenya kuhusiana na jinsi serikali inavyoshughulikia virusi hatari vya corona ambavyo vinaendelea kutikisa mataifa duniani.
Katika agizo lake Bw. Kenyatta anataka kamati ya kitaifa ya hali ya dharura kushughulikia mlipuko wa coronavirus.
Rais pia ameamrisha kukamilishwa kwa kituo cha kitaifa cha kuwatenga na kuwatibu wagonjwa mjini Nairobi katika kipindi cha siku saba.
"Kenya ni lango kuu la usafiri wa kimataifa, ikiwa na asilimia 70 ya wasafiri wa kimataifa wanaopitia nchi hii kuelekea mataifa mengine, hivyo basi ipo haja ya kuimarisha hali ya tahadhari ili kudhibiti hatari ya kusambaa kwa coronavirus nchini Kenya kutoka mataifa mengine ambayo yanakabiliwa na mlipuko unaoendelea wa maradhi yanayoathiri mfumo wa kupumua" kulingana na agizo hilo la rais nambari mbili la mwaka 2020.
Katika kile kinachoonekana kujibu malalamiko ya umma kuhusiana na jinsi serikali yake inavyoshughulikia suala hilo, Bw. Kenyatta amekiri kuwa "kuna haja ya kupatia kipaumbele suala hilo kwa maslahi ya umma kwa kuimarisha viwango vya tahadhari Kenya na kuongeza juhudi za kukabiliana na kudhibiti mlipuko wa virusi vya corona ambavyo vimekuwa janga la afya la kimataifa ."
Siku ya Ijumaa magazeti ya Kenya yameangazia kwa kina ghadhabu ya Wakenya baada ya serikali kuruhusu ndege kutoka China kutua nchini.
Hatua hiyo pia imelalamikiwa sana katika mitandao ya kijamii baada ya kuwasili nchini Kenya siku ya Jumanne, ambapo ndege ya shirika la Southern kuruhusiwa nchini ikiwa na abiria 239.
Saa kadhaa kabla ya hatua hiyo, maafisa wa Kenya walikuwa wametangaza kurejelewa kwa safari za ndege kuenda China, licha ya hofu ya kusambaa kwa virusi vya Covid-19.