Je ilikuwaje pombe ikatoka kutoka mifereji ya jikoni katika jimbo la Kerala India?

Pombe ya rangi ya kahawia ikitoka katika mifereji

Chanzo cha picha, Joshy Maliyekkal

Maelezo ya picha, Pombe ilianza kutoka katika mifereji ya nyumba hizo

Wakaazi wa mtaa mmoja wa nyumba za ghorofa kusini mwa India walipigwa na butwaa baada ya mchanganyiko wa pombe kuanza kutoka katika mifereji yao.

Mchanganyiko huo wa rangi ya kahawia ulianza kutoka kwenye mifereji ya jikoni katika nyumba hizo jimbo la Kerala siku ya Jumatatu asubuhi.

Wakaazi ambao hawakufurahishwa na kisa hicho waliwasiliana na mamlaka ili kupata usaidizi na kugundua kwamba kisima cha maji yao kilikuwa kimechafuliwa na maafisa - kwa bahati mbaya.

Ilibainika kwamba lita 6,000 za pombe zilikuwa zimezikwa karibu na eneo hilo.

Pombe hiyo ambayo maafisa walikuwa wameiweka katika shimo baada ya kuchukuliwa kutokana na agizo la mahakama ilipenya mchangani kabla ya kuingia katika kisima hicho - ambacho ndio chanzo cha maji yanayosambazwa katika ghorofa 18 za wilaya ya Thessur.

''Tulishangaa'' , mmiliki wa ghrofa hizo alimuambia mwandishi wa BBC Hindi Imran Qureshi.

Kwa bahati nzuri harufu kali iliokuwa ikitoka katika miferereji hiyo haikuwavutia wakaazi hao .

Hatahivyo ugunduzi huo ulimaanisha kwamba hakuna maji ya kunywa kwa familia mbali na pia hawakuweza kuosha chochote.

''Watoto hawakuweza kwenda shule na hata wazazi wao hawakuweza kwenda kazini'' , alisema bwana Malyiekkal.

Maji machafu kutoka katika kisima hicho yakitolewa

Chanzo cha picha, Joshy Maliyekkal

Maelezo ya picha, Maji machafu kutoka katika kisima hicho yakitolewa

Baada ya wakaazi kulalamika , maafisa waliingilia kati ili kurekebisha makosa. Hatahivyo huenda ikachukua muda wa mwezi mmoja kusafisha kisima hicho ,kulingana na wakaazi hatua itakayowafanya kutegemea maji kutoka kwa mamlaka.

''Wamekuwa wakisambaza takriban lita 5000 za maji kila siku lakini hazitoshi kuhudumia familia zote katika nyumba hizo'', alisema Malyiekkal akiongezea kwamba kisima hicho ndicho kilichokuwa chanzo cha pekee cha maji,

Maafisa kutoka kwa idara hawakujibu maswali kutoka kwa BBC.

Jimbo la Kerala lina sifa ya unywaji mkubwa wa pombe nchini humo

Presentational grey line