Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Andy Ruiz alaumu uzito kupita kiasi baada ya kushindwa na Anthony Joshua
Andy Ruiz Jr amesema kwamba miezi mitatu ya kusherehekea na ukosefu wa mazoezi ya kutosha kumemfanya kuwa na "uzito kupita kiasi" wakati wa shindano la kutetea taji lake dhidi ya Anthony Joshua.
Ruiz mwenye umri wa miaka 30, alishindwa kwa alama katika pigano hilo lililofanyika Saudi Arabia, ikiwa ni miezi sita baada ya kuutikisa ulimwengu pale alipomshinda bingwa wa ndondi katika uzani mzito Anthony Joshua kule Marekani.
Mwanandondi huyo wa Mexico amesema kwamba ingekuwa vizuri iwapo atapata pigano la tatu.
"Nilitakiwa kufanya mazoezi ya kutosha. Ningewasikiliza zaidi makocha na timu yangu," Ruiz amesema.
"Kwa pigano hili nilikuwa na uzito kupita kiasi. Sikufanikiwa kufanya mijongeo yangu kama nilivyotaka iwe."
"Hakuna sababu ya kujitetea ukweli ni kwamba nilisherekea zaidi. Lakini katika pigano jengine mambo yatakuwa tofauti."
Ruiz, anayeshikilia nafasi ya pili katika ubingwa wa dunia kwenye ndodi, aliongeza kilo 7 tangu alipomshinda Joshua, ambaye kwa sasa amekuwa mshindi mara mbili.
Wengi walikuwa wamehoji iwapo mtindo wake wa maisha ambao ni pamoja na kununua majumba mapya, magari na kufanya mikutano kadhaa na vyombo vya habari baada ya kushinda huenda iwaka sababu ya kujiachia.
Ruiz ameonekana mwenye kujutia na kuomba msamaha kwa makocha wake Manny Robles na babake Andres alipofanya mkutano na wanahabari baada ya pigano na mashabiki wake wakaashiria kumridhia kwa kumpigia makofi.
Mwandondi huyo aliyekuwa bingwa wa dunia anadai kwamba baada ya kupata ushindi alipunguza uzito lakini baadaye ukaanza kuongeza: "Niliongeza uzito na hilo lilikuwa kosa kubwa. Hakuna anayejua kuhusu mazoezi tuliyokuwa tunafanya. Tulijitihadi kadiri ya uwezo wetu.
"Kuwa bingwa kwa mara ya kwanza, kuwa hapa na pale na kukosa mazoezi, halikuwa jambo rahisi.
"Naahidi ya kwamba mambo yatakuwa mazuri na kwa sasa ninachotaka nikurejea nilivyokuwa hapa Saudi Arabia."
Kocha wake Robles aliongeza kwamba alikuwa na miezi mitatu ya kufanya mazoezi lakini ni mengi ambayo hayangeweza kufanywa katika kipindi cha miezi mitatu tangu alipomshinda Joshua na pale alipoanza kufanya mazoezi.
"Sitaki kusema kwamba miezi mitatu ya kusherehekea haikuniathiri", amesema Ruiz.
"Hakuna sababu ya kujitetea ukweli ni kwamba nilisherekea zaidi. Lakini katika pigano jengine mambo yatakuwa tofauti."
"Bado watu wanamashaka na mimi. Bado mimi ni mpiganaji mzuri katika uzani mzito na ukweli ni kwamba nina uwezo kumshinda yeyote duniani."
"Naomba muamini kwamba nitarejea katika nafasi yangu na kuwa tena bingwa wa ndodi dunia kwa kitengo cha uzani mzito dunia."
Anthony Joshua: Niko tayari kuzikunja na Oleksandr Usyk
Anthony Joshua amesema hakuamini macho yake alipomshinda Andy Ruiz Jr na kuwa bingwa wa ndondi wa dunia katika uzito wa juu kwa mara ya pili na kwamba yuko tayari kuzikunja na Oleksandr Usyk ndani ya kipindi cha miezi sita.
Raia huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 30, amemshinda Ruiz kwa alama huko Saudi Arabia na kulipiza kisasi ukizingatia kwamba Ruiz alimshinda bila kutarajia mwezi Juni mwaka huu.
"Sikutaka nifike kiwango cha kushindwa kujizuia lakini kilikuwa kipindi kilichobeba hisia zangu, " Joshua ameiambia BBC.
"Mimi ni mwanadamu na nimefanya makosa na wakati ambao nilikuwa nimepotea njia, nilikomaa kiakili na kurejea katika njia iliyo sawa ."
Wakati Joshua alipopigana na Ruiz huko New York, alipigiwa upatu kumrithi bingwa wa zamani katika uzani huo Mohamed Ali na kufananishwa na mabingwa wengine kama Lennox Lewis, Floyd Patterson na Wladimir Klitschko ambao waliwahi kuchukua ubingwa wa taji hilo.
Baada ya pigano hilo, WBO imesema lazima apimane nguvu na mwandondi wa Ukraine Usyk ndani ya siku 180.
"Kile ninachoweza kufanya nitafanya,"Joshua amesema hayo katika BBC Radio 5. "Ikiwa hilo ni sawa na kupigana na mwandondi mwengine wa juu katika kitengo hichi, niko tayari."
Baada ya Ruiz nani atakaye zichapa na Joshua?
Kubrat Pulev mwanandodi wa uzani wa juu kutoka Bulgaria pia naye yuko njiani kuzichapa na Joshua lakini makubaliano yanahitajika kufikiwa ya ikiwa kwanza azipime ulingoni na Pulev au Usyk.
Usyk - ambaye alipanda ngazi hadi daraja la uzito wa juu baada ya kushinda mataji yote ya daraja la chini tu ya uzani wa juu - alikuwa miongoni mwa watazamaji wa pigano la Joshua katika ulingo wa Diriyah.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa WBO wa kushindana na wengine baada tu ya kuibuka na ushindi, Joshua amesema: "Ndani ya siku 180? haina tatizo, tupambane kwenye ulingo."
Hata hivyo, mwandalizi wake Eddie Hearn ameondoa uwezekano wa kwamba Joshua atalazimika kuachia mataji wa IBF na WBO iwapo atakataa kupigana na mpinzani wake atakayechaguliwa.
"Sitaendelea kuwaita,"Joshua amesema. "Mimi ninatengeneza jina langu na iwapo wanataka kuwa sehemu ya hili, watainiita. Ruiz alifanya hivyo na kuunda jina lake pia."
"Iwapo hao nao wanataka pigano, na wao pia wanaweza kuliitisha. Angalieni kile ambacho nimewahi kufanya. Ninapoitisha pigano na mengineo, na kosa kuwa mwangalifu."