Je ripoti ya BBI itasaidia kutatua matatizo ya Wakenya?

    • Author, Wanyama wa Chebusiri
    • Nafasi, BBC Africa, Nairobi

Jopokazi La Maridhiano nchini Kenya maarufu kama BBI (Building Bridges Initiative) au handshake,lilianzishwa tarehe 9, mwezi Machi mwaka2018 baada ya rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake mkuu wa kisiasa, Raila Odinga , walipoamua kuzika tofauti zao za kisiasa na kusalimiana hadharani.

Lengo kuu likiwa kuunganisha taifa ambalo nusura litumbukie kwenye vita kufuatia uhasama uliozuka baada ya kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2017.

Uhuru Kenyatta na Raila Odinga baadae waliunda kamati ya watu kumi na nne ambao waliandaa mikutano ya Umma kwenye majimbo 47 kote nchini Kenya, ili kupokea maoni kuhusu mabadiliko wayatakayo wakenya hususani wakizingatia vigezo vifwatavyo;

  • Jinsi ya kumaliza migawanyiko ya kikabila
  • Kuwashirikisha watu wote kuhusu masuala ya utawala na kisiasa.
  • Jinsi ya kushughulikia suala la kumaliza uhasama wa kisiasa unaotokea wakati wa uchaguzi mkuu
  • Jinsi ya kuimarisha amani na usalama
  • Kukabiliana na janga la ufisadi
  • Jinsi ya kukabiliana na ukosefu wa maadili ya kitaifa
  • Maswala ya majukumu na haki za raia
  • Maswala ya kuwajibika kwa pamoja
  • Jinsi ya kuendeleza serikali za ugatuzi.

Kamati hiyo ilikusanya maoni kutoka kwa wakenya wapatao elfu saba na imendaa ripoti ambayo inatarajiwa kuwasilishwa kwa rais Kenyatta na Raila Odinga leo jumanne.

Ripoti hiyo baadae itatolewa hadhari na kuwasilishwa kwa umma ili ipigwe msasa.

Ikiwa Wakenya watakubaliana na yaliyomo kwenye ripoti hiyo, huenda kura ya maoni ikaitishwa na kuerekebisha katika ya mwaka wa 2010 ambayo itasababisha mabadiliko katika muundo wa serikali.

Mambo muhimu yaliyojitokeza katika Jopo hilo maarufuku kama 'Handisheki'

  • Mpasuko mkubwa wa kisiasa umejitokeza nchini Kenya kuhusu maridiano kati ya rais Uhuru na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
  • Maridhiano hayo yameleta mgawanyiko ndani ya chama tawala cha Jubilee na muungnao wa upinzani unoongozwa na Raila Odinga wa NASA.
  • Naibu rais William Ruto anaongoza mrembo wa kisiasa ujulikanao kama Tangatanga" unaoonekana kupinga handisheki kati ya Uhuru na Raila.
  • Uhuru na Raila nao katika juhudi zao za kupigia debe maridiano yao ya kisiasa wana wafuasi wao wanaoegemea mrengo wa kisiasa wa Kieleweke.
  • Miongoni mwa vigogo wa muungano wa NASA wanaopinga handisheki ni Musalia Mudavaidi, ambaye ni kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC).