Pweza na supu yake ina manufaa gani ya kiafya?

- Author, Na Paula Odek
- Nafasi, BBC News Swahili
Pweza na supu yake ni chakula cha kitamaduni tangu kale kinachopendwa na wakazi wa maeneo ya mwambao wa bahari ya Hindi , baadhi wakidai samaki huyo ni zaidi ya kitoweo, lakini je wataalamu wa lishe wanasemaje kuhusu kitoweo hiki?, Paula Odek alisafiri hadi visiwani Zanzibar kubaini mengi zaidi juu ya Pweza.
Katika utamaduni hasa wa wapwani supu ya samaki huyu hupendwa sana na kumekuwa na imani kuwa supu yake si supu tu ya kawaida kama ulizowahi kunywa. Pweza ni kiumbe wa baharini kama vile samaki wengine,ngisi,taa na papa ,lakini ni kiumbe nadra sana anayependwa zaidi kama kitoweo miongoni mwa wakazi wa maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi. Lakini leo nazungumzia utamaduni wa kitoweo hiki visiwani Zanzibar.

Suleiman Hamud ambaye anapenda sana kinywaji supu ya pweza aliniambia kuwa uraha yake inatokana na kinywaji hicho ambacho anadai humsaidia kuongeza damu mwilini, lakini wengi miongoni mwa wakazi wa pwani waliniambia kuwa supu hiyo huongeza nguvu za kiume mwilini.
Mwanamume mwengine ambaye hakutaka kutatwa jina lake litajwe aliniambia yeye hutumia supu hiyo majira ya jioni kwani ni wakati bora wa kuwa na mke wake kwani supu hiyo humpa msisimko wa aina yake.

Supu hiyo maalum hupatikana baada ya pweza kuchemshwa kwa muda na kuongezwa viungo na ladha ya limau. Suleiman Hamud ambaye ni shabiki wa kinywaji hicho amesema furaha yake inatokana na kinywaji hicho ambacho anadai humsaidia kuongeza damu lakini wengi miongoni mwa wakazi wa pwani waliniambia kuwa supu hiyo huongeza nguvu za kiume mwilini.

Supu hiyo maalum hupatikana baada ya pweza kuchemshwa kwa muda na kuongezwa viungo na limao.
''Kwangu binafsi pweza ni samaki ambaye hupendwa na kila mtu hapa Zanzibar, mimi mwenyewe nikiwa mmoja wao,'' alisisitiza Hamadi Katibu.

Abdalla Seif ni mpishi maarufu wa pweza hapa visiwani zanzibar amesema watu wengi kisiwani hapa hupenda kitoweo hiki ambacho anasema kimekidhi mahitaji yake na familia yake.
Seif amesema wateja wake ni wanaume kwa wanawake wengi wakitaka kitoweo hicho pamoja na kujipatia glasi moja ya supu yake ambayo anasema wengi wanaamini ni zaidi ya kinywaji kwa madai kuwa inaongeza nguvu za kiume.

Wataalamu wa lishe wanasema nini kuhusu Pweza?
Kulingana na afisa wa masuala ya lishe katika Wizara ya Afya kisiwani Zanzibar Subira Ali, pweza ni muhimu kwa afya na lishe ya mwanadamu kutokana na virutubisho alivyo navyo.
''Pweza ana madini joto (Iodine) yanayosaidia katika maswala ya uzazi kwa mwanamke na wanaume,''alieleza Bi Subra Ali.
Pweza ana protini ambayo inasaidia kujenga mwili na kuweka kinga mwilini na kujikinga na aina mbali mbali za saratani na huongeza damu mwilini kutokana na chembechembe nyekundu za damu anayoitoa.
Hata hivyo Bi Subra Ali aliniambia kwamba vijana wengi huita supu hiyo mkuyati kwamba hunasaidia kuongeza nguvu za kiume lakini amesema ni kutokana na virutubisho alivyonavyo pweza huyo.
Pweza hana madhara yoyote ya kiafya kwa binadamu na badala ya yake kina mama ambao hawana maziwa ya kutosha ya kuwanyonyesha watoto wanashauriwa na Bi Subra kunywa supu ya pweza. Aliongeza kwamba inaweza kuongeza kiwango cha maziwa ya mama kwa wingi kutokana na virutubisho vya protini na madini ya chuma.
Kumpata pweza si rahisi na anahitaji maandalizi.
Mvuvi Bw. Almasi ambaye amefanya kazi hii ya uvuvi wa pweza kwa miaka 12 aliniambia kuwa kazi ya kumtafuta pweza ni ngumu sana kwani mtu huhitaji kuwa na ujuzi maalum, afya bora na vifaa vilivyo vinavyostahili.

''Pweza ni kiumbe wa ajabu ambaye unaweza kumpita na usimuone na baadaye ukimchunguza zaidi unamuona palepale kwani hujibadilisha kwa rangi tofauti kulingana na sehemu aliyomo kwa wakati ule,'' Bw. Almasi alinieleza.
Pweza huandaliwa vipi?

Utamu wa kitoweo cha pweza unategemea matayarisho yanayofanywa baada ya kumvua. Pweza lazima aandaliwe kwa ustadi na unapokosea hatua moja basi utaupoteza utamu wake na huwa mgumu baada ya kupikwa.
Katika hatua yake ya kwanza ya kumtayarisha Pweza hupondwa ili alainike.

Maajabu ya Pweza
- Pweza hujibadilisha rangi kulingana na sehemu waliopo.
- Pweza ana damu ya rangi ya bluu ambayo inamadini ya kopa kwa jina hymocianin ambayo huwasaidia kuishi chini ya bahari.
- Mikono minane ya pweza huweza kufanya kazi tofauti kwa wakati mmoja.
- Akili yake ipo mikononi mwake huku mishipa yaani neuros ipo kichwani.














