Uchaguzi Israel: Je enzi ya utawala wa Benjamin Netanyahu inaelekea ukingoni?

Chanzo cha picha, Reuters
Matokeo ya awali baada ya uchaguzi mkuu wa pili Israel unaofanyika katika muda wa miezi mitano yanaonyesha kuwa matokeo ya kura yanakaribiana mno kuweza kupata mshindi wa wazi.
Muungano wa chama cha mrengo wa kati Blue and White alliance cha aliyekuwa mkuu wa jeshi Benny Gantz kinatabiriwa kushinda kati ya viti 32 na 34 bungeni na chama cha Likud cha mrengo wa kulia chake waziri mkuu Benjamin Netanyahu kikitabiriwa kujishindia kati ya viti 30 hadi 33.
Huenda kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu, Avigdor Lieberman akabaini mshindi wa siku.
Netanyahu aliitisha uchaguzi huo wa dharura baada ya kushindwa kuunda serikali ya muungano kufuatia uchaguzi mnamo Aprili.
Majadiliano ya kuunda serikali mpya ya muungano yanatarajiwa kuanza punde baada ya matokeo ya awali yatakapotangazwa leo Jumatano.
Akizungumza na wafuasi mapema leo, Netanyahu amesema: "Sote tumepitia kampeni ngumu ya uchaguzi.
"Bado tunasubiri matokeo yenyewe, lakini jambo moja li wazi. Hali nchini Israel ipo katika kiwango cha historia, tumekabiliwa na changamoto nyingi na fursa nyingi."
Kwa upande wake bwana Gantz alionekana kuwa na matumaini zaidi alipozungumza na wafuasi wake mapema kidogo.
"Bila shaka tutayasubiri matokeo halisi, lakini inavyoonekana ni kana kwamba tumelifikia lengo letu," amesema.
"Umoja na utangamano upo mbele yetu."
Matokeo yanaonyesha nini?
Matokeo ya baada ya kufungwa vituo vya kura yaliotolewa na shirika la utangazaji Israel Kan mapema Jumatano yanaonyesha kuwa chama cha Blue and White huenda kingejinyakulia viti 32 na chama cha Likud kikajipatia viti 31 kati ya jumla ya viti 120 bungeni.
Katika nafasi ya tatu ni chama cha Israeli Arab Joint List kilichojinyakulia viti 13; kikifuatwa kwa chama cha Lieberman, Yisrael Beitenu kilichojinyakulia viti 9; Vyama vya Shas na cha umoja wa Torah Judaism vikijinyakulia viti 9 kila mmoja; cha mrengo wa kulia Yamina viti 7, na cha mrengo wa kushoto Labour-Gesher na Democratic Union alliances vikijanyakulia viti vitano na sita mtawalia.
Channel 12 News kimeviweka vyama vya Blue and White na cha Likud kujinyakulia viti 32 kila mmoja huku matokeo yaliobadilishwa ya Channel 13 News yakitabiri kuwa chama cha Blue and White kitashinda viti 32 huku cha Likud kikijinyakulia 30.
Kulikuwa na ukimya katika makao makuu ya chama cha Likud mjini Tel Aviv wakati matokeo hayo yakitangazwa ya baada ya kufungwa vituo vya kupiga kura.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamia ya viti vya wafuasi vilikuwa havina watu wakati wanaharakati wakiambiwa wasubiri nje ya ukumbi na viongozi wakitafakari matokeo hayo.
Mkurugenzi wa mambo ya nje wa chama cha Likud amesema kwamba matokeo hayo ya baada ya kufungwa vituo vya kura yamekoseka katika siku za nyuma.
Mara ya mwisho makadirio ya chini yalitolewa kwa kura ilizojinyakulia Likud na pia kwa baadhi ya vyama vya kidini vilivyo washirika wa Netanyahu.
"Hakuna maana ya kuanza kutafuta serikali ya muungano kwa kutumia matokeo haya kwasababu yatabadilika," Eli Hazan amesema.
Lakini chama cha Blue and White kimekuwa na matumaini kwa uangalifu kwamba Israel itapata uongozi mpya, msemaji Melody Sucharewicz ameliambia gazeti la Times of Israel.

Kura zitahesabiwa usiku kucha. Lakini huenda ikachukua wiki kadhaa za majadiliano ya kuunda serikali ya muungano kabla ya serikali mpya na waziri mkuu mpya kuibuka.
Uchaguzi huo umekuwa ni kura ya maoni kwa utawala wa miaka kumi ya mwisho kwa Benjamin Netanyahu.
Katika ngome za upinzani mjini Tel Aviv mhariri wa masuala ya mashariki ya kati wa BBC Jeremy Bowen, anasema kulishuhudiwa misururu mirefu ya wapiga kura waliokuwa wakisubiri kwa matumaini kusitisha uongozi wake wa kisiasa.
Kama kawaida yake Netanyahu alifanya kampeni nzuri tu hata kushirikishwa katika matangazo yake ya kumtangaza. Ujumbe wake ni kwamba yeye ndiye mtu pekee - aliye na marafiki wenye nguvu kama Donald Trump - kuwalinda raia Israel dhidi ya Iran na Palestina.
Mwandishi wa BBC Bowen anasema wakati akizunguka mjini Tel Aviv, amekutana na Avigdor Lieberman, ambaye anaweza kuwa mwanasiasa anayeogopewa na waziri mkuu wakati majadiliano ya kuunda serikali ya muungano yatakapoanza. Chama chake Yisrael Beiteinu huenda ndicho kikaleta mshindi wa siku.
Jambo moja muhimu ni kwamba licha ya kwamba alikuwa mshirika wa karibu wa waziri mkuu huyo , sasa ni wapinzani na pengine hata maadui.
Baada ya matokeo hayo baada ya kufungwa kwa vituo vya kupiga kura, wafuasi wa Lieberman ndio waliokuwa wakisherehekea peke yake. Iwapo matokeo yatathibitishwa mwisho wa siku - kwasababu matokeo huwa mara nyingi sio sahihi - basi huenda enzi ya utawala wa Netanyahu katika siasa za Israel inamalizika.

Nini kinachoweza kufanya baada ya hapa?
Mwandishi wa BBC Tom Bateman, anasema iwapo matokeo ya kura yatathibitishwa, Netanyahu atakuwa hana njia rahisi kuingia serikalini. Kwa hakika takwimu hizo zinamuweka katika nafasi dhaifu kuliko aliyokuwa baada ya uchaguzi wa Aprili wakati mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano yalipotibuka, anaongeza.
Huenda Gantz akaibuka kiongozi wa chama kikubwa, lakini huenda akawa na kibarua kigumu zaidi kuunda serikali.
Lieberman, ambaye ni mshirika aliyegueka kuwa hasimu mkubwa wa waziri mkuu, huenda akawa kiungo muhimu katika maamuzi ya nani atakayeingia uongozini.
Alimzuia Netanyahu kuunda serikali ya muungano baada ya uchaguzi uliopita lakini alikataa kurudi nyuma kuhusu mzozo wa muda mrefu na vyama vya kisiasa kuhusu mswada unaotoa msamaha kwa vijana wa kiothodoxi kuingia jeshini.

Chanzo cha picha, Reuters
Avigdor Lieberman anataka "serikali pana huru ya kitaifa"
Katika mkutano wa kisiasa mjini Jerusalem Jumanne usiku, Lieberman alisisitiza wito wake aliotoa wakati wa kampeni wa serikali ya muungano.
"Tuna uamuzi mmoja tu," aliwaambia wafuasi. "Serikali pana huru ya kitaifa inayojumuisha vyama vya Yisrael Beiteinu, Likud na Blue and White."
Mwandishi wetu anasema muungano huo unawezekana iwapo tu bwana Netanyahu atapinduliwa kama kiongozi wa Likud, wakati makundi ya upinzani yameapa kutokaa na yeye uongozini.
Uwezekano mwingine unaweza kutokea, ikiwemo uchaguzi mwingine, unaotatizwa kwa kesi dhidi ya Netanyahu kuhusu tuhuma za ufisadi. Waziri mkuu huyo anakana kufanya makosa yoyote
Iwapo matokeo hayo hayatatoa mshindi, itakuwa ni jukumu la rais Reuven Rivlin kuamua ni nani anayepata jukumu la kujaribu kuunda serikali.
Atakayechaguliwa atakuwa na muda wa siku 28 kufanya hivyo huku kukiwepo uwezekano wa kuongezwa muda usizidi wiki mbili baada ya hapo.













