Watu 36 wahofiwa kufa maji katika ajali ya boti kwenye Mto Congo - Kinshasa

A barge on the Congo river filled with passengers and cargo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maboti ambayo mara nyingi hubeba abiria wengi kupita katika mto Congo huwa na usimamizi mbaya

Takriban watu 36 hawajulikani walipo, baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuzama katika Mto Congo, karibu kabisa na mji wa Kinshasa, huko Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.

Ajali hiyo inajiri, ikiwa ni siku mbili tu zimepita tangu ajali nyingine ya treni itokee kusini mashariki mwa nchi hiyo na kugharimu maisha ya watu, kwa mujibu wa Waziri wa masuala ya kibinaadamu, Steve Mbikayi

Polisi nchini DRC wanasema kwamba, zaidi ya watu 70 waliokolewa katika ajali hiyo ya boti iliyotokea usiku na ambayo hata hivyo chanzo chake hakijawekwa bayana.

Boti hilo lilikuwa likisafiri kuelekea mji mkuu Kinshasa kutoka jimbo la Mai Ndombe kaskazini mwa mji huo.

Kwanini ajali za vyombo vya usafiri zimekua jambo la kawaida nchini DRC?

Mwandishi wa BBC aliyepo mjini Kinshasa, Mbelechi Msochi anaeleza kwamba ajali hizi hutokea mara kwa mara kutokana na uduni wa boti au mashua zinazotumika.

Anafafanua kwamba kwa ubora huo ni vyombo visivyostahili kutumika kusafirisha watu, lakini kutokana na ukosefu wa boti nzuri, huchangia watu kuendelea kusafiri na boti hizo duni.

Polisi wanaohusika na usafiri wa maji, wamebaini kwamba kulikuwa na zaidi ya abiria 100, na kwamba kwa mara nyingi wakati ajali za aina hii zinapotokea, ni nadra kwa maiti kupatikana.

Kadhalika usimamizi mbaya wa usafiri ndio changamoto nyingine kubwa inayoonekana kuchangia kuongezeka kwa ajali za aina hii.

Mbelechi anaeleza kwamba hakuna kamati au taasisi inayofuatilia maagizo yanayotolewa na serikali, mfano agizo la hivi karibuni la rais Felix Tshisekedi aliyesema kuwa hakuna mtu atakayeruhusiwa kuabiri ndani ya boti za usafiri pasi kuvaa mavazi maalum ya kujiokoa.

Mavazi ambayo mwandishi wa huyo wa BBC Swahili anasema gharama yake ni ya juu kwa waendesha maboti na mashua na hata wahudumu kuweza kumudu.

Ajali katika vivukio vya maji ni jambo la kawaida nchini humo, na mara nyingi hutokana na kujazwa abiria kupita kiasi, na vyombo vya usafiri visivyo salama.

Map

Abiria wengi wanaopanda katika maboti hayo yalio na urefu wa futi 130, hawawezi kuogolea.

Maboti hayo hutumika sana kama njia ya usafiri kutokana na usimamizi mbaya wa usafiri wa barabarani nchini Congo.

Maelezo ya video, Ni kwanini raia wanaishi kwa umaskini Congo licha ya utajiri wa nchi?