Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Makonda asema yupo tayari kuchukiwa na wanaume
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema yupo tayari kuchukiwa na wanaume wa Mkoa huo wanaokwazika na uamuzi wake wa kuwatetea wanawake, Limeripoti gazeti la mwananchi nchini Tanzania
Bwana Makonda amesema yupo tayari kuchukiwa na wanaume wa Mkoa huo wanaokwazika na uamuzi wake wa kuwatetea wanawake.
Amesema hawezi kukaa kimya kuangalia mateso ya wanawake yanayoweza kupatiwa ufumbuzi ikiwa wanaume watabadilika.
Makonda alikuwa akizungumza Jumapili katika Kanisa la Inuka Uangaze la Mtume Boniface Mwamposa maarufu 'Bulldozer' lililopo Kawe, Dar es Salaam.
Amesema wakati wa wanawake kutembea kifua mbele umefika na siku zote atasimama kuwatetea.
"Wanawake wakati wa kutembea kifua mbele umefika, kama mlimbeba mtoto miezi tisa hakuna jambo litakalokushinda. Wanaume mjipange, siwezi kukaa kimya kwa ajili ya mama," amesema Makonda.
Amesema baada ya kuwasilisha serikalini mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya ndoa, anajipanga pia kupeleka mabadiliko ya sheria ya mtoto.
"Katika sheria ya mtoto tumependekeza matunzo yaanzie mimba inapoingia, mtoto atunzwe kuanzia hapo. Wasichana wengi wanatelekezwa wakipata ujauzito kwa madai mimba imeingia kwa bahati mbaya." alisema Makonda.
"Wasichana wa kazi wanateseka, wanapewa mimba na mabosi zao na kufukuzwa wakiambiwa wataharibu ndoa. Kama unajijua una ndoa jisitiri na ndoa yako unahangaika ili iweje. Hadi niondoke kwenye huu mkoa kuna watu mtakuwa mmenyooka," amesema Makonda.
Katika hatua nyingine iliyoibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii miongoni mwa Watanzania, Mkuu wa mkoa huyo jana Jumapili alitangaza kuwa sasa anatoa kibali kwa viongozi wa dini kwenda kuhubiri kwenye kumbi za burudani usiku ili watu wasikie neno la Mungu, wasije kusema hawakusikia.
Alitoa onyo kwa kwa wamiliki wa klabu watakaozuia watumishi hao, na kwamba yeye ndiyo Mkuu wa Mkoa. Kauli hiyo ilinukuliwa na Swahili Times kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Baadhi walipinga kauli hiyo ya kupitia mitandao ya kijami mfano Tonny Adamms kupitia ukurasa wake wa Twitter alisema hakuna mmiliki wa klabu atayeruhusu hilo halitafanyika:
Wengine kama Mtoto wa Meko alijiuliza swali hili nae kupitia ukurasa wa Twitter:
Katika hatua nyingine ya kukabiliana na mienendo ya wanaume mwanzoni mwa mwezi wa Agosti Bwana Makonda alitangaza kuwa amepanga kuzisajiri ndoa zote za mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na wanaume wanaowalaghai wanawake kimapenzi.
Alisema kuna mpango wa kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo kwenye mkoa wake ili kupunguza utapeli wanaofanyiwa wanawake kwa kudanganywa kuolewa.
Kanzidata hiyo itahusisha usajili wa ndoa zote ili wanaume waliooa waweze kubainika na kuwanusuru wanawake wasitapeliwe na kuumizwa mioyo kwa kutegemea ndoa.
Makonda amesema pamoja na kanzidata hiyo atatumia mkutano wa SADC kupata uzoefu kutoka kwa nchi nyingine kufahamu namna gani wanakabiliana na utapeli wa aina hiyo.
Si mara ya kwanza kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwashangaza Watanzania kwa maamuzi anayoyayachukua , Jumapili ya mwishi ya mwezi wa Agosti aliwaita.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam alidai kwamba amekuwa akikutana na malalamiko mengi sana kutoka kwa wadada wa mkoa huo kwamba wamechoka kutapeliwa.
Mwezi Aprili mwaka 2018, Bwn.Makonda alitoa agizo kwa wanawake wanaodai kutelekezwa na wazazi wenzao kufika katika ofisi yake ili wapate kusikilizwa
Kufuatia taarifa hiyo mamia ya wanawake walijitokeza na kwenda katika ofisi yake kuelezea machungu waliyodai kupitia kutokana na kutelekezwa na wame zao.
Hatua hiyo iliibua hisia tofauti miongoni mwa Watanzani hususan katika mitandao ya habari ya kijamii, baadhi wakimkosoa na baadhi wakiafiki hatua yake ya kuwasikiliza akina mama.
Unaweza pia kutazama: