Uganda: Je,Uhaba wa huduma ya dharura ya zima moto ni tatizo linaloweza kupatiwa suluhu?

Chanzo cha picha, Reuters
Siku chache baada ya gari la mafuta kulipuka na kuua zaidi ya watu 80 huko mkoani Morogoro nchini Tanzania, huko nchini Uganda la watu 18 wamekufa baada ya gari lililobeba mafuta kuacha njia na kulipuka moto baada ya kuwafikia watu walio kuwa karibu na eneo hilo.
Msemaji wa jeshi la Polisi nchini Uganda, Fred Enanga amesema hapo jana siku ya jumapili majira ya saa kumi jioni gari la kubeba mafuta lilipuka katika soko la Rubirizi ,Kyambura magharibi mwa Uganda.
Dereva wa lori la mafuta lililokuwa linatokea maeneo ya Mbarara kwenda Kasese karibu na mpaka DRC, kuacha njia na kugonga daladala ndogo za abiria mbili na gari ndogo moja na zote kushika moto na kulipuka gari hilo la mafuta kulipuka hapohapo.
Miili 9 iliweza kupatikana kwa usiku huo na leo idadi ya miili imeongezeka kwa kupatikana kwa miili mingine 9 hivyo idadi kuwa jumla watu 18 wamefariki na wengine kujeuhiwa.
Mpaka sasa watu 10 ndio wameweza kutambuliwa huku miili mingine 8 inasubiri majibu ya vipimo vya vina saba kutoka kwa jamaa zao ili waweze kutambulika.

Chanzo cha picha, Reuters
Athari nyingine zilizopatikana katika ajali hiyo ni maduka yapatayo 25 yameateketea pamoja na vitu vyake vyote ndani.
Aidha msemaji huyo wa jeshi la polisi nchini Uganda ameeleza kuwa iliwachukua saa mbili kufika katika eneo la tukio kwa sababu huduma za kuzima moto katika eneo hilo ziko mbali na hiyo ndio changamoto kubwa iliyosababisha athari kutokea kwa ukubwa.

Je,Uhaba wa huduma ya dharura ya zima moto ni tatizo linaloweza kupatiwa suluhu?
Matukio haya ya moto yamekuwa yakihatarisha na kupoteza maisha ya watu wengi. Suala la kutoa elimu kwa Umma ni endelevu, si la mara moja kwani kujua kwa mmoja si kujua kwa mwingine.
Msemaji mkuu wa zima moto nchini Tanzania, Joseph Mwasabeja ameiambia BBC kuwa changamoto ya uhaba wa gari za zima moto inatokana kuwa na gharama kubwa , "Gari za zima moto sio gari kama gari nyingine kama wengi wanavyodhani ila ni mashine inayohitaji uwekezaji.
Kwa upande wa Tanzania jitihada zimeanza kuanzisha vituo vingi zaidi vya zima moto kwa kila wilaya", Mwasabeja amefafanua.
Gharama ya uwekezaji wa vituo hivyo vya dharura ni miongoni mwa changamoto kubwa inayokabili utendaji wa kazi zao kwa urahisi na bila kusahau miundombinu bado sio rafiki katika nchi za Afrika.
Msemaji huyo ameongeza kueleza kuwa watu wengi huwa wanatoa lawama kwa jeshi la polisi kuchelewa kufika lakini tatizo kubwa huwa lipo kwa wananchi pia kuchelewesha kutoa taarifa.
"mara nyingi watu hawajui namba za dharura hivyo taarifa zinachelewa kufika na huduma itachelewa ,kwa mfano wananchi kupambana na moto si kosa ila jambo la muhimu ni kuanza kutoa taarifa kwa watoa huduma hiyo".
Baadhi ya matukio ya mikasa ya malori ya mafuta Afrika
January 31 2009 Kenya: Moto uliwachoma watu waliokuwa wakifyonza mafuta wakati lori la mafuta lilipoanguka huko Molo kaskazini mwa mji wa Nairobi na kuwaoa watu 122.
Julai 2, 2010, DR Congo: Takriban watu 292 waliuawa wakati lori la mafuta lilipolipuka mashariki mwa kijiji cha Sange. Baadhi ya waathiriwa walikuwa wakijaribu kuiba mafuta baada ya ajali hiyo huku wengine wakitazama mechi ya kombe la dunia.
Oktoba 6, 2018 DR Congo: Takriban watu 53 waliuawa baada ya lori la mafuta kugongana na gari jingine na kushika moto katika barabara kuu ya mji mkuu wa Kinshasa
Septemba 16 2015 Sudan Kusini: Watu 203 walifariki na wengine 150 kujeruhiwa wakati watu walipokuwa wakijaribu kuiba mafuta.
Novemba 17 2016 Msumbiji: Takriban watu 93 waliuawa wakati lori la mafuta lililokuwa likibeba petroli lilipolipuka magharibi mwa taifa hilo . Mamia walikuwa wakijaribu kufyonza mafuta kutoka katika gari hilo.
Julai 12 2012, Nigeria: Takriban watu 104 walifariki walipokuwa wakijaribu kuchukua mafuta kutoka kwa lori la mafuta baada ya kuanguka kusini mwa jimbo la River State.
Oktoba 9 2009 , Nigeria: Takriban watu 70 walifariki kusini mashariki mwa jimbo la Anambra baada ya lori la mafuta kulipuka huku moto ikichoma magari kadhaa.
Agosti 2019: Lori la mafuta lilipuka Morogoro nchini Tanzania na kuua watu 89













