Ajali ya Morogoro: Magufuli asema sio wakati wa kulaumiana

Chanzo cha picha, Ikulu ya rais
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewataka raia nchini humo kutowahukumu waathirika wa mkasa wa moto uliosababisha vifo vya watu 71 mjini Morogoro siku ya Jumamosi.
Akizungumza baada ya kuwasili katika hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuwajulia hali majeruhi, Magufuli amesema kuwa baadhi ya walioathirika na mkasa huo walikuwa wamekwenda eneo la tukio ili kutoa msaada huku wengine wakiwa wapita njia.
Rais huyo amesema kwamba huu sio muda wa kulaumiana na badala yake akawashukuru baadhi ya Watanzania waliojitolea kuokoa maisha ya watu.
''Naona watu wanasema kwamba hawa wote walienda kuiba , tusiwe majaji wengine walienda kusaidia huku wengine wakiwa wapita njia , Mwengine alikuwa safarini kuelekea Mtwara, akazuiliwa na moto ulipolipuka ukamkuta'', alisema kiongozi huyo wa taifa.
Amesema kwamba serikali yake itauvalia njuga mkasa huo na kuwalipia gharama zote za matibabu waliojeruhiwa.
Amewataka raia wa taifa hilo kuendelea kuwaombea walioathirika huku akitoa shilingi lakini tano kwa kila majeruhi.
Idadi ya waliolazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili ni watu 43 wakiwa wamejeruhiwa kwa asilimia 80.
Jumla ya majeruhi waliopokelewa katika hospitali hiyo ni 46 huku watatu wakifariki mpaka Jumapili mchana. Katika Hospitali ya mkoa ya Morogoro ni majeruhi 15 pekee waliosalia .
Hatua hiyo inajiri baada ya Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania kusema kwamba vifo hivyo vimetokana na tabia mbaya miongoni mwa watu wanaochukulia ajali kama fursa ya kujipatia mali kwa njia haramu ilioanza katika miaka ya hivi karibuni.
Mwenyekiti wa wahariri nchini humo aliitaka serikali kuwafungulia mashtaka walionusurika mkasa huo akidai kwamba walikuwa na nia ya kupora.
Baadhi ya matukio ya mikasa ya malori ya mafuta Afrika
- January 31 2009 Kenya: Moto uliwachoma watu waliokuwa wakifyonza mafuta wakati lori la mafuta lilipoanguka huko Molo kaskazini mwa mji wa Nairobi na kuwaoa watu 122.
- Julai 2, 2010, DR Congo: Takriban watu 292 waliuawa wakati lori la mafuta lilipolipuka mashariki mwa kijiji cha Sange. Baadhi ya waathiriwa walikuwa wakijaribu kuiba mafuta baada ya ajali hiyo huku wengine wakitazama mechi ya kombe la dunia.
- Oktoba 6, 2018 DR Congo: Takriban watu 53 waliuawa baada ya lori la mafuta kugongana na gari jingine na kushika moto katika barabara kuu ya mji mkuu wa Kinshasa
- Septemba 16 2015 Sudan Kusini: Watu 203 walifariki na wengine 150 kujeruhiwa wakati watu walipokuwa wakijaribu kuiba mafuta.
- Novemba 17 2016 Msumbiji: Takriban watu 93 waliuawa wakati lori la mafuta lililokuwa likibeba petroli lilipolipuka magharibi mwa taifa hilo . Mamia walikuwa wakijaribu kufyonza mafuta kutoka katika gari hilo.
- Julai 12 2012, Nigeria: Takriban watu 104 walifariki walipokuwa wakijaribu kuchukua mafuta kutoka kwa lori la mafuta baada ya kuanguka kusini mwa jimbo la River State.
- Oktoba 9 2009 , Nigeria: Takriban watu 70 walifariki kusini mashariki mwa jimbo la Anambra baada ya lori la mafuta kulipuka huku moto ikichoma magari kadhaa.













