Clauvino da Silva: Mfungwa raia wa Brazil aliyevalia kama mwanawe wa kike ili kutoroka jela apatikana amefariki

Clauvino da Silva alipigwa picha katika jela ya Bangu, Gericino, Rio De Janeiro, Brazil, Agosti 3, 2019

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Silva alikuwa anahudumia kifungo cha miaka na miezi 10 jela kwa ulanguzi wa mihadarati

Mamlaka nchini Brazil imempata mfungwa mlanguzi wa mihadarati Clauvino da Silva amefariki katika chumba chake jela , siku tatu baada ya jaribio lake la kutaka kutoroka kuzuiwa.

Maafisa wa jela hiyo wanasema kwamba inaonekana kwamba Silva alijinyonga mwenyewe.

Walinzi wa siku ya Jumamosi walimzuia Silva alipojaribu kutoroka jela akiwa amevalia kama mwanawe wa kike.

Kanda ya video iliomuonyesha akivua nguo zilizomfanya kufanana na mwanawe wa kike ikiwemo barakoa na nywele bandia ilisambaa sana mitandaoni.

Silva alidhania kwamba umbo lake dogo litamsaidia kupita kama mwanawe wa kike

Chanzo cha picha, SEAP

Maelezo ya picha, Silva alivyojibadilisha

Silva alikuwa na umri wa miaka 42 na alikuwa anahudumia kifungo cha miaka 73 na miezi 10 kwa ulanguzi wa mihadarati.

Siku ya Jumanne walinzi walimpata katika chumba chake cha jela ya bangu 1 mjini Rio de Jeneiro ambapo alikuwa amehamishwa baada ya jaribio hilo la kutoroka.

Mtandao wa habari wa O Globo uliripoti kwamba alikuwa akizuiliwa akiwa pekee tangu uhamisho wake.

Presentational grey line

Silva aligonga vichwa vya habari baada ya kujaribu kutoroka kutoka jela ya Bangu 3 ambapo alikuwa amevalia barakoa , nywele bandia, miwani sidiria na tishati ili kuonekana kama mwanawe wa kike mwenye umri wa miaka 19 ambaye alikua amemtembelea.

Walinzi hawakufanywa wajinga na hatua hiyo na wakalazimika kumpiga picha alipokuwa akivua vitu hivyo moja baada ya chengine.

Mwanawe wa kike ambaye alikuwa amesalia katika jela hiyo huku babake akijaribu kutoroka anachunguzwa pamoja na watu wengine wanane kuhusiana na njama hiyo.

Silva alikuwa amewahi kutoroka jela mara moja mwaka 2013, wakati alipotumia bomba la maji taka la jela ya Gericin .lakini alikamatwa .