Kenya: Kwa nini wachuuzi wa Mama Ngina mjini Mombasa wanafurushwa?

Wachuuzi wanaofanya biashara mbali mbali katika bustani ya Mama Ngina mjini Mombasa wako njia panda baada ya kufurushwa kutokana na ujenzi unaoendelea hivi sasa wa mradi wa kuvutia watalii.
Wanasema kinyume na amri ya Rais Uhuru Kenyatta wasifadhaishwe kwenye biashara zao ujenzi wa mradi huo ukiendelea, wamejikuta taabani kwani tayari wameondolewa kwenye bustani hiyo na hivi sasa hawajui la kufanya huku wakikakabiliwa na mzigo mkubwa wa kulisha familia zao bila ajira.
Hussein Hassan Mwakuricho ni miongoni mwa wachuuzi waliofurushwa kutoka kwa bustani hiyo.
Hajui la kufanya kwa sababu pale aliko sasa kando ya barabara ametishwa kung'olewa na mwenye ardhi hiyo.
``Mwenye sehemu hii ya ardhi tayari ametisha kuniondoa,`` anasema Mwakuricho, ``tena hapa biashara iko chini sana. Mimi nafanya biashara ya kuuza mhogo na kachiri niliyoiridhi kwa babangu. Mama Ngina nimefanya kazi kwa zaidi ya miaka 20, watoto wangu nawasomesha kwa kuuza mihogo na kachiri. Mimi mwenyewe ni hii kachiri imenisomesha

``Sasa najiuliza wanataka niende wapi? Mradi huu wa Rais wetu Uhuru ni mzuri sana lakini umetuumiza sisi wachuuzi wa Mama Ngina.''
Ujenzi wa mradi huo ukiendelea, kuna vibanda vinavyojengwa humo ndani lakini kulingana na Mwakuricho kuna fununu za watu wa nje kunyakua vibanda hivyo kujinufaisha wenyewe.
``Tunasikia kwamba kuna matajiri wanavitolea macho vitakapokamilika. Sisi wachuuzi wa Mama Ngina tuko wengi. Kuna wapiga picha, wauzaji madafu, mama ntilie wote wanajua vibanda hivi ni vyetu lakini sasa kama vitapewa matajiri hao sisi watu wa chini tutafanya nini. Tutazidi kuumia bila kujua vile tutalipa mikopo yetu ya benki.''
Mwakuricho anashangaa jinsi wanavyotatizika huku akisema kupata kazi nchini Kenya ni shida hivyo anashindwa afanye nini.
``Ndio kwa maana baadhi ya vijana hapa Mombasa wanajihusisha na ujambazi kwa sababu ya mambo kama haya. Hata mimi mwenyewe sitakubali watoto wangu walale njaa huku matajiri wanatufinya mpaka kwa biashara zetu tunaondolewa. Kazi hawatupi,'' anasema Mwakuricho.
Mwenyekiti wa wachuuzi hao Salim Dzombo Bawazir ametoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati suala hili, naye pia akidai kuna mpango wa kunyakua vibanda vya wachuuzi.

Anasema Bawazir:``Mimi kama mwenyekiti wa wachuuzi hawa namuomba Rais wetu tunayempenda atuokoe. Hatutakubali kunyanyaswa kwa haki yetu. Vibanda hivyo vipewe wachuuzi. Mimi mwenyewe naumia sana kwa sababu nina mikopo ya benki na deni zingine za biashara yangu Mama Ngina. Watoto sasa hawaendi shule sijui la kufanya. Mpaka tunajiuliza tuko Kenya kweli?.''
Abraham Macho amekuwa akitafakari aende wapi. Jengo lake ambalo lilikua linamletea chakula limebomolewa.
``Jengo langu lilikua la kuweka mizigo ya wachuuzi hapa Mama Ngina lakini sasa haliko tena. Askari wa kaunti wamelibomoa bila huruma ya kujiuliza nitajikidhi vipi kimaisha,`` anasema Macho.
Binti Athumani ameiambia BBC kwamba Rais Uhuru Kenyatta alipozindua mradi huo alisema ujenzi ukiendelea watafutiwe nafasi hapo waendelee na biashara zao.
``Kama nijuavyo mimi Rais wetu alisema ile sehemu tuko tuwape nafasi wakikaribia nasi twende sehemu nyingine hapa hapa Mama Ngina lakini sio kufukuzwa kabisa kama ilivyo sasa,'' anasema Binti Athumani kwa uchungu huku machozi yakimdondoka.
``Hawa wanatujali tu wakitaka kura zetu lakini sasa wameshiba hawajalii kabisa maslahi ya walala hoi. Twende wapi sisi watu wa chini masikini. Inauma sana hasa kwa mtu kama mimi mzaliwa wa pwani. Nimekua hapa tangu enzi za Rais Moi na mnarehemu Shariff Nassir.''

Mkuu wa ujenzi wa mradi huo wa kuvutia watalii Irfan Hobayo amekanusha madai ya wachuuzi hao, akisema wanatilia maanani maslahi yao hasa ujenzi wa vibanda.
``Hata waziri (Najib Balala) amesema hivi vibanda ni vya hawa wachuuzi. Mradi ukiwa tayari tutawapa. Kwa hivyo sio kweli wanavyosema kuna mpango wa kuwanyima vibanda hivi vinavyojengewa.``
Jitihada za BBC za kuzungumza na waziri wa utalii Najib Balala ziliambulia patupu.
Mwandishi wetu alimpigia simu mara kadhaa lakini hakujibu pamoja na ujumbe mfupi wa simu.














