Aaron Wan-Bissaka: Man United yafikia makubaliano na Crystal Palace

Aaron Wan-Bissaka

Chanzo cha picha, EPA

Manchester United imefikia makubaliano na klabu ya Crystal Palace ya kumnunua beki wa kulia Aaron Wan-Bissaka.

Bissaka anaelekea Old Trafford kwa dau la pauni milioni 50, na mchezaji huyo anayechezea timu ya taifa ya chini ya miaka 21 ya England atafanyiwa vipimo kabla ya kwenda mapumzikoni hivi karibuni.

United imetoa ofa ya mkataba muda mrefu na mshahara wa pauni 80,000 kwa wiki.

Bissaka analipwa pauni 10,000 kwa wiki, mshahara mdogo zaidi kuliko mchezaji yeyote wa kikosi cha kwanza wa Palace.

Wan-Bissaka, ambaye alikuwa na jukumu mwezi huu kukichezea kikosi chake cha chini ya miaka 21 kwenye michuano ya Ulaya, alijiunga na shule ya mpira ya Crystal Palace alipokuwa na miaka 11

Kwa kitita hicho, atakuwa miongoni mwa wachezaji watano wa Old Trafford kusajiliwa kwa dau kubwa nyuma ya Paul Pogba,Romelu Lukaku, Angel di Maria na Fred.

Aaron Wan-Bissaka akiwa kwenye mpambano Crystal Palace na Bournemouth

Chanzo cha picha, Getty Images

Makubaliano hayo yamechukua muda mrefu kutokana na mjadala wa kima cha asilimia 25 ya mauzo mabacho United walikweka kwenye mkataba wa Wilfried Zaha wakati makiwauzia Palace mshambuliaji huyo kwa pauni milioni 6 mwezi Februari 2015.

Palace walitaka kima hicho kiondolew au kupunguzwa, lakini United wamegoma kabisa - wakisema usajili huo ulikuwa wa bei chee.

Hii ina maana ya kuwa, endapo Palace watamuuza Zaha, United watapata asilimia 25 ya pesa hiyo.

Wissaka atakapokamilisha vipimo na kusajiliwa, atakuwa mchezaji wa pili kusainiwa katika dirisha hili la usajili, baada winga Daniel James ambaye wamemnasa kutoka Swansea kwa pauni milioni 15.