Ghuba ya Oman: Marekani kupeleka vikosi vya kijeshi kutokana na mzozo kati yake na Iran

Picha zikionyesha chombo kikiwa kimeharibiwa

Chanzo cha picha, US Department of Defense

Maelezo ya picha, Marekani yaonyesha picha ikisema ni ushahidi kuhusu mashambuizi kwenye Ghuba ya Oman

Jeshi la Marekani litatuma kikosi zaidi cha wanajeshi 1,000 kwenda Mashariki ya Kati wakati kukiwa na hali ya mvutano na Iran.

Waziri wa ulinzi Patrick Shanahan amesema hatua hiyo ni kutokana na kile alichodai kuwa ''tabia za uchokozi'' zinazodaiwa kufanywa na vikosi vya Iran.

Vikosi vya maji vya Marekani vilionyesha picha mpya, wakiihusisha Iran na vitendo vya mashambulizi dhidi ya meli ya kubeba mafuta katika Ghuba ya Oman.

Iran ilitangaza siku ya Jumatatu kuwa haitatekeleza sehemu ya makubaliano ya mwaka 2015 kuhusu nyukilia.

Ilisema itavunja makubaliano yaliyofikiwa na mataifa yenye nguvu kuhusu zana za nyukilia ifikapo tarehe 27 mwezi Juni.

Tunachofahamu kuhusu vikosi vya nyongeza

Kutumwa kwa vikosi vya Marekani kwenye eneo la Mashariki ya kati kulitangazwa na Bwana Shanahan mapema siku ya Jumatatu.

Katika taarifa yake,alisema ''Marekani haitafuti mgogoro na Iran'' lakini hatua imechukuliwa ili ''kuhakikisha kunakuwa na usalama na ustawi wa wanajeshi wanaofanya kazi katika ukanda huo kulinda maslahi ya taifa''.

''Mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran yanaonyesha wazi ni vitendo vya kichokozi vya vikosi vya Iran na mawakala wake ambayo yametishia wanajeshi wa Marekani na maslahi yake katika ukanda mzima.''

Alisema Jeshi litaendelea kufuatilia hali ilivyo eneo hilo na kufanya marekebisho ya vikosi ipasavyo.

Donald Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu eneo gani Marekani itapeleka vikosi vyake.

Tangazo la Jumatatu kuhusu kuongezwa kwa idadi ya vikosi limekuja ikiwa ni kando ya lile la vikosi 1,500 vilivyotangazwa na Rais Donald Trump mwezi uliopita.

Waziri wa mambo ya nje, Mike Pompeo alisema siku ya Jumapili kuwa Marekani haikutaka vita na Iran, lakini hata hivyo ''imekuwa ikifikiria kuwa na namna ya kufanya''.

Picha za sasa zinaonyesha nini?

Muda mfupi baada ya tangazo, Pentagon ilitoa picha mpya ikiwemo baadhi zikionyesha mabaki ya mabomu ambayo hayakulipuka katika meli ya mafuta inayomilikiwa na Japan.

Picha zinaonyesha ikiondolewa na maafisa wa polisi wa Iran.Pentagon imeshaonyesha video inayoonyesha tukio hilo.

Pia katika picha za karibuni palionekana tundu kwenye chombo usawa wa mstari wa maji wa chombo cha Kokuka.

PICHA

Chanzo cha picha, EPA

Meli ya mafuta ya Norway, the Front Altair, pia imeripotiwa kulipuliwa siku ya Alhamisi.

Marekani imeonyesha kuhusika kwa Iran katika mashambulizi ya hivi karibuni na mashambulizi mengine manne nje ya lango la Hormuz linalotenganisha ghuba ya uajemi na ghuba ya Oman mwezi Mei.

Iran imekana kuhusika na vitendo hivyo na kusema shutuma za Marekani ''hazina msingi''.

Kwa nini mvutano huu mpya?

Mwaka 2015, Iran ilikubali kutekeleza makubaliano yaliyowekwa na mataifa yenye nguvu kupambana na urutubishaji wa nyukilia.

ilikubali kiasi cha urutubishaji wa madini ya urani, ambayo hutumika kutengeneza silaha za nyukilia, na hatua nyingine ili kupata nafuu ya vikwazo.

Bwana Trump aliamua kuachana na mkataba huo mwaka jana na kuiwekea tena vikwazo.

Uamuzi huo uliathiri uchumi wa Iran, ambao ulitegemea sana mafuta, na Iran ikajibu kwa kuvunja makubaliano kuhusu nyukilia.

Siku ya Jumatatu, msemaji wa shirika lake la nguvu za Atomiki alisema Iran ina mpango wa kuvuka ukomo uliowekwa kuhusu urutubishaji madini ya urani katika kipindi cha siku kumi.

Lakini,Iran imesema bado ''muda upo'' kwa mataifa ya Ulaya kuchukua hatua kuilinda Iran dhidi ya vikwazo vya Marekani.

Marekani ilijibu kwa kushutumu Iran kwa kutumia nguvu kuhusu suala la nyukilia.

Uingereza, Ufaransa,Ujerumani zimeionya Iran kutokiuka mkataba wa mwaka 2015.