Eid ul-Fitr 2019: Waislamu kuadhimisha Eid lini?

Mwezi mtukufu wa Ramadhan umefikia ukingoni, na sikukuu ya Eid ul-Fitr inanukia.
Swali kwa walio wengi ni lini waislamu watasherehekea sikukuu hiyo?
Jawabu litategemea na mahali mtu alipo.
Kwa kawaida mwezi wa ramadhan hukamilika kwa siku 29 ama 30, kulingana na kuandama kwa mwezi.
Waislamu wa Kenya walianza mfungo wa Ramadhan kwa mwaka 2019 Jumatatu ya Mei 6, na leo kwao ni mwezi 29 Ramadhan, jioni watatazama mawinguni kuutafuta mwezi.
Endapo mwezi utaonekana popote pale Kenya basi kesho watasali sala ya Eid na kushereheka.

Hata hivyo kuna uwezekano wasiuone, na ikitokea hivyo watamalizia kufunga siku ya 30 na kusali Eid Jumatano.
Tayari serikali ya Kenya kupitia waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya ametangaza kupitia gazeti la serikali kuwa siku ya Jumatano itakuwa ni siku ya mapumziko ya kitaifa kusherehekea Eid.
Kwa upande wa Tanzania, rasmi waislamu walianza kufunga siku moja mbele ya Kenya yaani Jumanne Mei 7, na leo kwao ni mwezi 28 Ramadhan, hivyo kesho Jumanne Juni 4 lazima wafunge ili kutimiza siku 29 ili watazame mwezi muandamo.
Hivyo Eid kwa Tanzania inaweza kugongana na Kenya kwa siku ya Jumatano.

Endapo mwezi hautaonekana Jumanne, basi Tanzania itaendelea kusalia Ramadhani siku ya Jumatano ili kukamilisha siku 30 za Ramadhan na Eid itasaliwa Alhamisi.
Tofauti na Kenya, nchini Tanzania sikukuu hiyo huadhimishwa kwa siku mbili za mapumziko ya kitaifa.
Tayari Baraza Kuu la Waislamu nchini humo limeshatangaza kuwa Idd itakuwa Jumatano ama Alhamisi.
Tofauti ya kuanza kufunga na kusherehekea Eid miongoni mwa waislamu zaidi ya bilioni 1.8 duniani kote ni mjadala ambao uanaendelea kufukuta na bado hakuna suluhu iliyopatikana.
Na pia yawezekana suluhu juu ya tofauti hizo isipatikane, na kila upande kuendelea na msimamo wake.
Eid ul-Fitr ni nini?

Eid ul-Fitr maana yake ni "sikukuu ya kumaliza mfungo" na kutumiwa kuadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Siku hii huwa ni siku rasmi ya mapumziko katika mataifa mengi yenye waumini wengi wa Kiislamu. Hata hivyo idadi ya siku za mapumziko huwa tofauti katika nchi mbalimbali.
Waislamu huanza sherehe hizi kwa kukusanyika kwa maombi ya kila mwaka ambayo hufanyika muda mfupi baada ya macheo.
Ni kawaida kuwaona Waislamu wakikusanyika katika misikiti na viwanja vya wazi kwa maoni ya pamoja.
Kabla ya ibada hiyo, huwa wanatoa sadaka kwa maskini (huitwa Zakat ul-Fitr) ambayo ni moja ya nguzo kuu katika dini ya Kiislamu.
Ni kawaida kwa miji mikuu mataifa ya Kiislamu kupambwa sana na sherehe kubwa kuandaliwa, watoto kununuliwa nguo mpya na kupewa zawadi mbalimbali.












