Tanzania: Mganga anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mtoto akamatwa

Polisi nchini Tanzania wamemkamata mganga wa jadi anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mtoto mwenye miaka sita anayedaiwa kuuzwa na baba yake na baadaye kuuawa na kunyofolewa viungo vyake.

Mpaka sasa idadi ya watu waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji ya mtoto huyo , wamefika wanne.

Washukiwa katika kesi hiyo ni baba wa mtoto na mmiliki wa shule moja ya sekondari katika mkoa wa Mbeya, nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

Kamanda wa Polisi wa Mbeya Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo siku 10 zilizopita (Mei 03), ambapo baba anadaiwa kumuuza mtoto wake kwa wauaji kwa Sh5 milioni takribani $2,200.

Polisi wanabainisha kuwa mwili wa mtoto huyo ulitupwa katika msitu wa Hifadhi wa Chimala wilayani Mbarali na baada ya baba wa mtoto kukamatwa alikiri kuhusika na kueleza kuwa mguu wa mtoto umefukiwa kilomita 70 kutoka eneo alipouawa wilayani Mbalizi.

"Baada ya mmiliki wa shule kutajwa na kukamatwa, alikiri kuhusika na tukio hilo na wawili hao wapo mahabusu kupisha uchunguzi zaidi,"amesema Kamanda Matei.

Polisi wanasema kuwa mnamo tarehe 9/05 /2019 , walipokea taarifa kutoka kwa mzazi wa mtoto huyo kuwa mtoto amepotea, lakini baada ya ufuatiliaji waligundua kuwa mtoto huyo alikuwa anaishi na baba yake peke yake jambo ambalo ni kinyume cha sheria za Tanzania.

Na mazingira ya kupotea kwa mtoto huyo , uchunguzi ulionyesha kuwa baba wa mtoto anahusika kumuuza na kumtoa baadhi ya viungo vya huyo mtoto.

Mtoto huyo ambaye aliuwawa , kiganja cha mkono na mguu wa vilipatikana katika maeneo mawili tofauti na mwili wa marehemu na hata nyayo ilipatikana tofauti.

Aidha polisi alisema hawezi kueleza kila kitu kilichotokea kwa sababu za usiri wa kesi hiyo na uchunguzi uweze kuendelea.

Mauaji ya watoto Tanzania

Mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu Tanzania ilitikiswa na mauaji ya watoto chini ya miaka 10 katika mikoa ya Njombe na Simiyu.

Katika visa vyote hivyo, imani za kishirikina zimekuwa zikihusishwa kuwa ni chanzo kikuu.

Miili ya watoto hao wote ilikuwa ikinyofolewa baadhi ya viungo ikiwemo macho, pua meno masikio na viungo vya uzazi.

Waganga wa kienyeji wametupiwa lawama za kuwaaminisha watu kuwa viongo vya watoto hao vinauwezo wa kuchochea utajiri na bahati.

Washukiwa watatu mkoani Njombe ikiwemo ndugu wa karibu wa moja ya mtoto aliyeuawa tayari wameshafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Polisi ilibidi wakite kambi Njombe ili kukabiliana na wimbi la mauaji hayo huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akilihakikishia bunge mwezi Februari kuwa kuna hatua za makusudi zinachukuliwa na serikali mkoani Njombe.