LHRC: Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimezindua ripoti ya 2018 Tanzania

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Anna Henga

Chanzo cha picha, LHRC/Twitter

Maelezo ya picha, Mkurugenzi Mtendaji wa (LHRC), Bi. Anna Henga katika uzinduzi wa ripoti ya Haki za Binadamu 2018
Muda wa kusoma: Dakika 4

Zaidi ya visa 6000 vya ukatili au unyanyasaji dhidi ya watoto ikiwemo ukatili kiongono viliripotiwa mnamo 2018, kimebainisha Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) katika ripoti yake mpya iliyozinduliwa leo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliopewa jina "Ukatili wa Kingono: Tishio kwa Haki na Ustawi wa Mtoto Tanzania", iliowasilishwa na mwakilishi wa LHRC Fundikila Wazambi, haki ya kwanza kuvunjwa ni haki dhidi ya Ukatili.

"...Mambo yaliyoathiri haki za binadamu Tanzania kwa mwaka 2018 ni pamoja na Sheria kandamizi, Ukatili dhidi ya watoto, hasa matukio ya mauaji na ulawiti wa watoto... " ameeleza Fundikila ambaye pia ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo.

Imani za kishirikina zimetajwa kuchochea ukatili dhidi ya watoto huku watoto wenye ulemavu bado wakibaguliwa na kukabiliwa na ukatili...ikiwemo kufichwa.

Janga la mauaji ya watoto katika baadhi ya maeneo nchini ikiwemo mkoani Njombe, kusini magharibi Tanzania bado limegubika vyombo vya habari nchini tanzania tangu mapema mwaka huu.

Mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu Tanzania ilitikiswa na mauaji ya watoto chini ya miaka 10 katika mikoa ya Njombe na Simiyu.

Maelezo ya video, Haki 5 za binaadamu zilizovunjwa zaidi Tanzania 2018

Katika visa vyote hivyo, imani za kishirikina zimekuwa zikihusishwa kuwa ni chanzo kikuu na tayari mamlaka nchini Tanzania zimewakamata washukiwa kadhaa.

Kadhalika, haki za kujieleza na kukusanyika pia zinaarifiwa kukiukwa Tanzania na hilo LHRC inasema limeendelea kuathiri kukua kwa vyama vya siasa nchini.

Ripoti hiyo iliyoandikwa na LHRC kwa upande wa Tanzania bara, na ZLSC kwa upande wa Zanzibar, imeeleza kwamba uhuru wa kujieleza umezidi kudorora ikiwa imechangiwa na sheria mbalimbali ikiwemo ya sheria ya makosa ya mtandaoni, hususan kanuni zake za mwaka 2018 na nyinginezo ambazo zinatajwa kuchangia sana kudorora kwa uhuru na haki hii.

Ripoti hiyo ya mwaka huu imegusia haki za kisiasa, kiraia , kijamii na makundi ya watu walio katika hatari.

Ruka X ujumbe, 1
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 1

Ripoti ya LHRC 2018 imetolewa wakati ambapo mashirika yasio ya serikali 38 nchini Tanzania, barani Afrika na kimataifa yametoa wito kupitia barua iliyochapishwa kwa wanachama wa baraza la haki za bnaadamu katika Umoja wa mataifa kuchukua hatua kuhusu hali nchini Tanzania.

Ruka X ujumbe, 2
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 2

Katika barua hiyo yanaeleza kwamba nafasi imeendelea kupungua kwa watetezi wa haki za binaadamu, mashirika ya kiraia, waandishi habari, wamiliki blogu, wapenzi wa jinsia moja, upinzani na sauti jumla zinazoikosoa serikali.

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas ameipongeza ripoti hiyo na kusema hiyo ni sehemu ya demokrasia kwa sababu inazungumza tatizo ambalo lipo katika jamii.

Watoto wanakumbana na matukio mbalimbali ya ukatili hivyo ni wito kwa wanajamii kama wazazi, walezi kutimiza wajibu wetu katika ngazi ya familia, mtaa na taifa.

"Serikali imetimiza wajibu wake kwa kuweka mfumo wa kumtetea mtoto kisheria" Dkt.Abas aeleza.

Aidha Dkt Abas amesisitiza kuwa ameisoma ripoti hiyo na kuona kuwa kuna mikanganyo katika uwasilishaji wake jambo ambalo siku za mbeleni inabidi waboreshe.

Kwa kugusia eneo la uhuru wa habari kuwa wamepima vipi huo uhuru, ukosoaji wa serikali na kuna mambo mengine wametaja matukio ambayo yalishatolewa mahamuzi na mahakama je iweje ripoti inachapisha masuala hayo kuwa kukiukwa kwa haki za binadamu.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki Augustine Mahiga amewahi kusema kutofautiana kwa mitazamo na baadhi ya mataifa hayo kuhusiana na suala la haki za binadamu kunatokana na utofauti wa tafsiri ya misingi ya haki za binadamu.

"Mara nyingi watu wanapozungumzia suala la haki za binadamu wanapiga picha kwa mara moja bila kutazama mazingira yote, bila kutazama limetokana na nini na limetokea wapi na kwa nini suala hilo limezungumzwa?

Hapa katikati kumekuwa na masuala mbalimbali ambayo hayakufafanuliwa vizuri, misingi ya haki za kibinadamu huwezi kuchanganya na utamaduni wa nchi, huwezi kuchanganya na sheria za nchi na kuchanganya na misimamo ya kidini na Imani za watu." Mahiga ameieleza BBC.

Visa vya mauaji ya kutoweka kwa watu Tanzania

  • Mauaji ya Kibiti mwaka 2017: Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuwawa na watu wasiojulikana.
  • 11 Februari, 2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni.
  • Mnamo 7 Septemba, 2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.
  • 21 Novemba, 2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.
  • Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajulikani alipo.

Serikali ya Marekani katika ripoti ya haki za binaadamu ya mwaka 2018, imeeleza kwamba licha ya serikali ya Tanzania kuchukua hatua kuwashtaki maafisa ambao wamekiuka haki za binaadamu, lakini impunity imesambaa katika idara ya polisi na vitengo vingine vya usalama na vya kiraia ndani ya serikali.

Ripoti hii ya LHRC imetokana na mkusanyiko wa matukio yalioripotiwa ya ukiukaji wa haki za binaadamu tangu mnamo 2018 kupitia vyombo vya habari na pia kwa kutathmini nyaraka mbali mbali ambapo kumekuwepo ripoti za wanasiasa wa upinzani na wakosoaji wa serikali waliokamatwa, kushambuliwa na wengine hata kuuawa na watu wasiojulikana.