Bobi Wine awataka vijana wajisajili kupiga kura

Muda wa kusoma: Dakika 2

Mwanamuziki maarufu na mbunge wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi au Bobi Wine amewataka vijana nchini Uganda kujisajili kwa wingi kwa ajili ya kupiga kura ikiwa wanataka mabadiliko ya utawala nchini humo,limeripoti gazeti la kibinafsi la the Monitor nchini humo.

Mbunge huyo wa Kyadondo Mashariki ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa rais Yoweri Museveni wakati mmoja alituma ujumbe wake wa twitter akisema nchi yake imegeuka na kuwa kama kichekesho kutokana na mipango ya kuondoa ukomo wa umri wa rais.

Mwishoni mwa juma alikusanya umati mkubwa wa vijana katika wilaya ya Ntungamo akiwataka kujiandikisha kwa wingi ili kuung'oa madarakani utawala wa uliopo madarakani katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2021.

Bobi Wine ambaye mikutano yake kwa umma imekuwa ikivunjwa mara kwa mara na maafisa wa usalama nchini humo, alifanikiwa kusimama katika mji wa Rubaare wilayani Ntungamo njiani ,muda mfupi baada ya kushiriki ibada katika kanisa la All Saints Rubaare la Uganda.

Akiwa amevalia suti ya rangi ya kijani , Bobi Wine aliambatana na baba mkwe wake Dr Joseph Kagaju, mkewe Babra Itungo na watu wengine wa familia yake walipoingia kanisani na alipopewa muda wa kuongea , aliepuka kuzungumzia siasa kanisani.

"Nina bahati sana kwamba nipo hapa katika kanisa hili na ninawapenda sana watu wa Rubaare, sitaongea lolote juu ya siasa kwasababu niko pamoja na watu ambao jhawapendi siasa. Ninawashukuru sana kwa kuwa nasi ," alisema Bwana Kyagulanyi.

Muda mfupi tu baada ya hotuba yake, Bobi Wine aliwaacha waliomsindikiza , na kwenda kusimama kwenye kituo cha kuuza Petroli.

Mara gari lake likazingirwa na vijana wengi waliokuwa na ari ya kutaka kumsikiliza. Alijaribu kuwaepuka kwa dakika kadhaa lakini baadaye aliwapa ujumbe uliowataka wajitokeze kwa wingi kuung'oa madarakani utawala uliopo madarakani.