Kunyongwa kwa kuuwa Wakristo Misri

Mahakama nchini Misri imewahukumu wanaume wawili kunyongwa baada ya kuwashambulia wakristo wa dhehebu la Khufti (Coptic) mwaka 2017 na kusababisha watu 10 kuuwawa.

Mwanaume mmoja mwenye silaha kwanza alifyatua risasi katika duka moja linalomilikiwa na mkristo jijini Cairo, ba baadae alifyatua risasi kwa waumini waliokuwa wanaongia kanisani.

Kundi la kiislamu la Islamic state lilisadikiwa kuwa nyuma ya shambulio hilo.

Mwanaume mmoja kati ya wawili waliohukumiwa kunyongwa alijaribu kutoroka.

Washtakiwa wengine wawili walihukumiwa kifungo cha maisha.

Hofu ya wakristo nchini Misri ilianza mwaka jana, ambapo watu takribani 50 waliuwawa katika shambulio lililotokea katika makanisa mawili, wakati wa sherehe za sikukuu ya matawi mwaka 2018.

Kumbukumbu na masalia ya waliouawa katika shambulio hilo bado yamehifadhiwa katika kanisa la Mtakatifu Mina, lililopo eneo la jangwa nchini Misri.

Mapadre kutoka dhehebu hilo wanasema kuwa historia ya wakristo katika eneo hilo , kudharauliwa katika imani haina utofauti na zama za kale.

Wafuasi wa kundi la kiislamu la IS walisema kuwa wamewalenga wakristo zaidi.

Hakuna uhakika bado kama matukio kama haya hayatajirudia katika eneo hilo.

' Mzee mmoja anasimulia jinsi alivyompoteza mtoto wake '

Wakati shambulio hilo linatokea katika mlango wa kuingilia kanisani, mzee Gergis Bakhoom alikuwa amekwisha kuondoka katika eneo hilo.

Alikuwa nyuma ya duka dogo la mzee mwenye umri wa miaka 82 kipindi ambacho shambulio lilipoanza.

Mzee huyu anasema aliposikia mlio wa mlipuko, alikimbilia hospitali na kushuhudia hali ya mtoto wake mkubwa , Ibrahimu na alikuta akikata roho.

'Hatuna thamani hapa'

Bomu la mwisho kupigwa lilimpata Marian Abdel Malak akiwa na wapendwa wake watatu na miongoni mwao alikuepo mdogo wake mwenye umri wa miaka 18.

"Hivi karibuni , nimekuwa nikienda kanisani mara kwa mara na nmewaambia familia yangu kuwa nnataka kufa kama shujaa wa kidini.

Kila mtu anasubiri muda ambao watatakiwa kufanya kile ambacho wenzao walifanyiwa", kwa mujibu wa Marian.

"Kama hali itaendelea kuwa ya hofu namna hii, kama hatutapata hakizetu basi hatuna maisha tena hapa, bora tufe kwa sababu hatuna sehemu yetu katika nchi hii, au hata serikalini, hatuna thamani yeyote hapa", mkristo mwenye umri wa miaka 26 alieleza.

Mamlaka inapaswa kuongeza ulinzi.

Mwaka 2011, watu wawili waliuwawa baada ya kanisa la Alexandria kushambuliwa .

Ingawa ulinzi umeongezwa baada ya mashambulio ya hivi karibuni lakini wakristu bado wana hofu.

Wakhufti ni kina nani?

Wafuasi wa kanisa hilo wanafikia asilimia 10 ya raia wote wa Misri.

Kanisa hilo linaongozwa na Papa Tawadoros II.

Wakhufti walijitenga na madhehebu mengine ya kikristo mwaka 451, hivyo ni moja ya makanisa makongwe zaidi duniani.

Kanisa hilo linachukuliwa kuwa ndio kubwa zaidi katika Mashariki ya Kati, na pia lina wafuasi zaidi ya milioni moja nje ya Misri.