Baba 'amuuza' mtoto kwa wauaji Tanzania kwa $2,000

Ulrich Matei

Chanzo cha picha, POLISI, TANZANIA

Maelezo ya picha, Kamanda wa Polisi Mbeya Ulrich Matei athibitisha kuuawa kwa mtoto aliyeuzwa na baba yake

Polisi nchini Tanzania inawashikilia watu wawili kwa mauaji ya mtoto wa miaka sita ambayo yanahusianishwa na imani za kishirikina.

Washukiwa katika kesi hiyo ni baba wa mtoto na mmiliki wa shule moja ya sekondari katika mkoa wa Mbeya, nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

Kamanda wa Polisi wa Mbeya Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo siku 10 zilizopita (Mei 03), ambapo baba anadaiwa kumuuza mtoto wake kwa wauaji kwa Sh5 milioni takribani $2,200.

"...(baba) alikubali kumtoa mtoto wake kwa (jina linahifadhiwa) ambaye ni mfanyabiashara wa shule ya sekondari ili ili akatwe kanyagio la mguu wa kulia kwa ajili ya kutengenezea ndagu (dawa ya utajiri) kwa ajili ya kuendeshea biashara zake," Kamanda Matei amewaambia wanahabari.

Polisi wanabainisha kuwa mwili wa mtoto huyo ulitupwa katika msitu wa Hifadhi wa Chimala wilayani Mbarali na baada ya baba wa mtoto kukamatwa alikiri kuhusika na kueleza kuwa mguu wa mtoto umefukiwa kilomita 70 kutoka eneo alipouawa wilayani Mbalizi.

"Baada ya mmiliki wa shule kutajwa na kukamatwa, alikiri kuhusika na tukio hilo na wawili hao wapo mahabusu kupisha uchunguzi zaidi,"amesema Kamanda Matei.

Kwa sasa polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi ikiwemo kumsaka mganga aliyehusika na tukio hilo.

Mauaji ya watoto Tanzania

Washukiwa wa mauaji ya watoto Njombe
Maelezo ya picha, Washukiwa wa mauaji ya watoto Njombe walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Februari 12, 2019.

Mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu Tanzania ilitikiswa na mauaji ya watoto chini ya miaka 10 katika mikoa ya Njombe na Simiyu.

Katika visa vyote hivyo, imani za kishirikina zimekuwa zikihusishwa kuwa ni chanzo kikuu.

Maelezo ya video, Muaji Njombe: "Matumaini ya mama yaliokatizwa kwa mwanawe aliyeazimia kuwa Daktari

Miili ya watoto hao wote ilikuwa ikinyofolewa baadhi ya viungo ikiwemo macho, pua meno masikio na viungo vya uzazi.

Waganga wa kienyeji wametupiwa lawama za kuwaaminisha watu kuwa viongo vya watoto hao vinauwezo wa kuchochea utajiri na bahati.

Washukiwa watatu mkoani Njombe ikiwemo ndugu wa karibu wa moja ya mtoto aliyeuawa tayari wameshafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Polisi ilibidi wakite kambi Njombe ili kukabiliana na wimbi la mauaji hayo huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akilihakikishia bunge mwezi Februari kuwa kuna hatua za makusudi zinachukuliwa na serikali mkoani Njombe.