Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wafanyakazi Afrika Mashariki waambulia patupu
Wafanyakazi wa Afrika Mashariki hawana sababu ya kutabasamu, baada ya serikali zao kuwanyima nyongeza ya mishahara, wakati wa sherehe za kuadhimisha siku kuu ya wafanyakazi duniani
Nchini Kenya licha ya wafanyakazi kuwa wachangamfu na wenye furaha, tangazo walilosisubiri silo walilosikia.
Waziri wa leba (kazi) nchini Kenya Ukur Yattani amesema kuwa suala hilo lingali linajadilkiwa na washika dau, hali iliyowafanya wafanyakazi waliokuwa wakihudhuria sherehe hizo mjini Nairobi kuondoka wakati waziri alipokuwa akitoa hotuba hiyo ya rais.
Badala yake sherehe za siku ya wafanyakazi zilitawaliwa na miito kutoka kwa wanasiasa ambao wameilaumu serikali kwa kujaribu kuongeza mzigo kwa wafanyakazi kwa kuwatoza ushuru zaidi ili kugharamia ujenzi wa nyumba za bei ya chini.
Muungana wa waajiri nchini Kenya FKE umesusia sherehe za mwaka huu, na licha ya hayo yote wafanyakazi nchini Kenya wameiambia BBC kuwa wataendelea kuomba dua ili mashauriano kati ya serikali na vyama vya wafanyakazi yazae matunda la sivyo wataendelea kuvumilia na kusalia na mishahara yao ya sasa.
Awali Wafanyakazi wa serikali na makampuni mbali mbali walishiriki maonyesho hayo na muungano wa wafanyakazi nchini Kenya ulituma ujumbe huu kuonyesha baadhi ya wafanyakazi walioshiriki maonyesho.
Tanzania hali si tofauti na Kenya
Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema licha ya kutoa ahadi ya kuongeza mishahara ya wafanyakazi lakini bado anahitaji kujenga uchumi kabla ya kufanya hivyo.
Amesema hatua zinazochukuliwa sasa za kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ni kwa faida ya Tanzania ya leo na kesho.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 1, 2019 katika maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi (Mei Mosi) mkoani Mbeya katika uwanja wa Sokoine.
"Namshukuru sana Katibu mkuu Tucta...kwa kunikumbusha juu ya ahadi yangu niliyoitoa siku kama ya leo mwaka jana mkoani Iringa lakini niwaambie kuwa muda wangu bado haujaisha,"
Rais Magufuli amewaomba Watanzania waamini kuwa subira yavuta kheri, na akawaomba wasaidie kuujenga uchumi wa taifa lao ili uwe imara kabla ya kupandishiwa mishahara
Amewakumbusha Watanzania kuwa Serikali yake imeongeza ajira za walimu, madaktari na manesi, na akasema ahadi yake ya kutoa ajira bado haijaisha na muda wake wa utawala bado haujaisha."
Amesema miradi iliyoanzishwa itawanufaisha wafanyakazi, wakulima kwa kusafirisha mazao yao, wafugaji, wavuvi lakini inawanufaisha wafanyabiashara wote.
Uganda nako wafanyakazi hawana la kujivunia
Kwa miaka kumi, Notu na vyama vya wafanyakazi wameimba juu ya nyongeza ya mshahara, bila mafanikio - ingawa duniani siku hizi, kilio ni ujira wa kujikimu. Lakini sheria ya nyongeza ya msharara si ya kutekelezwa hivi karibuni, Waziri wa Jinsia, Nguvukazi na Maendeleo ya jamii, Janat Mukwaya ameiambia hadhara huko Agago:
'Sheria mbele yako rais, inabuni makao makuu mawili. Inamfanya waziri kutangaza mishahara ya kima cha chini, lakini pia inaifanya bodi nitakayounda kupendekeza mishahara kima cha chini. Ndio maana nilishauri kwamba tusubiri uamuzi wa baraza la mawaziri, ili kwayo tuwe na sheria unganishi - wafanyakazi, matajiri pia wana mapendekezo kwamba haiwezekani kuwa na ujira mmoja tu wa chini, bali tunapaswa kuwa na ujira wa chini tofauti-tofauti unaoendana na kazi husika.' Amesema Mukwaya.
Rais Museveni ambaye kwa muda mrefu anajulikana kuwa na ukosefu wa sera ya mishahara ya kima cha chini, hakutaja chochote kuhusu ombi la mishahara hiyo. Lakini karibuni tu, akizungumza na wawekezaji hoja ya malipo kama kawaida yake aliiweka baada ya mahitaji ya matajiri au wawekezaji:
'Ukishapata gharama ndogo ya usafiri, na gharama ndogo ya umeme, na gharama ndogo ya fedha (yaani mikopo), hapo tena unaweza kushughulikia masuala ya mshahara,'amesema Museveni.
Zaidi, Rais Museveni amepigia debe biashara na ajira, kupitia ujenzi wa miudombinu kama barabara, kuenezwa umeme vijijini, kilimo cha biashara, na umuhimu wa mashauri ya afya, mfano chanjo, kama njia imara za kuzalisha mali na raslimali nchini. Hakugusia hoja ya mishahara ya kima cha chini.