AFCON 2019: Rais wa Tanzania John Magufuli asema hakwenda uwanjani kuepuka fedheha, ushindi wa Stars umemfungua moyo wake

Rais John Magufuli

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania

Muda wa kusoma: Dakika 2

Rais wa Tanzania John Magufuli amesema kufuzu kwa timu ya taifa hilo, Taifa Stars, kwenye michuano ya AFCON kumemaliza machungu yake na ya Watanzania kwa ujumla.

Magufuli amewaalika Stars asubuhi ya leo Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwafunga Uganda 3-0 na kukata tiketi ya michuano ya AFCON baada ya kusubiri kwa miaka 39.

Kiongozi huyo amebainisha kuwa hakutarajia kuwa timu hiyo ingeibuka na ushindi hapo jana.

"Baada ya kutandikwa Lesotho huku tayari mkiwa mlishakula Shilingi milioni 50 zangunilichukizwa kweli kweli," amesema Magufuli, "siku ile wachezaji wengi wazuri hawakupangwa kwenye nafasi zao wanazostahili na wengine hawakupangwa kabisa."

Taifa Stars ilikuwa ifuzu Novemba 2018 endapo ingeifunga Lesotho nyumbani kwao lakini ikaishia kuchapwa goli moja.

"Siku moja kabla ya mchezo niliongea na (waziri wa michezo Harrison) Mwakyembe akaniambia timu iko vizuri na tungeshinda...baada ya kufungwa sikuongea nae mpaka hii leo. Inauma sana taifa la watu milioni 50 kufungwa na nchi ya watu milioni 2."

Matumaini madogo

Akiongelea mchezo wa jana, Magufuli amesema hakuenda uwanjani akiogopa kupata fedheha kwani matumaini ya kufuzu yalikuwa finyu.

Stars ilitakiwa kushinda lakini pia kusubiria matokeo ya Cape Verde dhidi ya Lesotho. Na laiti Lesotho wangeshinda basi Tanzania wasingefuzu.

"Matumaini ya kupita yalikuwa madogo...sikutaka kuja uwanjani kupata fedheha."

Ruka X ujumbe, 1
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 1

Hata baada ya Stars kuandika goli la kwanza, rais Magufuli anasema hakuamini kwamba lingedumu na kufikiria kuwa Uganda wangesawazisha.

"Mke wangu aliniambia baada ya goli kuwa leo tunashinda, nikamuuliza 'wewe unajuwa nini?'...lakini goli la pili na la tatu yakaingia na tukashinda."

Magufuli amewasifia wachezaji wote kwa mchezo mzuri na benchi la ufundi kwa kupanga kikosi kizuri.

Kutokana na ushindi huo, Magufuli amewapa zawadi ya viwanja wachezaji wote wa Stars jijini Dodoma.

Ruka X ujumbe, 2
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 2

Pia amempatia zawadi ya Shilingi milioni 5 mshambuliaji wa zamani wa Stars Peter Tino ambaye goli lake ndilo liliivusha Stars miaka 39 iliyopita.

Watanzania wanapenda furaha

"Machungu yangu mmeyamaliza jana; na bila shaka yalikuwa machungu ya Watanzania wote... Jana Watanzania wote wameweka tofauti zao pembeni wamefurahi kwa pamoja."

Amesema ameona kwenye mitandao watu wakimtaka kutoa siku moja ya mapumziko ili washerehekee, japo amesema haiwezekani lakini hyo ni ishara kubwa ya furaha.

Taifa Stars
Maelezo ya picha, Kikosi cha Taifa Stars kilichoandika historia ya kufuzu AFCON baada ya miaka 39.

"Wengine wamekunywa kweli, lakini waache walewe, wamefurahi. Najua wengine hawajarudi nyumbani jana usiku kwa kushangilia.

Magufuli amesema kwa kiwango wachezaji walichoonesha jana, na endapo hawatatawaliwa na kiburi cha kufuzu, basi Taifa Stars itafika mbali nchini Misri.

"Watanzania wanapenda sana michezo, na huumia sana tunapofungwa - sio mimi tu ambaye huwa naumia."

Ametaka ushindi wa jana uwe mwanzo mpya katika maendeleo ya michezo nchini, na kazi kubwa ifanyike kuhakikisha nchi hairudi nyuma.

"Inabidi tujiulize kwa nini tumekuwa tukifeli? Kwa nini ituchukue miaka 39? Kuna kipindi timu ya taifa ya ngumi ilibebeshwa madawa ya kulevya."