Nywila za mamilioni ya watu zafichuliwa katika Facebook

Nywila za mamilioni ya watu katika mtandao wa kijamii Facebook zilikuwa wazi na zilionekana na wafanyakazi takriban 20,000 wa kampuni hiyo, imeripotiwa.

Mtafiti wa masuala ya usalama Brian Krebs alitoa taarifa hiyo kuhusu ukiukaji wa kulindwa data ya watumizi , iliochangia nywila za watu milioni 600 kuandikwa kwa maadishi ya wazi.

Huenda nywila zilizofichuliwa ni tangu 2012, aliongeza.

Katika taarifa yake, Facebook imesema sasa imetatuwa "hitilafu hiyo" iliyochangia nywila za watu binafsi kuhifadhiwa katika mtandao wa ndani ya kampuni hiyo.

Katika ufichuzi wa kina, Krebs amesema duru ya ndani ya kampuni ya Facebook alimuambia kuhusu "mapungufu ya kiusalama" yaliochangia wabunifu au wasanifu kuunda programu tumishi zilizosajili na kunakili nywila pasi kuweka vizuizi vya kiusalama.

Akimjibu Krebs, mhandisi wa Facebook Scott Renfro amesema uchunguzi wa ndani uliidhinishwa baada ya Facebook kufichua orodha na umebaini kwamba hapakuwa na dalili zozote za matumizi mabaya ya data hizo.

Katika kauli ya wazi kwa umma, Facebook inasema iligundua hilo mnamo Januari wakati wa ukaguzi wa usalama.

Na uchunguzi huo umebaini kwamba wengi ya walioathirika ni wenye kutumia Facebook Lite, ambao huenda ukatumika katika mataifa ambako kuna matatizo ya matumizi na kasi ya mtandao.

"Tunakadiria kwamba tutawaarifu mamilioni ya watumiaji wa mtandao wa Facebook Lite na mamilioni wengine wanaotumia mtandao wa kawaida wa Facebook na maelfu ya watumiaji wa mtandao wa Instagram," kampuni hiyo imeiarifu Reuters.

Lakini imeongeza kusema itaidhinisha mfumo wa kuweka nywila mpya kwa watumiaji iwapo jopo linalo lishughulikia suala hilo litagundua ukiukaji na matumizi mabaya ya data za watumiaji.

Taarifa hii ni mojawapo ya nyingi zinazoitia kampuni ya Facebook mashakani zaidi kuhusu namna inavyopokea na kulinda data za wateja wake.

Mnamo Septemba mwaka jana, ilisema taarifa za watumiaji milioni 50 zimefichuliwa kwa makosa ya kiusalama.

Na mapema mwaka jana 2018 ilifichua kwamba data ya mamilioni ya watu zilitumika na kampuni ya data ya sayansi Cambridge Analytica.