Ajali ya Treni yaua 20 Misri

Ajali ya Treni nchini Misri

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Ajali ya Treni nchini Misri

Watu 20 wamekufa na wengine 40 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali ya treni katika njia kuu ya treni nchini humo.

Tukio hilo limetokea baada ya treni hiyo kugonga kizuizi cha kupunguza kasi, katika kituo kimoja cha treni katikati ya mji.

Ajali hiyo imesababishwa na kulipuka kwa tanki la mafuta la treni hiyo, hali iliyosababisha majengo ya jirani pia kuungua.

chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana, lakini saa chache baadaye, Waziri anayeshughulika na usafiri Hisham Arafat alijiuzulu.

Majeruhi wakisaidiwa

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Majeruhi wakisaidiwa

Watu walioshuhudia ajali hiyo wamesema wameona miili kadhaa katika janga baya kukumba nchi hiyo katika siku za hivi karibuni, hususan kwa usafiri wa treni.

Mmoja wa mashuhuda, Ahmed Mahmoud ameliambia shirika la Habari la AFP, kuwa alitoa miili ya watu 20 na kuiweka kwenye gari la wagonjwa, yote ikiwa imechomeka.

Aidha amesema kawaida treni likikaribia kituoni huja kwa mwendo wa taratibu, lakini siku hiyo lilikuwa katika kasi.

Awali vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kwamba watu waliofariki ni 25 huku wengine 50 wakiwa wamejeruhiwa.

Watu wakishuhudia ajali hiyo, nje ya kituo cha treni

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Watu wakishuhudia ajali hiyo, nje ya kituo cha treni

Waziri mkuu wa nchi hiyo Mostafa Madbouli ameapa kutoa adhabu kali kwa yeyote yule atakayehusika kupanga ajali hiyo.

Kwa upande wake, Rais wa nchi hiyo Abdul Fattah al Sisi ametuma salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na kusisitiza kuwa watu wote waliojeruhiwa watapata msaada wowote watakaohitaji.