Tanzania na Kenya zazindua kituo cha forodha cha pamoja

Rais wa Tanzania Dkt.John Magufuli na Rais wa kenya Uhuru Kenyatta wamefungua kituo cha forodha cha pamoja katika eneo la Namanga upande wa Tanzania na Kenya.

Lengo la kufungua kituo hicho cha forodha ni kuhamasisha ushirikiano katika upande wa utashi wa kisiasa , kuondoa vikwazo vya biashara kati ya nchi na nchi na uwekezaji pamoja na kuondoa vikwazo kwa mtu kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

Soko hili la pamoja limeelezwa kuwa muhimu kwa sababu nchi za Afrika mashariki zina historia moja ,jiografia na utamaduni unaofanana.

Marais wote wawili wamesisitiza undugu uliopo baina ya nchi zao, kwa kusema kwamba ndio maana ni unaweza kukuta mmasai Kenya na ukamkuta mmasai Tanzania .

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema nchi nyingi za Afrika zinarudisha nyuma maendeleo kwa sababu ya urasimu na ucheleweshwaji katika mipaka barabarani.

Na hivyo kufanya gharama za biashara kuwa juu zaidi tofauti na katika mabara mengine.

Wakati huohuo rais Kenyatta alieleza kuwa kituo hicho cha forodha kina nia ya kuwafanya watu wafanye biashara bila kupingwa na kuimarisha ushirikiano.

Vilevile alitoa angalizo kwa wale ambao wanaajiriwa kusimamia jukumu hilo wafanye kazi yao kwa uadilifu bila kupokea hongo au kuweka vikwazo kwa watu ambavyo vitawafanya washindwe kufanya biashara yao kwa urahisi.

"Na tupozungumzia mfanyabiashara tunamaanisha ni wote ,wakubwa na wadogo na tunataka kila mtu apate huduma hii" rais Kenyatta alisisitioza.

Kituo hicho ambacho kimetajwa kuwa muhimu sana kati ya nchi hizo mbili kwa kurahisisha huduma za usafiri na kuongeza chachu ya maendeleo katika nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki , Dkt. Augustine Mahiga amesema soko la pamoja hili ni hatua za awali za kuhamasisha ushirikiano na sasa wanajipanga kuwa na sarafu ya pamoja ifikapo mwaka 2020.