Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kenya: Mabadiliko katika usimamizi wa mitihani yaleta tija
- Author, Hezron Mogambi
- Nafasi, Mhadhiri, Chuo Kikuu cha Nairobi
Huku mitihani ya kitaifa ikiwa imeanza kote nchini Kenya, kuna kila dalili zinazoonyesha kuwa mfumo mpya ulioanzishwa kusimamia mitihani unaendelea kuboreshwa na kuleta nafuu.
Mabadiliko haya yaliyoanzishwa na aliyekuwa waziri wa elimu Dr. Fred Matiang'i ambaye sasa anasimamia masuala ya ndani nchini Kenya yalipingwa sana mwanzoni lakini baada ya kutumika tangu mwaka wa 2016 na kuboreshwa kila mwaka, hali inaendelea kuwa bora.
Juma hili, mtihani wa darasa la nane yaani Kenya Certificate of primary Education (KCPE) ulipoanza, kundi maalum lililoundwa na serikali linalojumuisha maafisa wakuu wa serikali kutoka wizara mbalimbali lilianza kusimamia mitihani ya darasa la nane na ule wa kidato cha nne.
Kundi hili linaongozwa na waziri wa elimu, usalama na masuala ya ndani, teknohama, na maafisa wakuu wa wizara ya elimu, Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC), Taasisi ya ukuzaji mitaala Kenya (KICD), majasusi, na maafisa wengine kutoka wizara mbalimbali za serikali.
Tofauti na miaka mingine tangu kuchukua hatamu za uongozi, Rais Uhuru Kenyatta anaonyesha kujihusisha zaidi na mitihani ya kitaifa mwaka huu kiasi cha kutembelea shule moja ya msingi jijini Nairobi kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda sawa sawa.
Rais Kenyatta alieleza kuwa serikali yake itahakikisha mfumo wa mtihani unalindwa.
Mabadiliko na hatua kali zilizoanzishwa na wizara ya elimu nchini Kenya zilitokana na matokea ya mtihani wa mwaka wa 2015 ambapo matokeo zaidi ya watahiniwa 5,000 yalifutiliwa mbali kutokana na udanganyifu.
Hali hii ilizua malalamiko nchini Kenya na kumpelekea waziri Matiang'i kuapa kuhakikisha kuwa hali katika mitihani inaimarishwa.
Waziri Matiang'i alianza kwa kuvunja bodi ya baraza la kitaifa la mitihani (KNEC) na kuwaondoa wanabodi tisa kazini.
Hatua nyingine zilikuwa ni pamoja na kuzibadilisha tarehe za mitihani kwa kuhakikisha kuwa wakati mitihani inapofanywa, wanafunzi wengine wa madarasa mengine hawapo shuleni.
Waziri Matiang'i alilifikia hili kwa kurefusha muhula wa pili kwa majuma mawili na kuufupisha muhula wa tatu kwa majuma mawili kutoka kwa muda wa majuma 12 hadi majuma 9 huku shule zikifungwa mwishoni mwa mwezi wa Oktoba.
Mbadiliko mengine yalikuwa ni pamoja kuufupisha muda wa mitihani kutoka majuma sita hadi majuma manne kama njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa mitihani inafanywa kulingana na mipango ya baraza la mitihani.
Shughuli zote ambazo si za kimasomo katika muhula wa tatu zilipigwa marufuku katika shule za Kenya.
Shughuli kama vile siku za maombi, kuwatembelea wanafunzi shuleni, likizo ya nusu muhula, michezo, sherehe za kutuzwa wanafunzi, na mikutano ya kila mwaka ya wazazi zilipigwa marufuku muhula wa tatu.
Hatua hizi zilipingwa na wadau wengi wakiwemo wanasiasa wengi lakini wizara ya elimu ilishikilia na kuzitekeleza.
Wakati huo, baadhi ya wadau walidai kuwa hatua hizo kali zisingesaidia katika kupunguza tatizo la udanganyifu kwenye mitihani ya kitaifa nchini Kenya.
Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga alilaumu hatua hizi kwa visa vya moto vilivyokuwa vimekumba shule zaidi ya 70 nchini Kenya mwaka huo.
Baada ya kutupilia mbali kupingwa kwa hatua ambazo alikuwa amezipendekeza na wadau, waziri Matiang'i alipiga hatua zaidi na kuanza kuwachuja wasimamizi wa mitihani hiyo nchini kote .
Hatua hii ilichukuliwa kwa ushirikiano na Tume ya Kuwaajiri Walimu nchini Kenya (TSC). Tume ya kuwaajiri walimu iliwachuja wasimamizi wote wa mitihani na kuhakikisha kuwa waliohusishwa walikuwa na sifa na maadili.
Mbali na hayo, walimu wakuu wa shule waliwekwa kusimamia vituo vyote vya mitihani katika hatua ya kuhakikisha kuwa wanajukumishwa zaidi katika usimamizi wa mitihani.
Walimu wakuu walitwekwa jukumu la kuichukua mitihani kutoka kwa kontena na kurejesha karatasi za mitihani kule kule baada ya mitihani kila siku.
Mwaka huu kuna kontena zipatazo 459, ambazo zinafunguliwa kila siku saa kumi na mbili asubuhi.
Zaidi, walimu wakuu wanatakiwa kurejesha karatasi za mitihani baada ya kukamilika wakiandamana na maafisa wa usalama.
Aidha, walimu wakuu wamepewa jukumu la kuhakikisha kuwa hakuna msimamizi yeyote wa mitihani atakayeiingia kwenye chumba cha mtihani akiwa na simu yoyote.
Mitihani inapoendelea, kituo maalum cha kuchunguza matumizi ya simu kinachunguza matumizi ya simu katika swala la mitihani.
Pamoja na haya, serikali ilichukua hatua na kuwalipia wanafunzi wote pesa za mitihani katika shule za serikali na kibinafsi pia kuanzia mwaka wa 2017, hatua ambayo ilipongezwa na wazazi na wadau wote nchini Kenya.
Hatua hii imesaidia sana maana baadhi ya shule za kibinafsi zilikuwa zinawapokonya pesa wazazi na kutozitoa kwa baraza la mitihani.
Hili lilipelekea baadhi ya wanafunzi kukosa kuandikishwa kwa mitihani na hivyo kukosa kuifanya.
Hatua nyingine ya mabadiliko iliyotekelezwa ilikuwa kutangazwa kwa matokeo ya mitihani mapema kuliko ilivyokuwa hapo awali ambapo matokeo yalitangazwa baada ya Krisimasi kwa KCPE na Februari mwaka uliofuta kwa KCSE.
Kulinga ana wizara ya elimu, hali hii ili ilipunguza hali ya wazazi na wadau wengine kujaribu kutumia mbinu zisizofaa kubadilisha matokeo ya wanafunzi fulani kwa sababu ya muda kati ya kumaliza kusahihisha na kutolewa kwa mitihani.
Aidha, wanafunzi waliofaulu katika darasa la nane, uteuzi wao kuingia shule za upili ulianza juma moja tu baada ya matokeo kutangazwa.
Waliofaulu kupata nafasi za kuingia shule za upili pia walipewa muda mfupi wa kuripoti kwa shule walizoteuliwa ikilinganishwa na hapo awali ambapo wanafunzi watakiwa kufika katika shule mwezi wa Februari.
Mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea katika usimamizi wa mitihani nchini yameweshwa kutokana na mfumo wa teknolojia ambao uliwahusisha wote katika mfumo wa usalama ili kuhakikisha kuwa matokeo ya mitihani yanayostahili katika shule zote nchini Kenya.
Kando na mabadiliko haya, tofauti ilivyokuwa hapo awali ambapo baraza la kitaifa la mitihani lilisimamia mitihani peke yake, tangu mwaka wa 2016, shughuli nzima ya mitihani imekuwa ikiwashughulisha maafisa wengi wa wizara mbali mbali za serikali.
Mafisa hawa ni pamoja na mawaziri na maafisa wa ngazi mbali mbali kutoka wizara ya elimu, tume ya kuwaajiri walimu(TSC), baraza la mitihani la Kenya(KNEC), Taasisi ya ukuzaji mitaala Kenya (KICD), pamoja na maafisa wa ngazi zote wa wizara ya usalama.
Mfumo mzima wa serikali ambao ulikuwa umewekwa tayari na kutumiwa kuhakikisha kuwa mitihani ya kitaifa inafanywa katika hali inayotakikana ambapo wanafunzi zaidi ya milioni 1.06 million wamekuwa wakifanya mtihani wa KCPE kabla ya wale wa shule za upili kuanza wao juma lijalo.
Srikali inapania kuhakikisha kuwa mwaka huu visa ambavyo vilipelekea kubatilishwa na kufutiliwa mbali kwa matokeo ya wanafunzi wapatao 1,200 wa kidato cha nne havitotokea tena.
Mpango mahususi serikalini umehakikisha kuwa mawaziri, makatibu na maafisa wengine wakuu serikalini wanashiriki katika kufuatilia kusimamia mitihani ya mwaka huu kwenye shule zote nchini Kenya.
Zaidi ya wasimamizi maalum 1,000 kutoka kwa wizara mbalimbali na idara za serikali wanashirikishwa katika kufuatilia jinsi mitihani ya mwaka huu inavyoendeshwa na kufanywa.
Ili kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda shwari maafisa katika wizara za elimu, tume ya kuwajiri walimu (TSC) wizara ya ndani wamekatazwa kuchukua likizo za aina yoyote ili kuhakikisha kuwa wanashiriki katika usimamizi wa mitihani ya kitaifa ambayo itamalizika Novemba 29.
Takwimu kutoka Baraza la Mitihani nchini Kenya (KNEC) zaonyesha kuwa walinda usalama zaidi ya 70,000 na zaidi ya walimu 150,000 wanashirikishwa katika kuendesha mitihani hii huku shule 222 zikilengwa zaidi kwa sababu ya visa hivyo kutokea katika vituo hivyo miaka ya nyuma.
Rais Uhuru Kenyatta ameonya wanaopanga wizi wa mitihani kuwa hawatafaulu na kuwahakikishia Wakenya kuwa mitihani italindwa ipasavyo.
Aidha, Rais Kenyatta alitembelea shule za msingi kuhakikisha kuwa mitihani inayoendelea ikifanywa katika mazingira yanayofaa.