Ikulu yafuta Kibali cha mwandishi wa CNN aliyejibizana na Rais Trump

Chanzo cha picha, Reuters
Ikulu ya Marekani imefuta kibali cha mwandishi wa habari wa kituo cha CNN saa chache baada ya majibizano kati yake na Rais Donald Trump.
Mfanyakazi wa Ikulu alijaribu kunyakua kipaza sauti kutoka kwa mwandishi Jim Acosta wakati wa mkutano wa waandishi wa habari siku ya Jumatano.
Lakini mkuu wa habari Sarah Sanders alisema kibali hicho kilifungwa kwa sababu mwandishi huyo aliwekelea mwanamke mikono yake.
Bw Acosta ameyataja madai ya Sanders kuwa ya uwongo.
Rais Trump alimtaja mwandishi huyo wa CNN kuwa mtu mbaya ajabu wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Kipi kilifanyika wakati wa mkutano?
Bw Acosta alimuuliza Trump juu ya hatua za hivi majuzi kuhusu maelfu ya wahamiaji wanaoelekea Marekani kutoka nchi za Marekani ya kati.
Mfanyakazi mwanamke wa Ikulu kisha akajaribu kuchukua kipaza sauti kutoka kwa mwandishi huyo.
"Imetosha, imetosha, Rais alimuambia Bw Acosta , kabla ya kumuambia aketi na kuweka kipaza sauti chini.
Ikulu ilisema nini?
Bi Sanders katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa twitter alisema Ikulu haiwezi kuvumilia kamwe mwandishi anayeweka mikoni yake kwa mwanamke mchanga anayejaribu kufanya kazi yake.
"Ukweli kuwa CNN inajivunia kile mfanyakazi wao alifanya sio tu cha kughadhabisha, ni mfano wa kukosa heshima kwa kila mtu, akiwemo mwanamke ambaye anafanya kazi katika uongozi huu," alisema.
Kutokana na hili , Ikulu inafuta kibali cha kuingia cha mwandishi wa habari aliyehusika hadi wakati usiojulikana.
Bw Acosta kwa njia ya Twitter alisema alizuiwa na kikosi cha kumlinda rais kuingia uwanja wa Ikulu.
Majibu yamekuwa ya aina gani?
Waandishi wa habari walipinga hatua ya kufutwa kibali cha Acosta.
CNN ilitoa taarifa kupitia Twitter ikisema marufuku hiyo ilikuwa ni ya kulipiza maswali magumu ya Jim Acosta.
"Mkuu wa habari wa White House Sarah Sander alidanganya," "Alitoa taarifa za uongo na kutaja kisa ambacho hakikutokea.












