Mitandao ya kijamii; Watanzania waendelea na harakati za kuomba kurejeshwa kwa Mo Dewji

Muda wa kusoma: Dakika 2

Ikiwa ni siku ya nne tangu kutoweka kwa bilionea mdogo zaidi barani Afrika, Mohamed Dewji, bado hakuna taarifa yeyote kutoka kwa familia au mamlaka ya usalama nchini Tanzania zinazoeleza chanzo cha kutekwa kwa bilionea huyo.

Aidha hakuna viashiria vyovyote ambavyo vimetajwa kubainisha uwepo wa bilionea huyo kuwa salama au la!

Na hata watekaji hawajatuma ujumbe wowote unaobainisha kudai kitu fulani au kuelezea nia yao ya kumteka.

Maswali ni mengi kuliko majibu ya wapi alipo bilionea huyo, huku siku na saa zikihesabiwa bila matumaini yeyote.

Kampeni zinazohamasisha kurejeshwa kwa Mo Dewji nazo ziko kwa wingi licha ya kuwa hajajulikana ni nani huyo ambaye anaambiwa amrejeshe Mo Dewji.

Ujumbe huu wa 'bringback our Mo' ukimaanisha mrejeshe Mo wetu unaenda kwa nani haswa?

Klabu ya mpira wa miguu aliyokuwa anaisimamia leo imefanya ibada maalumu kwa ajili ya kumuombea ,kiongozi wao wa Simba kurejea salama.

Kwa nini Mo hakuwa na ulinzi

Wanaomfahamo Mo wanasema ni mtu asiye na makuu wala kujikweza. Mmoja wa wafanyakazi wake wa zamani ameiambia BBC kuwa si Mo wala wanafamilia wengine wa Dewji ambao wamekuwa wakitembea na walinzi.

Mara kadhaa dewji ameonekana akipanda usafiri wa kukodi wa pikipiki, maarufu kama bodaboda ili kuwahi aendako na kupambana na foleni kali ya jiji la Dar es Salaam.

Kwaujumla, ni nadra kukuta matajiri wakijihami na walinzi nchini Tanzania tofauti na ilivyo katika miji mingine mikubwa ya Afrika mathalan Lagos, Nigeria na Johannesburg, Afrika Kusini.

Kwamujibu wa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam hali hiyo inatokana na kuwepo kwa usalama ndani ya jiji na Tanzania kwa ujumla.

Nukuu muhimu alizoziandika Mo Dewji kwenye mitandao wa kijamii

Ijumaa wiki iliyopita, aliandika: "Kila jambo unaloogopa, Mungu ana mpango wake. Mungu ni mkuu kuliko hofu uliyonayo. Ana mamlaka na maisha yako ya baadae. Kuwa na imani."

Kuhusu urafiki na mikopo, kauli yake hii: "Hamna kitu kinaua urafiki kama mikopo!"

Kuhusu utajiri na umaskini, aliweka nukuu hii aliyoitoa kwingine pengine kwenye Twitter majuzi: "Walio fukara hujaribiwa kwa umaskini, sisi nao hujaribiwa kwa kupewa zaidi ya tunavyovihitaji."

Ana ushauri pia kuhusu kufanikiwa maishani: "Vitu vingi katika maisha vinaweza kujaribu kukuondoa kwenye malengo yako lakini usipoteze mwelekeo. Mipango inaweza kubadilika lakini kamwe sio mwisho wa safari!"

Kuhusu kuwezeshwa kwa wanawake: "Kwenye Uislamu, mwanamke hahitaji kuwezeshwa na mwanaume, wameshawezeshwa na Mungu."

Kuhusu kuwa mfano bora kwa watoto: "Mtoto wako atafata mifano yako, sio ushauri wako. Hata tunapofikiri hawatuoni, wanatuona. Hata tunapofikiri hatulei, tunalea."