Rais Mnangagwa anusurika mlipuko Zimbabwe akiwa katika mkutano Bulawayo

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amenusurika baada ya mlipuko kutokea mkutano aliokuwa anauhudhuria Bulawayo.
Bw Mnangagwa amesema kitu "kililipuka inchi kama kutoka pahala nilipokuwa - lakini wakati wangu haujafika".
Video kutoka uwanja wa michezo wa White City unaonesha Bw Mnangagwa akiondoka kwenye jukwaa baada ya kutoa hotuba, mlipuko unapotokea.
Msemaji wake amesema rais huyo alinusurika bila majeraha.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Msemaji wa rais George Charamba ametoa taarifa akisema: "Kumekuwa na majaribio kadha ya kumuua rais miaka mitano iliyopita."
Gazeti la serikali la Herald limeripoti kuwa makamu wa rais Kembo Mohadi ameumia miguuni wakati wa mlipuko huo unaodhaniwa kutokana na bomu, lakini taarifa hizo hazijathibitishwa.
Maafisa wengine wakuu serikali pia wanadaiwa kujeruhiwa, sawa na walinzi wao.
Runinga ya taifa imesema Makamu wa Rais Kembo Mohadi aliumia mguuni.
Bw Mnangagwa amesema amewazuru waliojeruhiwa hospitalini na kushutumu shambulio hilo.
Ametoa wito kwa raia kudumisha umoja.

Chanzo cha picha, EPA
Makamu wa Rais wa kwanza wa Zimbabwe Constantino Chiwenga pia alipata majeraha madogo, shirika la habari la Reuters limeripoti.
Mke wake Marry pia ameumia na picha zake akitembelewa na Rais Mnangagwa hospitalini zimesambaa sana mtandaoni.
Gazeti la Herald limetaja mlipuko huo kama jaribio la kumuua rais.
Runinga ya taifa ZBC pia imesema mwenyekiti wa kitaifa wa Zanu PF Oppah Muchinguri-Kashiri, na afisa mkuu wa kisiasa Engelbert Rugeje pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa ZBC walijeruhiwa
Ubalozi wa Marekani mjini Harare umeshutumu shambulio hilo.
Rais Mnangagwa aliingia madarakani Novemba mwaka jana baada ya kuondolewa madarakani kwa Robert Mugabe aliyekuwa ameliongoza taifa hilo kwa miaka 37.
Bw Mnangagwa amekuwa akifanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika 30 Julai ambao utakuwa wa kwanza tangu kuondolewa madarakani kwa Bw Mugabe.


Mnangagwa ni nani hasa?
Bw Emerson Mnangagwa alikuwa mwandani wa Robert Mugabe kwa karibu miaka 40 tangu na hata kabla Zimbabwe kujipatia uhuru wake.

Chanzo cha picha, AFP
Alizaliwa tarehe 15 septemba mwaka 1942 kabla ya babake kuhamia nchini Zambia alikoanza harakati za mapambano.
Safari yake ya kufikia hadi kuwa rais wa Zimbabwe imekuwa ya utaratibu lakini ya kiuhakika.
Uhuru ulipopatikana, Bwana Mugabe hakumsahau rafiki yake alimchaguwa kuwa waziri wa Usalama wa kitaifa .
Lakini baadaye aliteuliwa kushikilia nyadhifa mbali mbali katika serikali ya rafiki yake na babake wa kisiasa - Robert Mugabe.
Lakini safari yake hadi kufikia kuchagulikwa kuwa naibu rais mwaka 2014 haikuwa rahisi .
Kuna wakati alipokukuwa akikosana na Bw Mugabe na mara kushushwa madaraka na mara nyegine kukumbukwa na kupandishwa tena cheo.
Kwa mfano mwaka 2004 Mnangagwa alifutwa kama katibu mkuu wa chama tawala cha ZANU-PF kwa madai eti alikuwa ananyemelea cheo cha naibu rais wa Zimbabwe.
Lakini mambo yalianza tena kumwendea vizuri pale mwaka wa 2008 alipochaguliwa na bwana Mugabe kuongoza kampeni yake ya Urais.
Inasadikiwa kwamba bwana Mugabe alipoteza duru ya kwanza katika uchaguzi huo kwa kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai.
Lakini wakati kura ya marudio ilipotangazwa tena , inasadikiwa kwamba bwana Mnangagwa aliongoza fujo na mashambulizi dhidi ya viongozi wa upinzani pamoja na wafuasi wao hivyo kumfanya upinzani wake mkuu Morgan Tsvangirai kususia kura hizo na kumfanya Mugabe achaguliwe tena kama rais.
Ni hapo ndipo nyota yake ilianza kung'ara tena
Na pale Mnangagwa alipofutwa kazi kama naibu rais wengi walitabiri kwamba, mamba huyo ameliwa na Bi Grace Mugabe, mke wa Robert Mugabe lakini sasa alirudi na kuchukua wadhifa wa rais mpya wa Zimbabwe.













