Vladimir Putin asema Urusi ina kombora 'lisiloweza kuzuiwa' na Marekani

Graphic of weaponry presented by Vladimir Putin during his annual address on 1 March 2018

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Michoro ilitumiwa kuonesha silaha hizo mpya kupitia video

Urusi inamiliki kombora ambalo haliwezi kutunguliwa na linaweza kufika pahala popote duniani, kwa mujibu wa Rais Vladimir Putin.

Amesema kombora "halipai juu sana, ni vigumu sana kulitambua likipita, lina uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia na linaweza kufika popote pale.

Aidha, njia linayofuata haiwezi kutabirika na adui, linaweza kukwepa vizuizi na kimsingi haliwezi kuzuiwa na mifumo ya sasa ya kinga dhidi ya makombora na hata mifumo inayotarajiwa kuundwa siku zijazo."

Russian President Vladimir Putin addresses the Federal Assembly at Moscow's Manezh exhibition centre on 1 March 2018

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Ilikuwa hotuba ya mwisho kwa Bw Putin kabla ya uchaguzi

Huku akitumia skrini kubwa, alionyesha video za alichosema ni kombora jipya la Urusi.

Alisema kombora hilo haliwezi kuzuiwa na mfumo wa kinga wa makombora wa Marekani barani Ulaya na Asia.

Kadhalika, ameonesha video ya ndege isiyo na rubani inayoweza kufanya kazi chini ya bahari.

Kwenye hotuba hiyo yake kwa kikao cha pamoja cha mabunge mawili, aliwahamasisha raia kupendekeza majina ya kupewa mifumo hiyo miwili ya silaha.

Ulinzi

Putin alisema uwezo wa kijeshi wa Urusi umepangwa na kustawishwa kwa lengo la kudumisha amani duniani.

Hata hivyo, amesema iwapo mtu yeyote yule atathubutu kurusha silaha za nyuklia dhidi ya Urusi, atajibiwa mara moja.

Operesheni ya kijeshi ya Urusi Syria, ambapo anasaidia Rais wa Syria Bashar al-Assad dhidi ya waasi na amesema hiyo inadhihirisha kuimarika kwa uwezo wa Urusi katika kujilinda.

Su-57

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Putin hakusema iwapo ndege zake mpya za kivita zimeanza kutumiwa Syria

Urusi iliteka Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014 wakati wa uongozi wa Bw Putin.

Kiongozi huyo amesema Urusi inalinda maslahi yake katika eneo la Arctic kwa kuimarisha miundo mbinu yake ya kijeshi eneo hilo.