Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Faru amuua mhifadhi kutoka Ulaya nchini Rwanda
Mhifadhi wa wanyama ambaye alitekeleza jukumu muhimu katika kuwarejesha tena faru weusi wa mashariki nchini Rwanda, ameuawa na mmoja wa wanyama hao.
Krisztián Gyöngyi alikuwa anawafuatilia wanyama hao katika mbuga ya taifa ya Akagera alipouawa.
Maafisa wa African Park waliotangaza kifo cha mhifadhi huyo hawakutoa maelezo zaidi, lakini faru wanafahamika sana kwa kuwakaripia na kuwashambulia watu na kuwaua kwa kutumia pembe zao.
Faru weusi wa mashariki waliangamia Rwanda karibu mwongo mmoja uliopita, lakini wakarejeshwa mwezi Mei baada ya African Parks waliwahamisha faru 20 kutoka Afrika Kusini.
Kifo cha Bw Gyöngyi, aliyetoka Hungary, ni cha "kusikitisha sana" na ni "hasara kubwa", amesema afisa mkuu mtendaji wa African Parks Peter Fearnhead kupitia taarifa.
Alikuwa mtaalamu kuhusu faru na alikuwa na tajriba ya miaka mitano.
Mhifadhi huyo alichangia sana juhudi za kuwarejesha tena faru weusi nchini Rwanda, alisema Bw Fearnhead.
Miaka ya 1970, zaidi ya faru weusi 50 waliishi mbuga ya taifa ya Akagera, lakini waliwindwa sana na majangili.
Mara ya mwisho kwa faru wa aina hiyo kuonekana nchini humo ilikuwa mwaka 2007.
African Parks waliwarejesha tena wanyama hao mbugani baada ya ulinzi kuimarishwa katika hifadhi hiyo.