Uchaguzi wa Kenya 2022: Kwa nini hatua ya Raila Odinga kupinga uchaguzi ni muhimu

Kwa mara ya tatu mfululizo Raila Odinga amepinga matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Kenya.
Kiongozi huyo wa muda mrefu wa upinzani mwenye umri wa miaka 77 amekuwa akikejeliwa na baadhi ya watu kuwa ni mtu asiyekubali kushindwa, lakini wachambuzi wanasemahatua yake yamekuwa muhimu katika kuunda na kuimarisha uendeshaji wa uchaguzi nchini Kenya, hivyo chochote Mahakama ya Juu itaamua, kesi hii itasaidia kuboresha chaguzi zinazofuata.
Baada ya shughuli ya kupiga kura kukamilila tarehe 9 Agosti, Wakenya wengi walistaajabia jinsi matokeo yalivyoanza kutiririka kwenye tovuti ya mtandaoni iliyoendeshwa na tume ya uchaguzi - mchakato ambao mara nyingi ulikumbwa na utata katika uchaguzi uliopita.
Kufikia asubuhi iliyofuata, asilimia 80 ya matokeo kutoka kwa zaidi ya vituo 46,000 vya kupigia kura kote nchini yalikuwa yametumwa.
Yalikuwa mafanikio ya ajabu kwa tume ambayo iliingia kwenye uchaguzi ikigubikwa na tuhuma ya kutoaminika - hata kama mchakato wa uthibitishaji haukulingana na kasi ya uwasilishaji wa matokeo.
Tume ya IEBC hata hivyo ilimiminiwa sifa tele kutoka Kenya na kwingineko, huku mwenyekiti wake Wafula Chebukati akivikejeli vyombo vya habari nchini - ambavyo vilihangaika na hesabu zao - kwa kutokuwa tayari "kujiandaa" kuendana na kasi ya uchaguzi.
IEBC ilikuwa ikichapisha matokeo kwa nia ya kuonyesha uwazi, ndiposa iliamua kuhimiza vyombo vya habari na umma kujumlisha matokeo wenyewe.

Chanzo cha picha, AFP
Kasi na uwazi wa uchapishaji wa matokeo ya awali uliwaacha wengine katika nchi nyingine za Kiafrika na mshangao.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Huku wakibainisha kuwa hakukuwa na kuzimwa kwa mtandao, kukamatwa kwa viongozi wa upinzani, na hakuna dalili kwamba kiongozi huyo anajipanga kung'ang'ania madarakani, walilinganisha kile walichokiona kuwa kasoro katika mifumo ya uchaguzi nchini mwao na kile walichokiona kinatokea nchini Kenya.
"Kwa kweli, tunahitaji kuchuma mti mzima kutoka kwa mchakato wa uchaguzi wa Kenya kwa sababu tulichonacho Uganda hakifai kuitwa uchaguzi," Dk Sarah Bireete alinukuliwa akisema katika kituo cha televisheni cha NBS cha Uganda.
"Asante Kenya kwa kufundisha Jumuiya ya Afrika Mashariki uchaguzi wa uwazi ni nini. Tunatumai Tanzania itazingatia hilo kaika uchaguzi ujao," Mtanzania aliandika kwenye Twitter.
"Wakenya wametuonyesha jinsi uchaguzi unavyoweza kuendeshwa kwa hadhi. Tuko kwenu Tume Huru ya Uchaguzi ya Nigeria," mtumiaji mwingine aliandika.
Msomi wa sheria za umma nchini Kenya Prof Migai Akech aliambia BBC kuwa tume hiyo ilifanya "kazi nzuri ya kusambaza matokeo kwa kasi ya juu".
"Mchakato ulikuwa wa uwazi zaidi. Hata kama kuna migogoro, unahesabu tu matokeo ya vituo vya kupigia kura."

Chanzo cha picha, Getty Images
Ufanisi katika upeperushaji matokeo haukuwa wa kubahatisha bali ni matokeo ya kesi iliyoletwa na Bw Odinga baada ya kushindwa katika uchaguzi uliopita akidai kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kushindwa kwa tume ya uchaguzi kuwasilisha matokeo yote kwa njia ya kielektroniki kama inavyotakiwa na sheria, ili kupunguza matokeo, jambo ambalo lilichangia wao kukabiliwa na hatari ya kulaghaiwa.
Katika uamuzi wa wengi, majaji wa Mahakama ya Juu waligundua kuwa "ukiukwaji haramu'' na "kasoro'' zilifanyika na kwa hivyo wakabatilisha uchaguzi wa 2017 na kuamuru urudiwe.
"Kimsingi Mahakama ya Juu ilikuwa ikisema kwamba hakukuwa na uchaguzi. Kuhesabu na kujumlisha kura havikuwa na dosari - tatizo lilihusiana na uwasilishaji na uthibitishaji wa matokeo. Kwa sababu hii ilikuwa ni ukiukaji wa sheria," alisema Prof Akech.
Kulingana na wakili Omwanza Ombati, ambaye alifanikiwa kutetea ushindi wa mbunge mwaka wa 2008 - wa kwanza tangu kurejeshwa kwa vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 1990 - ingawa Bw Odinga ana rekodi tofauti kuhusiana na changamoto zake za uchaguzi, amechangia "pakubwa" jinsi sheria ya uchaguzi inavyotumika katikauchaguzi wa urais."
Na bado Bw Odinga, ambaye sasa ameshindwa katika chaguzi tano za urais, amekuwa akidhihakiwa sana mitandaoni.
“Siamini alianza kupinga matokeo ya uchaguzi kabla sijazaliwa,” Mkenya mmoja alisema kwenye alisema, akiashiria uchaguzi wa 1997 ambapo Bw Odinga alikuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani waliyopinga ushindi wa Rais Daniel Moi wa wakati huo.
"Nadhani akishinda anaweza kupinga ushindi wake mwenyewe," mwingine alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini Bw Ombati anasema changamoto mbalimbali zilizoangaziwa na Bw Odinga na wengine zimeboresha demokrasia ya Kenya kwa njia tofauti, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya uchaguzi, kuajiri wasimamizi wa uchaguzi, na kwamba matokeo katika vituo vya kupigia kura yanapaswa kuwa ya mwisho.
Baada ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2013 kutupiliwa mbali, Bw Odinga alieleza ni kwa nini hakujutia kwenda mahakamani.
"Uamuzi wangu wa kuwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu kupinga uhalali wa uchaguzi ulikuwa kauli ya imani yangu katika uhuru wa mahakama.Tulifanya hivyo kwa ajili ya demokrasia yetu na kwa ajili ya Wakenya wote waliotaka kufanya hivyo."... kutekelezewa haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wao kupitia chaguzi huru na za haki."
Alikuwa akizungumza miaka mitano tu baada ya nchi hiyo kutumbukia katika ghasia za baada ya uchaguzi kufuatia baada ya madaiya wizi wa kura.
Ghasia hizo za kikabila zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 na kuwalazimisha wengine 600,000 kuondoka makwao. Bw Odinga pia alikuwa mmoja wa mawakili wakuu wa katiba mpya, ambayo ilipitishwa 2010.

Chanzo cha picha, Getty Images
Bw Odinga pia alikuwa mmoja wateteaji wakuu wa katiba mpya, ambayo ilipitishwa 2010.
Chini ya katiba iliyotangulia, wakati mwingine ilichukua miaka mitano - muhula kamili wa kisiasa - kusikiliza kesi ya kupinga uchaguzi, Bw Ombati alisema.
Wakati Bw Moi akiwa mamlakani, kuanzia 1978-2002, upinzani haungeweza kumpatia ilani ya kupinga ushindi wake kwa sababu walihitajika kufanya hivyo ana kwa ana.
"Katiba hiyo ilitoa hadhi maalum kwa mshindi wa uchaguzi," Bw Ombati alisema.
Majaji pia walionyesha uaminifu kwa Bw Moi - "sheria ilitumiwa kama chombo cha kutumikia udikteta wa Moi," aliongeza.
Katiba ya 2010 iliunda Mahakama ya Juu na mchakato wazi na wa haraka ambao hutoa njia kwa walioshindwa katika uchaguzi kutetea kesi yao.
Ombi la hivi punde la Bw Odinga dhidi ya kutangazwa kwa William Ruto kama rais mteule linaonekana kuwa fursa nyingine ya kusaidia kushughulikia baadhi ya masuala ambayo yameibuka wakati wa uchaguzi wa hivi majuzi, Bw Waikwa anasema.
Ingawa uchaguzi wa Kenya huo ulisifiwa na mashirika mengine ya uchaguzi kuwa ya uwazi na ya kuaminika, wanachama wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi wamedai kuwa hatua za mwisho za mchakato wa kuhakiki matokeo hazikuwa wazi, na kumshutumu Bw Chebukati kwa kuchukua hatua ya kutangaza matokeo kabla ya wote kukubaliana.
Makamishena hao waliotofautiana walimshutumu Bw Chebukati kwa kutangaza matokeo ambayo ni “upuuzi wa kihisabati unaokiuka mantiki”.
Walisema ukijumlisha asilimia ambazo kila mgombea alipokea kama ilivyotangazwa na mwenyekiti wa tume jumla yake ilifika 100.01%.
Lakini Bw Chebukati alisema hilo ni kosa la jumla na hakuwa na shaka nalo.
Mkuu huyo wa tume ya uchaguzi kwa upande wake aliwashutumu wenzake kwa kusaliti kiapo chao cha afisi na kumtaka "kusimamia" matokeo ili kulazimisha marudio ya uchaguzi.
Baada ya kesi ya awali ya Bw Odinga kusababisha kuboreshwa kwa mchakato wa uwasilishaji, sasa majaji wanapaswa kutoa uamuzi ili kuboresha hatua ya uthibitishaji, ambayo imesababisha mzozo wa sasa, mawakili wanasema.
Haya ndiyo maswali ambayo Bw Waikwa anataka Mahakama ya Juu ijibu:
- Tume ya uchaguzi inapaswa kufanya nini ikiwa mchakato wake wa uthibitishaji utakumbwa na hitilafu kubwa?
- Je, makamishena wa IEBC waapaswa kuamua kupitia kura jinsi ya kutatua hitilafu hizi na je, hatua yao ingewanyima haki wapigakura?
- Je, kuna majukumu tofauti kwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na makamishena na kama yapo ni yapi?
- Kwa mfano, kutangaza matokeo ya urais ni kazi ya tume au mwenyekiti?
- Katika uchaguzi wenye ushindani mkali, ni mambo gani ambayo Mahakama ya Juu itazingatia katika kuamua iwapo itaamuru uchaguzi mpya?
Katika muda wa siku 14 zijazo, Wakenya watajionea tamasha la mawakili bora na mahiri nchini wakikabiliana kisheria katika Mahakama ya Juu, jambo ambalo linaweza kufufua hisia kali zilizokuwepo wakati wa kampeni za urais zilizokuwa na ushindani mkali.
Lakini pia itakuwa wakati wa kusherehekea utamaduni ambao sasa umekita mizizi - kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani na sio mitaani ambayo mara nyingi yamezua ghasia mbaya siku za nyuma.
"Uwezo wa taasisi za Kenya sasa umepita utamaduni wa kisiasa," alisema Murithi Mutiga, Mkurugenzi wa Afrika wa Crisis Group.
Ima ashinde au ushindwe, Bw Odinga, ambaye amefungwa na kuteswa kwa ajili ya kupigania Kenya bora, kuna uwezekano, kwa mara ya tatu mfululizo, kutia msukumo uamuzi utakaosaidia kufanya uchaguzi kuwa wa kuaminika na wa uwazi zaidi - na huo ni mchango mkubwa katika katika kukuza na kudumisha demokrasia ya nchi.












