Joseph Boakai: Rais ajaye kuchukua nafasi ya George Weah ni nani?

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/SHUTTERSTOCK
Joseph Boakai, mgombea wa upinzani mwenye umri wa miaka 78 ambaye anaelezea umri kama "baraka", amepongezwa na kiongozi aliyeko madarakani baada ya uchaguzi wa rais uliokuwa na ushindani mkubwa nchini Liberia.
Matokeo ya hivi punde yanampa ushindi wa pekee dhidi ya nyota wa zamani wa kandanda George Weah katika kinyang’anyiro kikali zaidi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Anajulikana na wakosoaji kama "Sleepy Joe" baada ya kusambaa kwa taarifa za yeye akisinzia kwenye hafla rasmi, lakini Bw Boakai ameahidi kurejesha matumaini nchini Liberia na kuizuia nchi hiyo "kuporomoka".
Akiwa amehudumu kwa miaka 12 kama makamu wa rais chini ya Ellen Johnson Sirleaf, rais wa kwanza mwanamke Mwafrika aliyechaguliwa, anafahamu kuendesha nchi.
Ataanza rasmi majukumu yake Januari 2024 atakapoapishwa.
Bw Boakai alijitambulisha kama "gari lenye kasi lililoegeshwa katika gereji," msemo ambao ulisikika wakati wa uchaguzi wa 2017, ambapo alishindwa na Bw Weah.
Tovuti yake inaorodhesha mafanikio 58, kutoka kuanzisha vyuo vya jamii hadi kupatanisha mizozo mbalimbali kote Liberia.
Mafanikio makubwa zaidi wakati wake akiwa madarakani, hata hivyo, yalikuwa amani kufuatia karibu miaka 15 ya vita.
Kutafuta 'maisha bora'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alizaliwa Novemba 1944 katika kile ambacho wengi wamekiita "mwanzo mnyenyekevu," Joseph Boakai alikulia katika kijiji cha mbali cha Worsonga, kaunti ya kaskazini mwa Liberia, Lofa.
Wazazi wake hawakujua kusoma wala kuandika.
Bw Boakai alisoma katika shule moja nchi jirani ya Sierra Leone na kufuzu kutoka Chuo cha Afrika Magharibi, katika mji mkuu wa Liberia, Monrovia.
Kisha akamalizia shahada ya biashara katika Chuo Kikuu cha Liberia.
Katika mahojiano ya redio, Bw Boakai alisema akiwa kijana mdogo, alitembea kwa miguu kutoka Wonsonga hadi mji mkuu kutafuta "maisha bora".
Bw Boakai na mkewe Kartumu wana watoto wanne. Yeye ni Mbaptisti na shemasi wa Kanisa la Effort Baptist.
Katika miaka ya 1980 Bw Boakai aliwahi kuwa waziri wa kilimo wa Liberia chini ya Rais Samuel Doe, ambaye aliuawa kikatili mwaka 1990.
Moja ya miradi yake ya awali ilifanyika katika kijiji chake cha zamani, ambako aliusimamia na kufadhili yeye binafsi ujenzi wa barabara mpya ya maili saba (kilomita 11.2).
Amefanya kazi na wengine kujenga shule ya wanafunzi 150 na zahanati ya jamii
Bw Boakai pia alisimamia mpango wa kugatua kilimo kwa kuunda vituo vya kikanda - mradi mkuu nchini Libeŕia ambapo wengi ni wakulima wadogo wadogo.

Chanzo cha picha, Reuters
Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa 2017, Bw Boakai hakuchoka, badala yake aliazimia kujaribu tena bahati yake.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huu, si Bw Boakai wala Bw Weah aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika ili kupata ushindi, hivyo wakakabiliana katika duru ya pili ya uchaguzi.
Kampeni za Bw Boakai zililenga kilimo, huku akishutumu utawala wa Bw Weah kwa "usimamizi mbaya". Hata hivyo, Bw Weah alipuuzilia mbali madai ya Bw Boakai.
Akizungumza na BBC kuhusu malengo yake kabla ya uchaguzi huo, Bw Boakai alieleza kuwa alitaka kuangazia zaidi vita dhidi ya ufisadi, kuimarisha uzalishaji wa kilimo, kupunguza gharama ya chakula na kuboresha barabara nchini humo.
Alisema: "Watu wetu wanahitaji kuwa na nchi ambayo wanaweza kuiita yao, nchi ambayo wanaweza kuiheshimu na ufisadi umekuwa kikwazo."
"Katika siku 100 za kwanza, tutahakikisha kuwa hakuna gari litakalokwama kwenye matope nchini. Hilo litaathiri bei ya chakula na hali ya afya ya wananchi."
Rais mteule pia aliahidi uchunguzi kuhusu sababu za bei ya vyakula kuwa juu huku akisema atawasaidia wakulima.
"Uwezo wa kilimo wa nchi hii ni wa juu sana lakini hakuna kinachofanyika katika eneo hilo. Tunategemea kila kitu kinachotoka nje. Hii itabadilika. Najua tunaweza kufanya hivyo."
Bw Boakai anaelezea safari yake ya kuwa rais kwa muda mrefu, lakini anasema kwamba amedhamiria kusaidia "mamilioni ya Waliberia ambao wameachwa kukabili umaskini, magonjwa, na ukosefu wa usalama".













