Wapalestina watoroka hospitali ya Al-Shifa kwa miguu

Mamia ya watu wanaripotiwa kuondoka hospitali ya Al-Shifa, ambayo majeshi ya Israel yamekuwa yakiipekua kwa siku kadhaa.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Wapalestina watoroka hospitali ya Al-Shifa kwa miguu

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Shirika la habari la AFP limetoa picha za msafara wa Wapalestina wanaotoroka hospitali ya Al-Shifa kwa miguu.

    Mamia ya watu wanaripotiwa kuondoka katika hospitali hiyo, ambayo majeshi ya Israel yamekuwa yakiipekua kwa siku kadhaa.

    Picha zilizowasilishwa na AFP zinaonyesha wanaume, wanawake na watoto wakitembea kwenye mitaa iliyojaa vifusi huku tingatinga la kijeshi likiwa kwa nyuma.

    Mwandishi wake anasema umati huo ulijumuisha wagonjwa na majeruhi na walikuwa wakielekea kwenye ufuo wa bahari wa Gaza.

    Hapo awali tuliripoti kuwa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza ilisema kulikuwa na wagonjwa 120 na idadi isiyojulikana ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati walioachwa katika kituo hicho.

    Mkurugenzi wa hospitali amelishutumu jeshi la Israel kwa kuamuru raia kuhama, lakini IDF inasema ilisaidia kuwezesha ombi kutoka kwa mkurugenzi.

    Soma zaidi:

  3. Nestory Irankunda: Burundi inatarajia kumvutia kinda mzaliwa wa Tanzania anayekwenda Bayern Munich

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Shirikisho la Soka la Burundi bado linatumai kumshawishi Nestory Irankunda kuchezea nchi ya wazazi wake baada ya kijana huyo kukubali kuhamia kwa wababe wa Ujerumani Bayern Munich.

    Fowadi huyo wa Adelaide United mwenye umri wa miaka 17 alizaliwa katika kambi ya wakimbizi nchini Tanzania na sasa anaishi Australia, na ameiwakilisha nchi hiyo katika ngazi ya chini ya miaka 17.

    Tayari amekuwa sehemu ya kikosi cha Australia, baada ya kuwa mbadala wa Socceroos wakati wa mechi mbili za kirafiki dhidi ya Ecuador mwezi Machi.

    "Tungependa achezee Burundi lakini ana ndiye mwenye uamuzi wa mwisho - anaweza au asije kucheza kwa niaba yetu," rais wa FA wa Burundi Alexandre Muyenge aliambia BBC Sport Africa.

  4. Taylor Swift 'ahuzunika' baada ya shabiki kufariki kabla ya onyesho lake

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Taylor Swift amesema "amehuzunika" baada ya shabiki mmoja kufariki kabla ya tamasha lake huko Rio de Janeiro, Brazil, Ijumaa usiku.

    Katika taarifa yake kwenye Instagram, mwimbaji huyo wa muziki aina ya pop amesema moyo wake "umeumia sana", na kuongeza: "Alikuwa mrembo na mchanga."

    Hilo limetokea wakati halijoto ilipoongezeka katika jiji, ambalo ndilo kituo cha hivi punde zaidi kwenye Ziara ya Eras iliyovunja rekodi ya Swift.

    Nyota huyo alionekana akiwapa mashabiki chupa za maji wakati wa tamasha hilo.

    "Siamini ninaandika maneno haya lakini ni kwa moyo ulioumia kwamba nasema tulipoteza shabiki mapema usiku wa leo kabla ya tamasha langu," Swift aliandika.

    "Siwezi hata kukuambia jinsi nilivyofadhaika na hili."

    Swift alisema hangeweza kuzungumza juu ya tukio hilo akiwa jukwaani kwa sababu alihisi "kuzidiwa na huzuni" kila alipojaribu kulizungumzia.

    "Nataka kusema ninahisi hasara hii ndani ya moyo wangu ulio na huzuni hadi kwa familia yake na marafiki."

    Aliongeza kuwa hili lilikuwa "jambo la mwisho" alilofikiria lingetokea wakati akiwa ziara nchini Brazil.

  5. Takriban watoto 15 waliojeruhiwa kutoka Gaza wanaohitaji matibabu wamewasili Abu Dhabi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Madaktari wakimpokea mvulana aliyejeruhiwa wakati watoto na familia za Kipalestina zilipofika Abu Dhabi

    Ndege ya kwanza iliyobeba watoto wa Kipalestina waliojeruhiwa kutoka Gaza wanaohitaji matibabu imetua Abu Dhabi.

    Ndege hiyo ilibeba watoto wapatao 15 na familia zao, na iliwasili kutoka Misri baada ya kuruhusiwa kuvuka kuingia nchini kutoka Gaza kwa kutumia Kivuko cha Rafah.

    UAE inapanga kuleta wanawake na watoto wapatao 1,000 kutoka Gaza kwa matibabu katika hospitali zake katika siku na wiki chache zijazo.

    Tawi la Imarati la Red Crescent pia linatengeneza uwanja wa hospitali upande wa Misri wa kivuko cha Rafah kwa wale ambao ni wagonjwa sana kusafiri.

    Hospitali za Gaza zinakabiliwa na changamoto kubwa kwa sababu ya mzingiro wa Israel, ambao umesababisha ukosefu wa mafuta, maji na vifaa muhimu.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Jeshi la wanamaji la China 'limetumia mbinu hatari ya sonar' dhidi ya wapiga mbizi wa Australia

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Australia imeshutumu jeshi la wanamaji la Uchina kwa kutumia mbinu inayotumia sauti kusafiri, kuwasiliana na au kugundua vitu vilivyo juu au chini ya uso wa maji maarufu kama ‘sonar’ katika tukio kwenye maji ya kimataifa ambalo lilisababisha wapiga mbizi wa Australia kupata majeraha.

    Waziri wa ulinzi wa Australia amesema meli ya kivita ya Uchina imeamua kuchukua hatua "zisizo salama na zisizo za kitaalamu" wakati wa kukabiliana na Japan mapema wiki hii.

    Meli ya kivita ilikaribia frigate ya Australia wakati wapiga mbizi walikuwa wakiondoa nyavu za uvuvi kutoka kwa propela zake, alisema.

    Meli ya China kisha ikatumia mbinu hatari ya sonar, waziri aliongeza.

    Hii ilikuwa imesababisha "hatari kwa usalama wa wapiga mbizi wa Australia, ambao walilazimika kutoka majini", Waziri wa Ulinzi Richard Marles alisema katika taarifa yake Jumamosi.

    Wapiga mbizi hao walipata majeraha madogo ambayo huenda yalisababishwa na sonar, Bw Marles alisema.

    "Australia inatarajia nchi zote, ikiwa ni pamoja na China, kuendesha majeshi yao kwa njia ya kitaalamu na salama," alisema.

  7. Mwandishi wa Al-Shifa asema watu wengi sasa wameondoka hospitalini, Hamas inasema wagonjwa 120 bado wako

    Mwandishi wa habari ndani ya hospitali ya Al-Shifa ambaye amekuwa akizungumza na BBC wiki nzima, anasema yeye na watu wengine wengi sasa wameondoka katika eneo hilo, wakiwa wamebeba bendera nyeupe.

    Mapema wiki hii Khader Al Zaanoun alizungumza kuhusu milio ya risasi huku wanajeshi wa Israel wakipekua eneo hilo.

    "Hospitali ilihamishwa isipokuwa wagonjwa ambao hawakuweza kusonga na idadi ndogo ya madaktari," anasema.

    Anaongeza:

    Tuliinua mikono yetu na kubeba bendera nyeupe. Jana usiku ulikuwa mgumu sana. Milio ya risasi na milipuko ilikuwa ya kutisha. Tingatinga zilitengeneza mashimo makubwa kwenye yadi ya hospitali na kufagia baadhi ya majengo."

    Wakati huo huo, Wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema kuwa mamia ya watu walikimbia hospitali ya Al-Shifa kwa miguu asubuhi ya leo, kulingana na shirika la habari la AFP.

    Inasema wagonjwa 120 waliojeruhiwa wamesalia katika hospitali hiyo, pamoja na idadi isiyojulikana ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

    Hapo awali, maafisa wa afya waliambia AFP kwamba "majeruhi 450 na wagonjwa wenye magonjwa sugu" hawawezi kuhamishwa na idadi ya wafanyikazi wa matibabu wangekaa hospitalini kuwahudumia.

    BBC haiwezi kuthibitisha takwimu hizi kwa kujitegemea.

  8. Israel yatoa onyo jipya kwa raia kuondoka Khan Younis

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Israel imetoa onyo jipya kwa raia wa Gaza walioko Khan Younis kusini mwa eneo hilo kuondoka.

    Siku tatu baada ya Israel kuangusha vipeperushi vya kuwaonya watu kuondoka Khan Younis, onyo jingine la kuhama mji huo limetolewa.

    Khan Younis ndio mji mkubwa zaidi kusini mwa Gaza - ambapo mamia ya maelfu ya watu walikimbilia baada ya kuambiwa wahame kaskazini.

    Huku mzozo wa kibinadamu ukizidi kuwa mbaya katika jiji hilo lililojaa watu wengi, onyo la Israel lilidokeza kwamba operesheni za kijeshi ziko karibu.

    Mark Regev, mshauri wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliviambia vyombo vya habari vya Marekani wakati wanajeshi wa Israel watalazimika kuingia mjini humo kuharibu mahandaki ya Hamas, watu wa Khan Younis wanaweza kuhamia magharibi, "Ambapo kwa matumaini kutakuwa na mahema na uwanja hospitali”.

    "Nina hakika kwamba hawatalazimika kuhama tena" ikiwa watahamia magharibi, alisema.

    Mamia ya maelfu ya watu wa Gaza walikimbia kaskazini kuelekea maeneo ya kusini ikiwa ni pamoja na Khan Younis baada ya kuamriwa kuondoka na Israel kwa usalama wao. Lakini eneo la kusini limeendelea kuwa chini ya mashambulizi ya Israel pia.

  9. Polisi wa Kenya kupata nyongeza ya mishahara

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Malipo kwa maafisa wa polisi na magereza nchini Kenya yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 40 katika kipindi cha miaka mitatu kufuatia mapendekezo ya mapitio ya sekta ya usalama, Rais William Ruto amesema.

    Nyongeza ya mishahara inakusudiwa kuongeza ari na kuimarisha usalama.

    Ilikuwa ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na jopo kazi linaloangalia jinsi ya kuboresha ulinzi wa polisi nchini.

    Polisi wa Kenya wana sifa ya ukatili na hongo, lakini pia kumekuwa na wasiwasi kuhusu ustawi wao.

    Wanalipwa pesa kidogo na wengine wameishia kugeukia uhalifu wenyewe. Polisi kadhaa wamejiua katika miaka ya hivi karibuni na ukweli kwamba wengi wanahangaika na afya yao ya akili umetambuliwa.

    Hapo awali kumekuwa na hatua za kuongeza malipo yao lakini haijaleta mabadiliko makubwa jinsi Wakenya wanavyowachukulia.

    Habari za nyongeza hiyo ya mishahara inajiri huku Kenya ikikabiliana na mzozo wa gharama ya maisha ambao umesababisha serikali kuongeza ushuru na tozo mbalimbali.

  10. Urusi inataka kuweka msimamo mkali dhidi ya harakati za mapenzi ya jinsia moja

    .

    Chanzo cha picha, SOPA IMAGES

    Wizara ya sheria ya Urusi imewasilisha ombi kwa Mahakama ya Juu Zaidi ya nchi hiyo kupiga marufuku shughuli za kile inachokiita "vuguvugu la kimataifa la LGBT" kama lenye itikadi kali.

    Haiko wazi kama taarifa ya wizara inarejelea jumuiya ya LGBT kwa ujumla au mashirika maalum.

    Ilisema vuguvugu hilo limeonyesha dalili za "shughuli zenye itikadi kali", ikiwa ni pamoja na kuchochea "migogoro ya kijamii na kidini".

    Marufuku hiyo inaweza kumwacha mwanaharakati yeyote wa LGBT katika hatari ya kufunguliwa mashitaka ya jinai.

    Hatua hiyo yenye msimamo mkali imekuwa ikitumiwa hapo awali na mamlaka ya Urusi dhidi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu na makundi ya upinzani kama vile Wakfu wa Kupambana na Ufisadi wa Alexei Navalny.

    Mahakama ya Juu Zaidi itachunguza ombi hilo tarehe 30 Novemba.

    Marufuku hiyo ingefanya mashirika ya LGBT kutoweza kufanya kazi na kuwaweka wanaharakati na wafanyikazi katika hatari ya kufunguliwa mashtaka ya jinai, gazeti la Moscow Times lilimnukuu mmoja wa wanaharakati wachache wa LGBT ambaye bado wako ndani ya Urusi akisema.

    "Kimsingi, itahusisha mashtaka ya jinai kwa kuzingatia tu mwelekeo au utambulisho wa mtu."

    Pia unaweza kusoma:

  11. Israel kuruhusu lori mbili za mafuta kuingia Gaza kwa siku

    .

    Israel inasema itaruhusu lori mbili za mafuta kwa siku kuingia Ukanda wa Gaza, baada ya kushinikizwa na Marekani kufanya hivyo.

    Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani anasema takriban lita 140,000 za mafuta zitaruhusiwa kuingia Gaza kila baada ya siku mbili.

    Mengi ya mafuta hayo yatatumiwa na lori zinazopeleka misaada, kusaidia yale ya Umoja wa Mataifa kutoa huduma za maji na usafi wa mazingira, afisa huyo alisema.

    Zilizosalia ni za simu na huduma za mtandao, ambazo zilikuwa zimekatika kutokana na ukosefu wa mafuta.

    Siku ya Ijumaa, kampuni inayotoa mawasiliano ya Gaza ilisema kuwa huduma zake zilikuwa zikirejea baada ya kupokea mafuta kupitia Unrwa, shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina.

    Afisa huyo wa Marekani alisema Washington ilitoa shinikizo kubwa kwa Israel kufikia makubaliano haya ya mafuta.

    Mpango huo ulikubaliwa kimsingi wiki zilizopita, afisa huyo aliongeza, lakini uliahirishwa na Israeli kwa sababu mbili.

    Maafisa wa Israel waliiambia Marekani kwamba mafuta yalikuwa hayajaisha kusini mwa Gaza, na pia walitaka kusubiri na kuona kama wanaweza kujadiliana kwanza kuhusu mpango wa mateka wao wanaozuiliwa Gaza.

  12. Jude Bellingham: Kiungo wa Uingereza na Real Madrid ashinda tuzo ya Golden Boy

    Jude Bellingham akishangilia bao akiwa na Real Madrid

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kiungo wa kimatiafa wa Uingereza na Real Madrid, Jude Bellingham ameshinda tuzo ya Golden Boy 2023 - iliyotolewa kwa mchezaji bora wa chini ya miaka 21 katika ligi kuu za Ulaya.

    Mshambuliaji wa Colombia na Real Madrid Linda Caicedo, 18, alishinda tuzo ya Golden Girl.

    Bellingham, 20, alihama kutoka Borussia Dortmund hadi Real katika msimu wa joto na amefunga mabao 13 katika mechi 14 alizocheza.

    Tuzo hii inakuja baada ya kutambuliwa kama mchezaji bora wa chini ya umri wa miaka 21 katika kandanda ya dunia katika sherehe ya Ballon d'Or mwezi Oktoba.

    "Ningependa kumshukuru kila mtu ambaye amekuwa sehemu ya safari yangu kuanzia Birmingham, Dortmund na sasa Madrid. Singeweza kufikia hatua hii bila wao," alisema.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Weah rais wa kwanza kushindwa uchaguzi Liberia

    .

    Chanzo cha picha, AFP/GETTY

    Kiongozi anayeondoka madarakani nchini Liberia George Weah anaweka historia nchinni humo kwa kuwa rais wa kwanza kushindwa katika kinyang’anyiro cha kuwania muhula wa pili madarakani.

    Weah ambaye alijizolea umaarufu mkubwa nchini mwake na duniani kwa ujumla wake kwa kucheza soka katika ngazi za juu zaidi kimataifa aliingia madarakani mwaka 2018 kwa muhula wa kwanza na alikuwa akitaraji kuendelea na awamu ya pili mwaka huu kabla ya kubwagwa na mpinzani wake Joseph Bokai katika uchaguzi wa marudio uliofanyika wiki iliyopita.

    Bokai amepata ushindi mwembamba wa asilimia 50.89 ya kura dhidi ya asilimia 49.11 alizopata Weah. Ikiwa takriban kura zote zimeshahesabiwa, Bokai amemzidi Weah kwa takribani kura 28,000. Takwimu hizi zinaonesha ni kwa namna gani mchuano baina ya wawili hao ulivyokuwa mkali.

    Kwa upande wa Bokai ushindi wake pia umeweka historia nchini humo kwa kuwa mtu wa pili kukirudisha chama tawala cha zamani madarakani. Na kwa Bokai binafsi ushindi wake ni kisasi dhidi ya Weah ambaye alimshinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2017.

    Weah sasa anatarajiwa kuondoka madarakani mwezi Januari baada ya kuapishwa kwa rais mteule Bokai.

    Soma zaidi:

  14. Ushindi wa Bokai wapokewa kwa shangwe

    .

    Wafuasi wa rais mteule wa Liberia Joseph Bokai wamepokea ushindi wa mgombea wao kwa shangwe. Hata kabla matokeo ya mwisho kutangazwa, tayari walishaanza kuingia katika mitaa ya jiji kuu la Monrovia na kushangilia.

    Wafuasi wengi zaidi walikusanyika katika makao makuu ya chama chao wakiimba kwa furaha na kumtaka Rais George Weah aliyeshindwa kwenye kinyang’anyiro hicho kukubali kubwaga manyanga.

    Wengi wao walikuwa wakiimba kuwa "tumemshinda mcheza densi la Buga” – wakimaanisha Weah ambaye kampeni yake ilipambwa na kibao Buga kilichoimbwa na msanii Kizz Daniel kutoka Nigeria.

    Shangwe zaidi zinategemewa kushuhudiwa leo Jumamosi hasa baada ya Rais Weah kukubali matokeo na kumpigia simu Bokai kwa ushindi alioupata.

    Soma zaidi:

  15. Matokeo ya uchaguzi wa Liberia: Rais George Weah ampigia simu Joseph Boakai kumpongeza

    George Weah

    Chanzo cha picha, ge

    Matokeo ya uchaguzi wa Liberia: Rais George Weah ampigia simu Joseph Boakai kumpongeza Rais wa Liberia George Weah amempigia simu mpinzani wake katika kinyang'anyiro cha urais, Joseph Boakai, kumpongeza kwa ushindi wake

    Katika hotuba kwa taifa alisema "watu wa Liberia wamezungumza na tumesikia sauti yao".

    Mgombea wa upinzani anaongoza kwa kura 28,000 huku takriban kura zote zikiwa zimehesabiwa.

    Nyota wa zamani wa kandanda, Rais Weah amekuwa madarakani tangu 2018 na ataondoka uongozini mnamo mwezi Januari.

    Aliingia katika kiti cha urais akiwa na shauku, hasa kutoka kwa wapiga kura vijana, baada ya kushinda uchaguzi huo - pia dhidi ya Bw Boakai - kwa tofauti kubwa.

    Lakini dhana kwamba ameshindwa kukabiliana na ufisadi, kupanda kwa gharama ya maisha na kuendelea kwa matatizo ya kiuchumi kuliharibu sifa yake.

    Bw Weah alieleza kwa hekima kuwa ameshindwa, akianza hotuba yake ya dakika tano kwa kusema "anaheshimu sana mchakato wa kidemokrasia ambao umelifafanua taifa letu", akiongeza kuwa alizungumza na Bw Boakai ambaye alimwita "rais mteule".

    Hapo awali tume ya uchaguzi ilitangaza kuwa Bw Boakai, mkongwe wa kisiasa mwenye umri wa miaka 78 alikuwa na asilimia 50.89 ya kura, huku Rais Weah akiwa na 49.11%.

    Rais alirejelea ukaribu wa kinyang'anyiro hicho akisema "unafichua mgawanyiko mkubwa ndani ya nchi yetu" na kutoa wito kwa Waliberia "kushirikiana kutafuta muafaka... umoja ni muhimu kwa mama Liberia".

    Kipindi kirefu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo takriban watu 250,000 walifariki dunia kilimalizika miaka 20 tu iliyopita.

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 18/11 2023