Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ukraine na Urusi: Finland na Sweden zinakabiliwa na hatari gani iwapo zitajiunga na NATO?
Rais Vladimir Putin anaamini kuwa upanuzi wa Nato ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa nchi yake, hivyo Sweden na Finland kujiunga na muungano huo kunaweza kuonekana kama uchokozi.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi inasema nchi zote mbili zimeonywa kuhusu matokeo ya hatua hiyo. Rais wa zamani Dmitry Medvedev, mshirika wa karibu wa kiongozi wa Urusi, ameonya kwamba kujiunga na Nato kunaweza kusababisha Moscow kupeleka silaha za nyuklia huko Kaliningrad, eneo la Urusi kati ya Poland na Lithuania.
Ingawa hakutupilia mbali vitisho hivi, Waziri Mkuu wa zamani wa Finland Alexander Stubb alipendekeza hatari ya kweli zaidi ilikuwa ya mashambulizi ya mtandaoni ya Urusi, kampeni za kutoa taarifa potofu na uchokozi wa mara kwa mara wa anga.
Uturuki yaunga mkono ombi la Finland na Sweden kujiunga na Nato
Mwanachama wa Nato Uturuki imekubali kuunga mkono uanachama wa Sweden na Finland katika muungano huo.
Hapo awali ilikuwa imepinga pendekezo la nchi hizo za Nordic kujiunga.
Uturuki ilikasirishwa na kile ilichokiona kuwa nia yao ya kuwakaribisha wanamgambo wa Kikurdi. Sweden na Finland hazingeweza kujiunga na Nato bila msaada wa Uturuki.
Urusi inapinga vikali mataifa hayo mawili kujiunga na imetumia upanuzi wa muungano huo wa kijeshi wa kujihami wa nchi za Magharibi kama kisingizio cha vita vyake nchini Ukraine.
Lakini uvamizi wa Moscow umekuwa na athari kinyume, na njia sasa iko wazi kwa nchi hizo mbili kujiunga na Nato.
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi hizo tatu walitia saini mkataba wa pamoja wa usalama ambao ulishughulikia wasiwasi wa Uturuki.
Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg alisema Sweden ilikubali kuitikia ombi la Uturuki la kuwarejesha watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo.
Mataifa hayo mawili ya Nordic pia yataondoa vikwazo vyao vya kuiuzia Uturuki silaha, alisema Stoltenberg.
Rais wa Finland Niinisto alisema nchi hizo tatu zilitia saini mkataba wa pamoja "ili kutoa uungaji mkono wao kamili dhidi ya vitisho kwa usalama wa kila mmoja".
Waziri Mkuu wa Sweden Magdalena Andersson alisema ni "hatua muhimu sana kwa Nato".
Ofisi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ilisema "imepata ilichotaka" kutoka Sweden na Finland.
Pia unaweza kusoma kuhusu:
Mataifa hayo mawili ya Nordic yalitangaza nia yao ya kujiunga na Nato mwezi Mei, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Bw Stoltenberg alikuwa amependekeza mchakato huo ungesonga kwa haraka kwani tayari walikuwa na uhusiano wa karibu na muungano huo.
Lakini haikuwa hivyo kwani mwanachama wa Nato Uturuki alishutumu nchi hizo mbili kwa kuwalinda wanamgambo wa Kikurdi na kusema kuwa haitaunga mkono uanachama wao. Upanuzi wowote wa Nato lazima uidhinishwe na wanachama wote 30.
Uturuki kwa muda mrefu imekuwa ikiishutumu Swedeni kwa kuhifadhi kile inachokiita wanamgambo kutoka chama kilichopigwa marufuku cha Kurdistan Workers Party (PKK), lakini Sweden inakanusha.
Sasa nchi hizo mbili zimekubaliana na baadhi ya matakwa ya Uturuki, na wanamgambo watakabiliwa na msako chini ya marekebisho ya sheria za Sweden na Finland.
Iwapo Sweden na Finland zitakuwa wanachama, itamaliza zaidi ya miaka 200 ya kutojiunga kwa Sweden. Finland ilikubali kutoegemea upande wowote kufuatia kushindwa vibaya na Muungano wa Sovieti wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu.
Uungwaji mkono wa umma wa Finland kujiunga na Nato ulikuwa wa karibu asilimia 20-25 kwa miaka. Lakini tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, umepanda hadi rekodi ya juu ya asilimia 79, kulingana na kura ya maoni ya hivi punde. Nchini Sweden, asilimia 60 ya watu wanasema ilikuwa sawa kutuma maombi, juu zaidi kuliko kabla ya vita.
Bahari ya baltic kuwa 'ziwa la NATO'
Finland na Sweden tayari ni demokrasia za kisasa, zinazoegemea upande wa Magharibi na wanajeshi waliofunzwa vyema na walio na vifaa vya kutosha vinavyotumika kufanya kazi katika hali zenye changamoto nyingi za Kaskazini mwa Ulaya.
Kujiunga kwao, mara kutakapokamilika, kutafanya idadi ya nchi za Nato zinazopakana na Bahari ya Baltic kufikia nane, na kuifanya kuwa ziwa la Nato.
Maeneo mawili ya Urusi, huko St Petersburg na Kaliningrad, yatazidi kutengwa.
Finland na Sweden zinajiunga na Nato kwa sababu Urusi iliivamia Ukraine. Uvamizi huo ulikusudiwa kuisukuma Nato zaidi kutoka kwenye mipaka ya Urusi. Badala yake, imekuwa kinyume kabisa.