José Mujica: Kutoka uasi hadi rais masikini zaidi duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Jose “Pepe” Mujica, muasi wa zamani wa mrengo wa kushoto ambaye alikua rais wa Uruguay kuanzia 2010 hadi 2015, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89. Rais wa Uruguay Yamandu Orsi alitangaza kifo chake kupitia mtandao wa kijamii siku ya Jumanne. Mujica aligundulika na saratani ya koo mwaka 2024.
Mujica aliarifiwa mwezi Septemba 2024 kuwa matibabu ya mionzi yamefanikiwa kuondoa saratani hiyo, lakini daktari aliripoti mwezi Januari 2025 kwamba saratani hiyo ilirejea na kuenea kwenye ini lake.
"Kusema kweli, ninakufa," Mujica aliliambia gazeti la kila wiki la Busqueda katika kile alichosema itakuwa mahojiano yake ya mwisho. "Shujaa ana haki ya kupumzika."
Muasi wa zamani
Mujica, anayejulikana sana kwa jina lake la utani, "Pepe," alikuwa na umri wa miaka 8 babake alipokufa, na kumwacha alelewe na mama yake muuza maua. Akiwa amekasirishwa na pengo la Uruguay kati ya matajiri na maskini na kuvutiwa na Mapinduzi ya Cuba ya 1959, alitafuta mabadiliko ya kisiasa kupitia vita vya msituni.
Akiwa kijana katika miaka ya 1960, Mujica alijiunga na National Liberation Movement, kundi la waasi lililojulikana sana kama Tupamaros. Wanachama wake walilipua mabomu, wizi wa benki na utekaji nyara na mwaka 1969 waliteka mji wa Uruguay wa Pando.
Lakini Tupamaro hawakukaribia kunyakua mamlaka na kupindua serikali, na 1970 Mujica alikamatwa baada ya kurushiana risasi na polisi ambapo alijeruhiwa vibaya.
Alikaa jela na wafungwa wenzake wa Tupamaros na wakati huo ndipo walipojenga handaki lenye urefu wa futi 130 hadi nyumba moja kando ya barabara kutoka gereza hilo, jambo ambalo lilimruhusu Mujica na waasi wengine 105 kutoroka.
Lakini wengi wao walikamatwa tena. Mujica alipigwa na kuteswa, na alitumia muda mwingi katika kifungo cha upweke hadi akafanya urafiki na mchwa, vyura na panya.
Hakika, ghasia za waasi na machafuko yalidhoofisha serikali ya kiraia ya Uruguay na kuchangia kutokea mapinduzi ya 1973 ambayo yaliiingiza nchi hiyo katika udikteta wa kijeshi.
Mujica aliachiliwa mwaka 1985. Kufikia wakati huo, udikteta wa Uruguay ulikuwa umetoa nafasi kwa serikali ya kidemokrasia, na hatimaye Mujica akakubali kuingia katika siasa.
Alianza kuwa na nguvu katika siasa za Uruguay, akajiunga na chama cha Frente Amplio au Broad Front, muungano wa mrengo wa kati na wapiganaji wengine wa zamani.
Mageuzi ya sheria na uchumi

Chanzo cha picha, Xinhua
Alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 1994, akateuliwa kuwa waziri wa mifugo, kilimo na uvuvi mwaka 2005 na, miaka minne baadaye, alishinda urais.
Mujica alikua nembo hata nje ya mipaka ya Uruguay, alipoongoza nchi yake kutekeleza mageuzi ya mazingira, kuhalalisha ndoa za jinsia moja, uavyaji mimba na kulegeza vikwazo vya bangi. Pia alisisitiza matumizi ya nishati ya kijani, na kuiweka Uruguay katika mstari wa mbele katika kushughulikia mzozo wa mabadiliko ya tabia nchi.
Alisimamia ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa uwekezaji wa kigeni na kupunguza umaskini katika taifa hilo dogo la Amerika Kusini lenye zaidi ya watu milioni 3, huku akiepuka kashfa za ufisadi. Sera zake za kimaendeleo pia zilijumuisha kuwapa makazi wakimbizi wa vita kutoka Afghanistan.
"Ulikuwa urais wenye mafanikio makubwa," anasema Pablo Brum, ambaye alimhoji Mujica wakati akiandika kitabu chake The Robin Hood Guerrillas.
Rais Masikini duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Alisherehekewa kwa kuishi maisha ya kawaida hata wakati wa urais wake, Mujica aliepuka kuishi katika makazi ya rais na kubaki katika nyumba yake katika viunga vya mji mkuu wa Montevideo. Badala ya msafara wa rais, mara nyingi aliendesha gari lake la miaka mingi la Volkswagen Beetle la 1987.
Alivaa kawaida na alitoa karibu mshahara wake wote kwa misaada. Maisha yake ya kawaida yaliwafanya wengine kumwita "rais maskini zaidi duniani."
“Tunamchagua rais, na sio mfalme anayetaka zulia jekundu, na kuishi katika jumba la kifahari," alisema mwaka 2022.
Mujica alisalia kuwa mtu mashuhuri kwa umma hata baada ya kuacha urais, akihudhuria hafla ya kuapishwa kwa viongozi wa kisiasa kote Amerika ya Kusini.
Mke wake ni mpenzi wake wa muda mrefu Lucia Topolansky, aliyekutana naye wakati wakiwa waasi wa Tupamaros, ambaye pia aligeukia siasa, na aliwahi kuwa makamu wake wa rais baada ya wawili hao kufunga ndoa mwaka 2005.













