Eid ul Fitr 2025: Mambo 6 waislamu wanatakiwa kufanya kabla na baada ya sala ya Eid

Waislamu

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Saudi Arabia imetangaza Jumapili, Machi 30 kuwa Eid Al Fitr 2025.

Nchi hiyo ya Ghuba ilitangaza tarehe rasmi baada ya kamati za kidini kushuhudia muandamo wa mwezi Jumamosi.

Kwa mujibu wa matokeo ya kuonekana kwa mwezi, kamati iliona mwezi mpevu wa mwezi wa Shawaal, mwezi wa kumi katika kalenda ya Kiislamu.

Uthibitisho huo unamaanisha kuwa Jumapili ni sikukuu ya Eid Al Fitr nchini Saudi Arabia, ikitangaza mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ulioanza Machi 1.

Mtu anayefunga mwezi mtukufu wa Ramadhan anatarajiwa kumaliza mfungo kwa sala ya Eid.

Sala ya Eid ni moja ya vitendo vilivyoelezwa kama hatua ya kuabudu kuashiria mwisho wa kufunga mwezi mtukufu.

Sala ya Eid sio kwamba inatekelezwa kuashiria siku ya kuzaliwa au ushindi fulani, hapana, Eid ni kitendo cha kuabudu na kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu wetu.

Haya ni baadhi ya mambo ambayo Waislamu wanatarajiwa kufanya siku ya sala ya Eid;

Kutoa Zakat al-fitri

Zakat-ul-Fitr au Sadaqat-ul-Fitr ni kiwango fulani cha chakula kinachotolewa na waislamu katika siku chache za mwisho wa Ramadhan au siku ya 'Idd asubuhi, kabla ya kuswaliwa Swala ya 'Idd.

Kutoa Zakat al-fitr ni lazima kama ilivyoelezwa na Mtume Muhammad (S.A.W). Ni vyema kutoa Zakat al-fitr kabla ya kwenda msikitini kusali sala ya Eid.

Zakat al-fitr inatolewa kuwatakasa wale waliofunga na kuzisafisha saumu zao.

Pia inatolewa kuwalisha Waislamu masikini ili nao wawe na chakula cha kuwatosha siku ya 'Idd.

Wanawake wa Kiislamu

Chanzo cha picha, Getty Images

Kulingana na mafunzo ya Mtume Muhammed (S.A.W). Mwenyezi Mungu ametuamrisha kutoa Zakat-ul-Fitr ili mwenye kufunga ajitakase kutokamana na maneno machafu au0 vitendo vibaya na pia kuwalisha wanaohitaji.

Lakini pia inageuka na kuwa sadaqa ya kawaida kwa yule anaetoa baada ya swala ya Idd.

Hivyo basi, itakuwa rahisi ikiwa utaitoa usiku wa kuamkia Eid au siku mbili au tatu kabla ya Eid, yaani kuanzia Ramadhan 27 hasa katika mashirika au mawakala wanaokusanya sadaka kwa ajili ya wasiojiweza.

Kutolewa mapema kwa zakah hiyo itasaidia kufikia maskini mapema vizuri.

Kuoga kabla ya kwenda kusali

Inapendeza ikiwa mtu ataoga kabla ya kwenda kuswali swala ya Eid na kujitia manukato mazuri kwa wanaume.

Kula kabla ya kuswali swala ya Eid

Kula kabla ya kwenda kusali ni Sunna.

Ni katika sunnah kula tende kabla ya kwenda kuswali Eid al-Fitri au chochote kile cha halali kwasababu huo ndio uliokuwa utaratibu wa Mtume Muhammad (S.A.W).

Kuvaa nguo ambazo zitakufanya uhisi uko sawa

Ni ni utamaduni waliojiwekea Waislamu. Ni sunnah kuvaa nguo yake safi. Na kwa wanaume, sio lazima laikini inapendeza ikiwa watavaa guo nyeupe.

Eid ni siku ya furaha na kuonesha shukran kwa Allah kwa neema yake, kuwezesha muumini kufunga mwezi huo na zawadi ya usiku wa Lailatul- Qadar.

Kusema Takbir wakati unakwenda kusali Eid

Muumini akiswali

Ni utamaduni kusema takbir wakati unakwenda kusali hadi utakapofika kusali sala ya Eid na imam atakapowasili.

Muumin atasema: "Allahu Akbar, Allahu Akbar, Allahu Akbar," au aseme "Allahu Akbar, Allahu Akbar, Lailaha illahahu Wallahu Akbar, Allahu Akbar Walillahil Hamd.

Pia inasemwa hivi: "Allahu Akbar Kabira Walhamdu lillahiu kasira, Walhamdulillahi bukratan wa asila."

Kusikiliza hutba baada ya sala ya Eid

Baada ya kuswali, hutba hutolewa. Inatakuwa muumini anaketi na kusikiliza hutba wala sio kuondoka tu punde baada ya swala.

Ingawa sio wajibu, inasemekana kuwa miongoni mwa baraka ambazo Mtume Muhammad (S.A.W) alisema kuwa mtu anapata kwa kusikiliza mawaida.

Badilisha njia wakati unarejea nyumbani

Ni Sunnah kwa mtu kubadilisha njia wakati anarejea nyumbani baada ya kusali Eid kwasababu atasalimia wengine ambao hajakutaa nao.

Mama na watoto

Chanzo cha picha, Getty Images

Jamii nzima inatarajiwa kuwa katika sherehe wakubwa kwa wadogo.

Kwa sherehe zinazofanyiwa misikitini, italazimu wanawake walio katika siku zao kusimama kandokado ya msikiti kusikiliza au kutazama.

Wanawake wanatarajiwa kufunika miili yao wanapokwenda kwenye sherehe.

Na wanawake hawaruhusiwi kutangamana na wanaume wakiwa wanaswali. Yaani wanawake upande wao na wanaume upande wao.