Je, visikizi visivyotumia waya ni salama kwa afya?

vc

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa sababu ya wingi wa muziki na podikasti zinazopatikana siku hizi, haishangazi kwamba visikizi (headphones ) vimekuwa maarufu.

Kulingana na kampuni ya data ya Statista, binadamu hutumia takriban pauni bilioni moja kila mwaka kununua visikizi nchini Uingereza pekee, huku visikizi visivyotumia waya vikinunuliwa zaidi.

Ingawa watumiaji wengi wanavipenda, lakini kumekuwa na wasiwasi kwa jamii kuhusu afya. BBC umechunguza swala hili, ili kutenganisha ukweli na uwongo.

Visikizi visivyotumia waya vinatumia teknolojia ya Bluetooth kuunganisha na simu zetu. Teknolojia hiyo inatumia sumakuumeme (electromagnete) na imesababisha baadhi ya watu kuamini kuwa inaweza kudhuru akili zetu.

Kuna tafiti za kisayansi kuhusu visikizi visivyotumia waya na hatari zinazoweza kutokea. Visikizi hivi hutoa aina ya mionzi inayoitwa mionzi ya radiofrequency, ambayo hufanya kazi katika masafa ya chini sana kuliko aina ya mionzi ambayo inaweza kusababisha madhara kwa wanadamu.

Mwaka 2019, Kituo cha Utafiti wa Saratani nchini Uingereza kilisema, hakuna ushahidi wa kutosha kupendekeza kwamba visikizi vya Bluetooth vinaweza kusababisha madhara na utafiti huo haukupata uhusiano wowote wa visikizi hivyo na kuongezeka hatari ya kupata saratani.

Hata hivyo, kufikia 2025, tafiti kuhusu madhara ya visikizi visivyotumia waya kwa afya zetu bado zinaendelea.

Pia unaweza kusoma

Kiwango salama cha sauti

v

Chanzo cha picha, Getty Images

Visikizi vinavyodhibiti sauti zisizo hitajika ni uvumbuzi mpya na ni bora. Visikizi hivi vina programu maalum inayozuia kelele zisizohitajika, ikiwa ni kelele ya TV au mbwa anayebweka, hivyo kumruhusu mtumiaji kusikiliza sauti moja pekee.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Claire Benton, rais wa Chuo cha British Audiology, anasema visikizi vya aina hii vinaweza kusaidia kulinda usikivu wa watu kwani huzuia sauti nyingine na kupitisha sauti moja na nyingine zote huzuiwa, maana yake huhitaji kusikiliza kwa sauti kubwa.

"Hata hivyo, bado unapaswa kufuata ushauri kuhusu matumizi ya visikizi," Claire anasema. "Yape masikio yako mapumziko na weka kiwango cha chini cha sauti wakati wa kusikiliza.”

Anaongeza kwa kusema, “tunajua baadhi ya watu wanapenda muziki kwa sauti kubwa, lakini hilo ni hatari sana ikiwa utafanya kwa muda mrefu. Kiwango cha Decibel cha themanini na tano (85 db) kwa saa nane, ndicho kiwango salama kwa mujibu wa kanuni rasmi."

85 bd ni sawa na kelele inayotolewa na blenda wakati wa kusaga chakula. Mfano sauti ya kunong’oneza ni 20db. Sauti ya kiwango cha 40db ni mazungumzo ya kawaida.

Kelele nyingi zinaweza kuharibu usikivu wako. Kiwango cha sauti cha decibel 90 kwa muda mrefu kinaweza kusababisha tatizo la kudumu la usikivu. Kiwango cha sauti cha desibeli 140, husababisha maumivu na tatizo la kudumu la usikivu.

Utafiti wa Taasisi ya Kitaifa ya Viziwi (RNID) uligundua kuwa 58% ya watu wenye umri wa kati ya miaka 18 na 28 wana shida ya kusikia au shida inayohusiana na kusikia baada ya kusikiliza muziki kwa sauti kubwa.

Mara nyingi, madhara hayadumu, lakini kuendelea kuweka masikio yetu kwenye mazingira ya sauti kubwa kunaweza kuleta uharibifu wa kudumu.

Kulinda masikio yako

o

Chanzo cha picha, Getty Images

Sponji za kulinda masikio dhidi ya sauti husaidia kulinda masikio. Hata sponji za bei nafuu huunda kizuizi kati ya sauti ya nje na mfereji wa sikio.

Tamasha la muziki kwa kawaida lina kiwango cha sauti kati ya 90db na 100db, lakini sikio la mwanadamu linaweza kukabiliana kwa usalama na usikilizaji wa muda mrefu wa sauti isiyozidi 80db.

Saira Hussain ni mtaalamu wa sauti, ambaye ameiambia BBC: "Kwa mtazamo wa huduma ya afya, ninafurahi kuwa kuna ufahamu sasa, kuhusu kulinda usikivu wako dhidi ya kelele. Kwa hivyo, unapokwenda kwenye tamasha... hakikisha una kitu cha kulinda masikio yako."

Trevor Cox, Profesa wa Uhandisi wa Sauti katika Chuo Kikuu cha Salford, anasema, akinunua visikizi, atatafuta vile vinavyodhibiti sauti.”