Tetesi za soka Ulaya: Barcelona wamtaka Kane

Muda wa kusoma: Dakika 2

Barcelona wamemfanya mshambuliaji wa Bayern Munich na England, Harry Kane, mwenye umri wa miaka 32, kuwa chaguo lao la kwanza kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Poland Robert Lewandowski, mwenye umri wa miaka 37, majira ya kiangazi yajayo (Guardian)

Kiungo wa kati wa Crystal Palace na England, Adam Wharton, mwenye umri wa miaka 21, yuko kwenye orodha ndefu ya Chelsea katika dirisha dogo la usajili la Januari. (Teamtalk)

Aliyekuwa mshambuliaji wa Tottenham, Son Heung-min, mwenye umri wa miaka 33, amesema hataondoka Los Angeles FC kwa mkopo mwezi Januari baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu ya Soka Marekani. (Evening Standard)

Juventus wanatarajia kumshawishi kipa wa Ufaransa Mike Maignan kujiunga nao mara tu mkataba wake na AC Milan utakapoisha majira ya kiangazi, huku mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 pia akihusishwa pia na Chelsea. (Gazzetta dello Sport)

Chelsea hawajafanya mawasiliano yoyote kuhusu mshambuliaji wa Real Madrid na Brazil, Rodrygo, mwenye umri wa miaka 24, ambaye anavutiwa na Manchester City na Tottenham. (Fabrizio Romano)

Juventus wameshindwa kufikia makubaliano na mshambuliaji wa Uturuki mwenye umri wa miaka 20, Kenan Yildiz ambaye anahusishwa na vilabu vya Arsenal, Chelsea na Real Madrid kuhusu mkataba mpya, na mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamesitisitishwa. (Gazzetta dello Sport)

Real Madrid wako katika hatua za mwisho kukamilisha makubaliano na Lyon ili mshambuliaji wa Brazil mwenye umri wa miaka 19, Endrick, ajiunge na klabu hiyo ya Ufaransa kwa mkopo mwezi Januari. (Globo Esporte)

Kiungo wa England Kobbie Mainoo, mwenye umri wa miaka 20, bado anawindwa na Napoli na Leeds United, ingawa Manchester United watamruhusu tu kuondoka kwa mkopo endapo watapata mbadala wake. (Teamtalk)

Beki wa Denmark Andreas Christensen, mwenye umri wa miaka 29, anataka kubaki Barcelona lakini amesema hana "mpango mwingine kwa sasa" endapo mabingwa hao wa La Liga hawatampa mkataba mpya mwishoni mwa msimu ujao. (Tipsbladet)

Aliyekuwa beki wa Croatia Slaven Bilic amesema almanusura arejea kwa mara ya pili kama kocha wa West Ham kabla ya klabu hiyo kuamua kumteua Nuno Espirito Santo. (Talksport)