'Nadhani mimi ni mchezaji niliyekamilika zaidi kuwahi kutokea' - Ronaldo

Chanzo cha picha, Rex Features
Kila wakati, Cristiano Ronaldo angetuma ujumbe kwa daktari wa timu ya taifa ya Ureno Jose Carlos Noronha.
"Vipi Daktari, unaweza kunishauri kitabu gani naweza kusoma kinachohusu masuala ya sayansi?" Ronaldo alikuwa akiuliza.
Ronaldo ambaye alizaliwa katika kisiwa cha Madeira alikuwa tayari ameonyesha kuwa anapenda kusoma, na pia kuvutiwa na masuala ya sayansi, kwa hivyo jambo hilo halikumshangaza Noronha, ambaye amejuana na Ronaldo tangu wakati akiichezea klabu ya Manchester United.
Daktari huyo, ambaye anaheshimika sana nchini humo ambapo kuna wakati Kocha wa zamani wa United na Chelsea, Jose Mourinho alimwita "Mtu maalumu sana", na kuwa wakati alimtaja Ronaldo kama mtu "anayependa kujifunza mambo''.
"Angeniuliza iwapo kuna makala mapya ya kisayansi angesoma kuhusu lishe au mada tofauti zinazohusiana," alisema Noronha. "Ronaldo ni mtu ambaye hufanya lolote linalohitajika ili kuwa na afya njema ya kimwili na kiakili. Yeye ni mfano mzuri wa kuigwa."
Akiwa ametimiza miaka 40 ya kuzaliwa Jumatano wiki hii, Ronaldo analenga kuthibitisha kuwa maisha huanzia katika umri wa miaka 40.
"Nadhani mimi ndiye mchezaji niliyekamilika zaidi kuwahi kutoka katika hii dunia,'' Alisema kwenye mahojiano na Televisheni moja ya nchini Hispania wiki hii. "Kwa maoni yangu, nadhani ni mimi. Najitahidi kufanya kila kitu kwa njia iliyo sawa katika kandanda.
" Ikiwa unampenda Messi, Pele, Maradona, naelewa na naheshimu msimamo huo – lakini kusema kuwa Ronaldo hajakamilika… mimi ndiye niliyekamilika zaidi. Sijamuona mwingine yeyote aliye bora kuliko mimi, na nasema haya kutoka moyoni mwangu."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Amekuwa akitamani kucheza mpira kwa muda mrefu zaidi.
Mchezaji mwenzake wa zamani Costinha anakumbuka mazungumzo baina yao wakati alipoichezea kwa mara ya kwanza timu ya taifa ya Ureno mwaka 2003 dhidi ya Kazakhstan.
"Aliniambia, 'Costa, Mimi nitacheza kandanda hadi nitakapofikisha miaka 30 kisha nifanye shughuli nyengine tofauti.'"
Sio tu alitimiza ahadi hiyo, lakini alikwenda mbali zaidi na kufunga mabao mengi zaidi akiwa na miaka hiyo 30 – mabao 460 . Amefunga mengi zaidi kuliko hata alipokuwa na umri wa miaka ya 20 – alipofunga mabao 440.
Hii si kawaida, lakini hakujakuwa na jambo la kawaida kumhusu Ronaldo.
Mchezaji huyu anayechezea Al-Nassr kwa sasa anapania kuongeza kiwango chake zaidi akiwa amefikisha umri wa miaka 40 na hajaonesha dalili zozote za kustaafu hivi soka karibuni.
Licha ya mashabiki kuendelea kumkosoa zaidi kutokana na umri wake kwenye mchezo huko, bado anahisi kuna mengi ya kufanikisha.
Miongoni mwa malengo anayoyataka kufikia ni:
- Kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026 - na kushinda kombe, akiwa alisema hivi karibuni kwamba angependa "kushinda kitu kingine na timu ya taifa"
- Kufunga mabao 1,000 katika maisha yake ya soka - kwa sasa ana magoli 923
- Kufikia mechi 250 za kimataifa na Ureno - amecheza mechi 217 kufikia sasa
- Na kucheza pamoja na mwanae Cristiano Ronaldo Jr, ambaye ana miaka 14 na anacheza kwa timu za vijana za Al-Nassr.
Kwa Ronaldo, wenzake wa Ureno wamejifunza kuwa, kama anavyosema kila mara, "hakuna kinachoshindikana".
"Ronaldo hufanya mambo, lakini hufanya akijua kila sababu, na hilo ndilo linanivutia. Nina imani atacheza kwa miaka mingine moja, miwili, au hata mitatu," alisema kocha wake wa zamani wa Al-Nassr, Luis Castro.
'Amefanya nchi yetu ndogo kujulikana duniani kote'
Ili kuwa na uhakika kwamba Ronaldo angefanikisha kila alichofanya, ilikuwa vigumu kutabiri, lakini fikra hiyo ilikuwapo tangu mwanzo.
"Nakumbuka tulikuwa tumejiandaa kuingia uwanjani kukutana na Manchester United [katika mchezo wa kirafiki wa 2003 Alvalade], ambapo timu zote zilisimama kando kando - United ikiwa na majina makubwa kama [Ryan] Giggs, Paul Scholes, na [Ruud] Van Nistelrooy," alisema Joao Aroso, ambaye alikuwa kocha wa mazoezi wa mchezo wa mipira wakati huo, akizungumza na BBC Sport.
"Ungeweza kutarajia Cristiano, akiwa na umri wa miaka 18 wakati huo, angewaangalia wachezaji hao maarufu. Lakini nakumbuka nilivyomuona Cristiano, akiwa amejikita kabisa kwenye mchezo, bila kuangalia wala kutenguka - hakuwaangalia hata kidogo.
"Hilo linaashiria mengi kuhusu utu wake."
Ronaldo alitoka hapo na kwenda Manchester United, kisha Real Madrid na hatimaye Juventus, akishinda tuzo ya Ballon d'Or mara tano na kuwa mchezaji bora zaidi wa Ureno katika historia.
Kocha wa zamani wa utendaji wa Manchester United, Mick Clegg, alisema kwenye BBC Radio 5 Live's Football Daily: "Nimeangalia watu wengi maarufu tangu nifanye kazi na Ronaldo na nadhani Cristiano Ronaldo yupo katika kundi moja na Leonardo da Vinci, Albert Einstein, Isaac Newton, Nikola Tesla, na Stephen Hawking. Na wao ni nani? Wote ni mahiri kwa mpira, na yeye ana kipaji.
"Katika kikao cha kwanza katika chumba cha kufanyia mazoezi alipokuja United alisema 'Nitakuwa mchezaji bora duniani', na ilikuwa ni jambo la kushangaza. Yeye ni wa kipekee.
"Mpango wake ulikuwa kupata kila aina ya taarifa kutoka kwa wale watakaokuwa wakimfundisha na kuwa changamoto kwao. Akili yake yote ni kuhusu kuunda kitu kikubwa.
"Cristiano ni binadamu wa kawaida.
Je, inawezekana kuna watu wengine kama yeye? Nilikuwa natarajia mtu atakayekuja na kitu kama alichonacho lakini ni nadra sana."
Ronaldo ameshiriki katika zaidi ya asilimia 30% ya mechi zote za timu ya taifa.
Lakini muhimu zaidi, ameibadilisha mtazamo wa timu ambayo ilijulikana kwa kuwa na hisia za chini ambayo zilizuia mafanikio yao zamani.
"Cristiano ni wa kipekee," alisema Aroso, ambaye pia alifanya kazi na Ronaldo kama kocha msaidizi wa Ureno na sasa ni sehemu ya timu ya taifa ya Korea Kusini.
"Amekubaliana na mtindo fulani, kwa kila njia, kwa juhudi zake zisizo na kikomo za kuvunja rekodi na umri anaocheza hadi sasa.
Kama vile Maradona alivyokuwa wa kipekee, kama Pele alivyokuwa wa kipekee, kama [Lionel] Messi alivyo wa kipekee, Cristiano pia ni wa kipekee, kwa sababu zake mwenyewe.
"Kinachotaka kuangaziwa ni kwamba kwa Ureno, kuwa na mchezaji kama Cristiano ni jambo muhimu sana. Sisi ni nchi ndogo ambayo mara nyingi haina athari kubwa kimataifa nje ya soka.
"Anaruhusu nchi yetu ndogo ijulikane duniani kwa jambo kubwa - kwa sababu ya Cristiano na mambo yote mazuri anayoyasimamia."
Hakuna shaka kubwa kwamba - endapo Ureno itafuzu kwa Kombe la Dunia 2026 - atakuwa sehemu ya mashindano hayo.
Swali halisi ni kama ataweza kufika 2030, wakati Ureno itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo pamoja na nchi nyingine.
"Sina shaka [kwamba anaweza kufanya hivyo]. Ataenda kwenye lishe nyingine na kuwa hapo, awe mwembamba na mwepesi," alisema winga wa zamani, Nani, akitabasamu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kujenga himaya ya biashara
Kwa ofa inayosemekana kuwa ya kuvutia kuhusu mkataba mpya wa kuendelea na Al-Nassr, ambayo itamfanya kuwa mmiliki mwenza wa timu hiyo ya Saudi Arabia, Ronaldo hajatangaza bado uamuzi wake.
Akiwa ameshinda kombe moja tu tangu ajiunge na Mashariki ya Kati mwezi Desemba 2022 - Kombe la Mabingwa wa Waarabu mwaka 2023 - mchezaji huyu wa Ureno atazingatia hilo katika kufanya maamuzi yake, kwani anataka kuwa na uwezo wa kushindania vikombe katika miaka yake ya mwisho ya soka.
Ingawa bado haijajulikana atacheza wapi baada ya mwezi Juni, tayari anajiandaa kwa maisha yake ya baadaye.
"Niko bado mdogo, nina mipango mingi na ndoto mbele yangu, lakini semeni maneno yangu - nitakuwa mmiliki wa klabu kubwa, hiyo ni hakika," aliahidi Ronaldo wakati wa hafla ya tuzo za Globe Soccer.
Mbali na uwanjani, kesi ya madai ya kubaka ambayo imekuwa ikimkabili kwa muda mrefu - ambayo Ronaldo amekuwa akikanusha kila mara na ambayo ilitupiliwa mbali na mahakama - sasa iko nyuma yake kwa miaka kadhaa.
Ameanza kujenga himaya ya biashara na miradi katika sekta mbalimbali - ikiwa ni pamoja na vituo vya televisheni, hoteli, kliniki za upandikizaji nywele, michezo ya raketi, na nguo za ndani.
Kulingana na gazeti maarufu la kila wiki la Ureno, Expresso, Ronaldo ameongeza mara mbili idadi ya mashirika ambayo anamiliki sehemu kubwa kupitia kampuni yake, CR7 SA, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Kwa jumla, ana hisa katika biashara 21 tofauti.
"Kama mnavyojua, nina uwekezaji katika sekta mbalimbali, na kinachonisisitizia zaidi ni kuendelea mbele," alisema.
Ronaldo, ambaye chaneli yake ya YouTube ilikuwa ya kwanza kufikia watazamaji milioni moja kwa haraka zaidi - kwa sasa ana wapenzi milioni 73 - ana kaka yake mkubwa, Hugo Aveiro, na rafiki yake wa zamani wa timu ya Sporting, Miguel Paixao, miongoni mwa wasaidizi wake wakuu katika usimamizi wa biashara zake.
Mgombea katika uchaguzi wa urais wa Ureno ujao alitangaza hivi karibuni kwamba angependa kumchukua Ronaldo katika Baraza lake la Taifa endapo atachaguliwa, lakini hilo linaweza kutolewa nje kwa sasa, angalau kwa sasa.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












