Iran kununua ndege za kivita za aina ya Su-35 kutoka Urusi - unajua ni kwa nini?

Ndege

Chanzo cha picha, Getty Images

Ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na Iran umekuwa ukiimarika tangu shambulio la Februari 2022 dhidi ya Ukraine.

Marekani inaichukulia Iran kuwa 'mshirika bora wa kijeshi wa Urusi'. Iran inaipatia Moscow silaha mbalimbali, zikiwemo za mizinga na ndege zisizo na rubani (UAVs).

Waziri wa ulinzi wa Urusi anasema uhusiano wa kijeshi na Iran unazidi kukua katika mwelekeo 'chanya'. Lakini alikataa kufichua undani wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Iran imekiri kutuma ndege zisizo na rubani nchini Urusi lakini inasema 'hazitatumika katika vita vya Ukraine.'

Hata hivyo, Iran haijaficha ushirikiano wake wa kijeshi na Urusi, badala yake inapanga kufanya vikosi vyake kuwa vya kisasa kwa kutumia ndege za Urusi.

Uhusiano wa Urusi na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images

Historia ya ushirikiano wa ulinzi kati ya Urusi na Iran

Wakati Iraq ilipokuwa vitani na Iran kati ya mwaka 1980 na 1988, Umoja wa Kisovieti ulikuwa mojawapo ya wasambazaji wakuu wa silaha. Lakini mwisho wa vita hivi ulifungua mlango wa ushirikiano kati ya Urusi na Iran.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), makubaliano makubwa ya kibiashara yalitiwa saini kati ya Umoja wa Kisovieti na Iran mwaka 1989. Chini ya hili, Iran ilipaswa kupokea takribani dola bilioni 1.9 za vifaa. Kati ya 1990 na 1999, ndege za kivita, vifaru, na nyambizi pia zilitolewa kwa Iran.

Ushirikiano huu wa kiulinzi kati ya Urusi na Iran uliendelea. Hata hivyo, Urusi imekuwa makini siku zote isishutumiwe kwa kukiuka waziwazi vikwazo dhidi ya Iran. Kutokana na ushirikiano huo baina ya nchi hizo mbili ulikuwa mdogo.

Mwaka 1987, rais wa tatu wa Iran, Ali Khamenei, na naibu waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Kisovieti, Vladimir Petrovsky, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Lakini baada ya Urusi kuivamia Ukraine na kuiwekea vikwazo sekta yake ya uchumi na ulinzi, Urusi imejaribu kutumia kila fursa kupata silaha ili kuendeleza vita vyake.

Ushirikiano wa ulinzi wa Urusi ulipata nguvu tena wakati vikwazo vya utengenezaji, utengenezaji na utafiti wa makombora ya balestiki vilipokamilika mwezi Oktoba.

Katika maonesho ya Moscow mwezi Agosti, Iran ilionesha silaha zake. Bado hazijauzwa kwa nchi yoyote na iliundwa mahsusi kwa ajili ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC).

Orodha ya silaha hizi ni pamoja na makombora ya Zoheer na Ababil/Ababil OP, Shaheed-129, ndege zisizo na rubani za Shaheed-133 na ndege ya masafa marefu ya Arash.

Je, mikataba mingapi ya silaha ilitekelezwa?

Mikataba ya silaha yenye thamani ya dola milioni 200 ilitiwa saini.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hakuna taarifa rasmi ya kina inayopatikana kuhusu mikataba mingapi ya silaha imehitimishwa kati ya Urusi na Iran.

Hata hivyo, hifadhidata ya Umoja wa Mataifa ya Comtrade na data kutoka kwa Huduma ya Forodha ya Urusi hutoa maelezo yenye utata kuhusu hili.

Mwaka mmoja baada ya makubaliano ya nyuklia, 2016 ni mwaka wa rekodi katika suala la biashara ya silaha kati ya Urusi na Iran, kulingana na data ya UN ya Comtrade. Mikataba ya silaha yenye thamani ya takribani dola milioni 200 ilitiwa saini kati ya nchi hizo mbili mwaka huu.

Bado hakuna tathmini ya kina ya biashara ya silaha ya Urusi na Iran katika mwaka 2022 au mwaka huu (2023).

Kulingana na habari iliyoripotiwa na Sky News, mkataba wa kijeshi uliotiwa saini kati ya Urusi na Iran mnamo 2022 una thamani ya takribani dola milioni 1.7.

Makubaliano hayo yanaripotiwa kuwa yanajumuisha risasi na sehemu za mizinga ya T-72 iliyotengenezwa nchini Urusi.

Kupatiwa droni

Raslan Bukov anakiri kusambaza ndege zisizo na rubani za Iran kwa Urusi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na Iran uliimarika wakati Urusi ilipoanza kutumia ndege zisizo na rubani za Iran katika vita vya Ukraine. Ndege zisizo na rubani zilizotumika katika kipindi hiki ni pamoja na Shaheed-131, Shaheed-136, Mohajir-6.

UAV za Shaheed ni droni za kamikaze, zinazotengenezwa nchini Iran.

Kulingana na shirika la Airwars lenye makao yake Uholanzi, Urusi ilitumia takribani ndege zisizo na rubani 2000 za Shaheed nchini Ukraine kati ya Septemba 2022 na Septemba 2023.

Iran na Urusi zimekanusha madai kwamba Iran ilitoa ndege zisizo na rubani za Shaheed kusaidia Urusi nchini Ukraine.

Hata hivyo, mnamo Novemba 2022, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdullahiyan alithibitisha kwamba Iran ilikuwa imetuma ndege zisizo na rubani "kidogo" nchini Urusi "miezi michache kabla ya kuanza kwa vita".

Hata hivyo, Iran inaendelea kusisitiza kuwa haijaipatia Urusi silaha zozote kwa ajili ya matumizi katika vita vya Ukraine. Iran pia imesema kuwa Ukraine bado haijaweza kuwasilisha ushahidi wowote wa matumizi ya ndege zisizo na rubani za Iran.

Vyombo vya habari vya Urusi na wanablogu wanakiri kimyakimya kwamba wanapata ndege zisizo na rubani kutoka Iran.

Jarida la Wizara ya Ulinzi lilikiri mnamo Julai 2023 kwamba ndege isiyo na rubani ya Zeran-2 inaendana na droni ya Shaheed-136.

Ruslan Bukov, mtaalam wa kijeshi wa Urusi na aliye karibu na Wizara ya Ulinzi, aliiambia RBC mnamo Oktoba 2022. Katika mahojiano ya televisheni, alikiri kutoa ndege zisizo na rubani za Iran kwa Urusi.

Iran kununua ndege za kivita aina ya Su-35 kutoka Urusi

Iran yatia saini makubaliano ya kununua ndege za kivita aina ya Su-35 kutoka Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images

Aidha, Iran inataka kufanya zana zake za kijeshi kuwa za kisasa. Hasa, inaonesha nia ya kuboresha ndege za kijeshi zilizopitwa na wakati kwa msaada wa teknolojia ya Kirusi.

Kununua ndege za Urusi ni moja ya sababu kwa nini Iran ichukue hatua isiyo ya kawaida ya kuchangia vita nje ya Mashariki ya Kati.

Iran ilithibitisha mwezi Machi kuwa imetia saini mkataba wa kununua ndege za kivita za aina ya Su-35 kutoka Urusi.

Lakini mchakato huu umechelewa. Wakati huo huo, Iran ilipokea ndege kadhaa za mafunzo aina ya Yak-130 zilizotengenezwa na Urusi mwezi Septemba.

Baada ya yote, naibu waziri wa kwanza wa ulinzi wa Iran, Mehdi Farahi, alisema mwezi Novemba kwamba mkataba wa helikopta za mashambulizi aina ya Mi-28, ndege za kivita za aina ya Su-35 na ndege za mafunzo ya Yak-130 kutoka Urusi umekamilika na mchakato wa kuziagiza unaendelea. .

Kupata ndege hizi itakuwa ni mafanikio makubwa kwa Iran. Hata hivyo, inadhaniwa kuwa itakuwa ya kuvutia kuona ni ndege ngapi ambazo Urusi iko tayari kutoa kwa Iran huku kukiwa na ongezeko la mahitaji ya Iran katika vita vya Ukraine.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga