Kwa nini Iran ni ya kwanza kutajwa unapozungumzia vita vya Gaza?

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya Hamas kufanya mashambulizi yake ya kushtukiza dhidi ya Israel, Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, alijitokeza na kusifu kile alichokiita "tetemeko la ardhi baya" kwa Israel, na kusema, "Tunabusu mikono ya wale waliopanga mashambulizi."
Lakini kiongozi mkuu pia alikuwa mwepesi kukanusha kuhusika kwa Iran katika shambulio hilo - ambalo liliua watu 1,200 na wengine karibu 240 wakishikiliwa mateka - na tangu wakati huo, Israeli imefanya mashambulizi ya anga na ya ardhini huko Gaza, na kuua Wapalestina zaidi ya 11,000, kulingana na Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza
Iwapo tutatilia maanani kukanusha kwa Iran kuhusika kwake na kile kilichotokea Oktoba 7, swali linasalia kuwa: Kwa nini vyombo vikuu vya habari na vya kijamii vinaitaja Iran kila mara pamoja na Hamas vinapozungumzia shambulio hilo?
Pengine mantiki nyuma ya hili ni wazi na ya moja kwa moja: Uungaji mkono usioyumba wa Iran kwa kile kinachoitwa mhimili wa upinzani
Mhimili wa upinzani ni muungano wa makundi yanayoipinga Israel na ushawishi wa Marekani katika Mashariki ya Kati. Muungano huo unajumuisha Hamas, Hezbollah ya Lebanon, wanamgambo nchini Iraq, na kundi la Houthi nchini Yemen.
Iran - ambayo iko chini ya vikwazo vya kimataifa kutokana na malengo yake ya nyuklia na ukiukaji wa haki za binadamu - inakabiliwa na changamoto za kiuchumi na kisiasa. Katika juhudi zake za kulinda maslahi yake, nchi hiyo ililaumiwa kwa kutumia washirika na mawakala wake dhidi ya wapinzani wake wa kieneo, huku Hezbollah na Hamas zote zikinufaika na uungaji mkono wa Iran ulioelekezwa dhidi ya Israel.
Uhusiano wa Israel na Iran katika historia

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel na Iran hawakuwa daima maadui wakubwa. Kabla ya kuzuka Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu, Iran ilikuwa mshirika wa kimkakati wa Israel.
Lakini hali ilibadilika baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na kurejea kwa Ayatollah Khomeini madarakani, na Iran ikageuka kuwa dola ya kitheokrasi yenye maneno ya chuki dhidi ya Israel.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Suala la Palestina haraka likawa sehemu muhimu ya wasiwasi kwa nchi kwani lilipata umaarufu mkubwa, sio tu kati ya duru za Kiislamu bali pia ndani ya jamii za wasomi na wale wa mrengo wa kushoto.
Siku sita tu baada ya kuzuka Mapinduzi ya Kiislamu, Yasser Arafat, kiongozi wa wakati huo wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina, alikuwa kiongozi wa kwanza wa mtu wa ngazi ya juu raia wa kigeni kukutana na Ayatollah Khomeini na serikali ya mpito ya Tehran.
Saa chache tu baada ya Arafat kukutana na serikali mpya, Iran ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Israel
Licha ya kuwapenda Wapalestina, haikuchukua muda mrefu kabla ya Iran kukubali msaada wa kijeshi kutoka Israel. Katika miaka ya mwanzo ya Vita vya Iran na Iraq vilivyodumu kuanzia mwaka 1980 hadi 1988 - Israel ilitoa misaada mbalimbali isiyo rasmi kupitia wengine.
Muungano huu haukutarajiwa, lakini kwa Israeli kuendelea na vita kunamaanisha kuweka Iran na Iraq kuwa na shughuli za kufanya na kila mmoja wao.
Lakini muungano huu ulikuwa wa kipekee katika mzunguko usio na mwisho wa uchokozi, vitisho, na shutuma za pande zote. Katika miaka ya 1980 na 1990, Israel na Marekani ziliishutumu Iran kwa kuhusika na mfululizo wa mashambulizi mabaya ya mabomu, ambayo Iran ilikanusha. Iran imesema kuwa Israel ilihusika na mauaji ya wanasayansi kadhaa wa nyuklia wa Iran, na nchi hizo mbili zinaendelea kulaumiana kwa mashambulizi ya mtandaoni yanayoendelea
Je, uhusiano wa Iran na Hamas ni upi

Chanzo cha picha, Getty Images
"Hamas" ilianzishwa mwaka 1987, na vuguvugu hilo la Wapalestina limedhibiti Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2007, ambapo mara kwa mara hurusha makombora yanayolenga miji ya Israel, na inachukuliwa kuwa "shirika la kigaidi" na Marekani, Uingereza na nchi nyingine.
Katika kipindi chote cha miaka ya 1990 na 2000, Iran ilichukua nafasi muhimu katika kuunga mkono Hamas, ikisukumwa hasa na chuki ya pamoja dhidi ya adui yuleyule badala ya itikadi za kidini au mitazamo ya kisiasa ya pamoja. Hamas inafuata Uislamu wa Kisunni huku utawala wa Iran ukiegemea Uislamu wa Kishia
Mnamo 2012, uhusiano kati ya Hamas na Iran ulizidi kuwa mbaya. Wakati vuguvugu lilipokataa kumuunga mkono Rais wa Syria, Bashar al-Assad, mshirika wa karibu wa Iran, huku kukiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake. Kwa kujibu, Iran ilisitisha msaada wa kifedha kwa Hamas na kupunguza uungaji mkono wake kwa shughuli za silaha za kundi hilo lenye kujihami.
Mnamo mwaka wa 2015, mgawanyiko huo uliongezeka kwa sababu ya maelewano yanayoonekana kati ya Hamas na Saudi Arabia, adui wa zamani wa Iran.
Iran imewaunga mkono waasi wa Kishia wa Houthi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen, na kuwagonganisha na Saudi Arabia, ambayo inaunga mkono vikosi vya serikali huko.
Tangu mwaka 2017, hasa kwa baadhi ya nchi za Kiarabu kuimarisha uhusiano wao na Israel, Iran na Hamas wamejaribu kufanya juhudi zaidi kurejesha uhusiano katika nchi yao ya awali, ambayo ni kweli imetokea
Sasa, Marekani, mshirika wa Israel, inasema ingawa hakuna ushahidi wa kuhusika moja kwa moja kwa Iran katika shambulio la Oktoba 7, inaamini kuwa Iran ilichukua jukumu la kufadhili tawi la kijeshi la Hamas kwa miaka mingi.
Je, ni uhusiano gani uliopo wa Hezbollah na mzozo wa sasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Hezbollah - kundi la waasi la Kishia lenye makao yake makuu nchini Lebanon kwenye mpaka wa kaskazini wa Israel - ni nguvu nyingine muhimu katika kile kinachoitwa mhimili wa upinzani. Iran ilichukua jukumu kuu katika kuundwa kwake, na Marekani, Uingereza na nchi nyingine zinachukuliwa kundi hilo kama "shirika la kigaidi."
Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, uungaji mkono wa chama hicho kwa Iran umeendelea kuwa thabiti na usioyumba, huku Katibu Mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah akitangaza hadharani uaminifu wake kwa Kiongozi Mkuu wa Iran.
Hezbollah ina nguvu na zana za silaha za teknolojia ya juu zaidi kuliko Hamas, na imeshiriki katika ujanja mwingi wa kisiasa katika Mashariki ya Kati.
Inasemekana uwezo wa kijeshi wa chama hicho katika masuala ya mafunzo na vifaa ni bora kuliko baadhi ya majeshi ya kawaida katika eneo hilo.
Mwaka 2006, wakati Hezbollah ilipopigana vita vyake vikubwa na Israel, wengi walishangazwa na nidhamu ya kijeshi ya chama hicho na uwezo wake wa kurusha makombora.
Katika wiki chache zilizopita, ubadilishanaji wa silaha kati ya Hezbollah na Israel umeongezeka.
Je, Iran itaingilia kati mgogoro kati ya Israel na Hamas?
Mwanzoni mwa mwezi huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani siku ya Jumatatu), James Cleverley, katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran, Hossein Amir Abdollahian, aliiomba Iran itumie ushawishi wake dhidi ya makundi yenye silaha katika eneo hilo ili kuzuia kuongezeka kwa mvutano unaozunguka vita vya Gaza.
Wiki moja baada ya shambulio la Oktoba 7, na huku kukiwa na shutuma nyingi za kimataifa kwa vitendo vya Hamas, Hussein Amir Abdullahian alikutana na Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, nchini Qatar
Waziri wa Iran alichukua fursa hii kuionya Israel kwamba iwapo itaendelea na mashambulizi yake ya mabomu huko Gaza, kunaweza kuwa na athari mbaya isiyotarajiwa katika eneo hilo.
Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran ameunga mkono onyo hilo na kusema: "Majeshi ya upinzani yataishiwa na subira, na hakuna atakayeweza kuwazuia."












